Friday 11 December 2015

JE KILA UNACHOKUBALIANA NA MTU NI MKATABA KISHERIA ?.


Image result for MKATABA

NA  BASHIR  YAKUB -

Makubaliano  ni  sehemu  ya  maisha  yetu  ya  kila  siku.  Shughuli  zetu  za  kila siku  hutegemea  makubaliano.   Ukimkuta  mtu  anabeba  zege  kwa  ajili  ya  ujenzi  yupo  katika  makubaliano. Ukimkuta  mtu  anaendesha  daladala, bodaboda   yupo  katika  makubaliano. 

Ukimkuta  mtu  katika  ofisi  yoyote  ya  umma  yupo katika  makubaliano,walio kwenye  ndoa  na  uchumba nao  ni  makubaliano,  mfanyakazi  wa  ndani  yupo katika  makubaliano.  Aliyechukua  mkopo,  aliyeuza, kununua  nyumba au  kifaa  kingine  chochote  nao  wote  wapo  katika  makubaliano. Haraka  utaona kuwa  makubaliano  hubeba  sehemu  kubwa  ya  maisha yetu  ya  kila  siku.

Yatutosha  kusema  kuwa  makubaliano  ndio  maisha  yenyewe haswaa.Hata  biashara  yoyote  unayoshirikiana  na  mwenzako  nayo  bila  shaka ni  zao  la  makubaliano. Tutaona hapa makubaliano  yenye  hadhi  ya  kuitwa  mkataba na  ikiwa  mkataba  wa  maneno  unakubalika.

1.MAKUBALIANO  AMBAYO  MTU  ANAWEZA  KUYARUKA.

Makubaliano  yana  hadhi. Makubaliano yote  si  makubaliano.  Yapo  makubaliano  ambayo   hayawezi  kulindwa  na  sheria  na  yapo  yanayoweza  kulindwa  na  sheria.  Ni  vema sana  unapokuwa  unafanya  makubaliano  hata  yawe  ya  mdomo  ukajua  ni  vitu  gani  vya  msingi  uvizingatie  ili  makubaliano   yako  yawe   na  uwezo  wa  kukubalika  na  kulindwa  na  sheria.

Tatizo  ni  kuwa  unapokuwa  na  makubaliano  ambayo   hayawezi  kulindwa  na  sheria  maana  yake  ni  kuwa   likitokea  tatizo  lolote  au  kutoelewana  kwa  namna  yoyote  basi huwezi  kushitaki  au  unaweza  kushitaki  lakini  hautapata  kile  unacholalamikia. Utakachoambiwa  ni  chepesi  tu  kuwa  makubaliano  yako  hayakuwa  halali  kisheria. Lakini  pia ni  rahisi  yule  aliyelenga  kukudhulumu  kuyaruka. Itaelezwa  hapa  chini  ni  vitu  gani  uvizingatie  unapoingia katika  makubaliano  ili likitokea la  kutokea  uwe  na  uwezo  wa  kudai  haki  yako.

2.  MAKUBALIANO  GANI  NI  HALALI.

Mapema  ifahamike kuwa makubaliano  yote  halali  ndiyo huitwa  mikataba. Maana  yake ni  hiyohiyo kuwa  makubaliano  yote  yanayokubalika  kisheria  ndiyo  huitwa  mikataba.  Na  makubaliano  yanayoitwa   mikataba  ndiyo  makubaliano  yanayolindwa  na  sheria.
Kifungu  cha  10 cha  sheria  ya  mikataba  kimeainisha  masharti  kadhaa  ili makubaliano  yaitwe  mikataba  na  hivyo  yaweze  kulindwa  na  sheria  kama  ifuatavyo :

( a ) Kwanza  ili  makubaliano  yawe  halali  kisheria  ni  lazima  yawe  yamefanyika  kwa  hiari. Utaona  mara  nyingi  katika  mikataba  huwa  yanawekwa  maneno   “tumekubaliana  kwa  hiari  yetu  bila  kukazimishwa na mtu yeyote”.  Maneno  haya huwa  yanawekwa  ili   kutimiza  takwa  hili  la  kisheria.  Lakini  haitakiwi  tu  iwe  hiari  bali  sheria  inataka  hiari  huru ( free  consent).  Hiari  ni  lazima  iwe  huru.  Hiari  tu  haitoshi.  Hiari  huru  maana  yake  ni  kuwa  hakuna  chembe  ya  kitisho  iliyo  nyuma  ya  huyu  anayefanya  makubaliano.

