Wednesday 6 January 2016

AINA ZA FIDIA UNAZOWEZA KULIPWA SERIKALI INAPOTWAA ARDHI YAKO.



Image result for BOMOABOMOA
NA  BASHIR  YAKUB - 

Kawaida  serikali  hutwaa  maeneo. Huhamisha  wahusika  wamiliki  na  kuchukua  eneo  kwa  malengo  maalum  yaliyokusudiwa. Yaweza  kuchukuliwa  nyumba yako, kiwanja,au  hata  shamba. Mara  kadhaa  serikali  hufanya  hivi  panapo  mahitaji  maalum  ya shughuli  za  umma  kama  ujenzi  wa  miundombinu  kama  barabara  reli, huduma za  umeme  na  maji,  ujenzi  wa  shule vyuo, vituo  vya  afya  na  miradi  mingineyo  kwa  manufaa  ya umma.

1.FIDIA  YA  ARDHI  NININI.

Fidia  ya  ardhi  ni  stahili  ambayo mwenye  ardhi  mmiliki  anatakiwa  kupata  pale  ambapo  ardhi  yake  inatwaliwa/inachukuliwa  na  serikali  kwa  matumizi  maalum  ya  serikali/umma.

2.  JE UNAWEZA  KUIKATALIA  SERIKALI   ARDHI  YAKO  ISICHUKULIWE ? .

Serikali  inapotaka  kumhamisha  mwananchi na  kuchukua ardhi  yake kupisha mradi wa umma  kisheria  mwananchi   hana  uwezo  wa  kukataa. Hii  ni  kwasababu  ardhi  yote  ni  mali  ya  umma  ambayo  mdhamini  wake  mkuu  ni  serikali kupitia  mamlaka  ya  rais. Hivyo  tunaweza  kusema  kuwa  ardhi  ni  mali  ya umma inayodhaminiwa na serikali/rais.

Kwa  hiyo  mwananchi  hawezi  kuikatalia  serikali kuchukua  mali   hiyo  isipokuwa  kisheria  ni  kuwa  anayehamishwa  apewe  fidia.  
Hata  ukiamua  kwenda  mahakamani  kupinga  kutwaliwa  ardhi  hautapinga  kuwa  serikali  isichukue  ardhi yako  kabisa, isipokuwa  utapinga  kuhusu  fidia,  labda  fidia  ndogo  au  utaratibu  mbovu  uliotumika  kukadiria  fidia, riba n.k.

Labda  kuwe  na  uonevu  au  hila  katika  kutaka  kutwaliwa  ardhi  yako  au namna  nyingineyo  ya  nia  ovu  ndipo  unaweza  kupinga  ardhi  yako  kutwaliwa.  Lakini  haitawezekana  kupinga  hatua  hiyo  ikiwa  kuna  malengo  maalum  ya  kutwaa  ardhi  kwa  ajili  ya  shughuli  za  umma.

3.  ZIJUE AINA  ZA  FIDIA.

Watu  wengi  wamekuwa  wakijua  kuwa  fidia  ni  pesa  tu. Linapokuja  suala  la fidia ya  ardhi watu  hudhani  kinachotakiwa  kutolewa  na  serikali  ni pesa. Hili  si  kweli  kwakuwa fidia  haimaanishi  pesa  pekee  kama  tutakavyoona  hapa  chini.

( a )  Fidia  ya  pesa.  Hii  ni  fidia  inayojulikana  sana  na  ni  aina  ya  fidia  ambayo  imekuwa  ikipendwa  mno  na  ndiyo aina  ya  fidia  ambayo  hutumiwa  na  serikali  mara  kwa  mara  kuliko  fidia  nyinginezo. Maeneo  ya  watu  hukadiriwa  na  hulipwa  pesa  kutokana  na  bei  ya  soko  ya  eneo  husika.Imefanyika  hivyo  sehemu  nyingi  na  inaendelea  kufanyika.

( b ) Fidia  ya  ardhi. Hii  ni  aina  ya  fidia  ambayo  huhusisha  kupewa ardhi.  Inachukuliwa  ardhi  yako  kwa  ajili  ya  shughuli  za  umma  unapewa  ardhi  nyingine  kufidia  iliyochukuliwa. Muhimu  ni  kuwa  usipewe  ardhi  nyingine  kama  fidia  ambayo  hadhi  yake,  ubora  wake, matumizi  yake,  na  ukubwa  wake  uko chini  ya  ile  ya  kwako  iliyochukuliwa.

Unatakiwa  upewe  ardhi  yenye  ubora  uleule, ukubwa  uleuleule, matumizi  yaleyale  na  hadhi  ileile. Hadhi, ubora  na  ukubwa  vinaweza  kuzidi  lakini  visipungue.  Ikiwa  utapewa  ardhi  kama  fidia  na ikawa  chini  ya  ile  kiukubwa,ubora  na  hadhi  basi    unayo  malakamiko  ya  msingi  ambayo  utayapeleka  kwa  Kamishna  wa  ardhi  au  mahakamani  ili  kupata  kiwango  cha  haki  kilichoporwa.

Isipokuwa  hautaenda  mahakamani  kulalamika  kuwa  umepewa  ardhi  kubwa  zaidi  na  yenye  ubora  zaidi  kuliko  ile  ya  kwako  iliyochukuliwa.

( c  ) Fidia  ya  jengo. Badala  ya  pesa  unaweza  kupewa  jengo  au  majengo  yanayofanana  na  lile  ambalo  limechukuliwa  au  kubolewa  kupisha  mradi wa  umma.  Kama  nilivyoeleza  hapa  juu  kuwa   utatakiwa  kupewa  jengo  lenye  ubora,hadhi  na  ukubwa  uleule.  Malalamiko  utakuwa  na  haki  nayo  ikiwa  umepewa  jengo  lililo chini  ya  ubora  na  hadhi  ya  lile lililochukuliwa.

( d )  Fidia ya  kutumia  mali  za  umma.  Hii  ni  aina  ya  fidia  ambapo baada ya   kuchukuliwa  ardhi  yako  kwa  mfano  jengo  ambalo  ulikuwa  ukipokea  kodi  unapewa  jengo  jingine   si kwa  kulimiliki  bali  kulitumia   ambapo  unaweza  kuwa  ukichukua  kodi  kama  mmiliki  kwa  muda  fulani  utakaokubaliwa  mpaka  hapo  kiwango  cha  pesa  ambacho  ungelipwa kama  fidia  kitaisha.  

Hii  pia  hutumika   kufidia  mashamba   ambapo  utapangiwa  kutumia  shamba  la  umma  kwa  muda  fulani  kufidia  la  kwako  lililochukuliwa.

( e ) Fidia  ya  miche  na  mimea.  Hii  hutolewa  panapo  uharibifu  wa  miche  na  mimea  katika  eneo  lako. Yawezekana  eneo  lililochukuliwa  lilikuwa na   miche  na  mimea  na  imeharibiwa.  Si  lazima  upewe  pesa  unaweza  pewa  miche  na  mimea  yenye  hadhi  na  ubora  kama  wa  ile  ya  kwako. Hii  hujumuisha  fidia  ya  mazao  na  nafaka  pia.


( f) Fidia  kwa  makubaliano.  Hii  ni  aina  ya  fidia  ambapo  mdai  na  kamishana  wa  ardhi  hukaa  meza  ya  mazungumzo  na  kukubaliana  aina  ya  fidia  inayofaa  kwa  kiwango  cha  ardhi, jengo  lililochukuliwa  kupisha  mradi. Hapa  fidia  inaweza  kuwa  yoyote  kutegemea  na  makubaliano ya  pande  hizo  mbili.
Haya  yote  ni  kwa  mujibu  wa sheria  ya  ardhi  ya 1999 na  sheria  ya  ardhi  ya  vijiji ya 1999.                NYUMBA  HII  INAUZWA  BUNJU "B".



1. Ina vyumba 3, kimoja master na fremu ya duka mbele.
2. Ipo ndani  ya  fensi  kubwa sana.
3. Umeme, maji vimo ndani, jiko na public toilet.
4. Ipo Bunju B  mkono  wa kulia ukitokea mjini.
5. Eneo zuri tulivu kwa makazi.
6.Ni nyumba yenye eneo kubwa.
7. Mita chache kutoka  barabara  kuu ya  Bagamoyo .
8. Bei milioni  90 inapungua .
0784482959.








0 comments:

Post a Comment