( b ) Ili  makubaliano  yawe  mkataba  ni  lazima  kile  kitu  mnachokubaliana  kiwe  halali ( subject  matter). Kama  kitu  mnachokubaliana  sio  halali  basi  hayo  makubaliano hayawezi  kuitwa  mkataba na  katu  hayatalindwa  na  sheria. Kwa  mfano  hamuwezi  kukubaliana  kuiba  halafu   mkasema  ni  mkataba. Hamuwezi  kukubaliana  kubaka, kumpiga  mtu  au  kuvunja  sheria  kwa  namna  yoyote  halafu mkaita  makubaliano  hayo  mkataba.
( c )  Ili makubaliano   yawe  halali  ni  lazima  yawe  yamefanywa  na  watu  wenye  hadhi ya  kufanya  makubaliano  kisheria. Watu  wenye  hadhi  ya  kufanya  makubaliano  kisheria  ni  watu  wenye  akili  timamu, na  watu  wazima  wenye  umri  kuanzia  miaka  kumi  na  nane. Akili  timamu  inahusu  hata  mtu  kutokuwa  mlevi  wakati  akifanya  makubaliano.

( d ) Ili  makubaliano  yawe  halali  na  yaitwe  mkataba  ni  lazima  kusiwepo  na  udanganyifu  wowote  katika  masharti  ya   makubaliano  hayo. Huwa  inatokea  unaelezwa  hivi  na  vile na  unakubali  kusaini  au  kuingia  makubaliano lakini  kumbe  siyo  hivo  jambo  liko  vingine.Kwa  mfano  wapo  watu  hutolewa  nchini  na  kusafirishwa  nje kwa  mkataba  kuwa  wanaenda  kuuza  madukani  hasa huko  dubai. 

Wakifika  huko wanakuta kumbe  sio  dukani  ila  ni  kazi  za  ndani.  Na  mbaya  zaidi  hili  unaligundua  wakati  umeshasaini  makubaliano. Hiyo  ikiwa  itatokea  makubaliano  hayo ni mkataba   batili.
Haya  ni baadhi  tu  ya  mambo  ya  kisheria  ambayo  ukiyazingatia yatasaidia  makubaliano  yako  kuwa  na  hadhi  ya  kisheria  ili  hata  likitokea  tatizo  uweze  kudai  haki  yako.

3.  JE  MAKUBALIANO  NI  LAZIMA  MAANDISHI.

Hapana  kisheria  makubaliano  si  lazima  maandishi, hata  makubaliano    ya  mdomo  yanaruhusiwa. Isipokuwa  tu  maandishi  ni  lazima  katika  baadhi  ya  makubaliano  kwa  mfano  manunuzi  ya  ardhi.  Hata  hivyo  inahimizwa  kuweka   makubaliano  katika  maandishi  hata  kama  yale  ya  mdomo  nayo  yanakubalika.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com
                                                       
NYUMBA  HIZI  ZINAUZWA.














A.         
1. Ina vyumba  3.
2. Uwanja  unabaki.
3. Ipo kigamboni, kibugumo.
4. Ni  karibu  na  mji mwema.
5. Mita 300 kutoka  barabara  kuu ya  lami .
6. Bei milioni 38 inapungua  kidogo.
0784482959.

B.
NYUMBA  MBEZI  JOGOO.

1.Ipo  Mbezi  Jogoo  karibu  na  kiwanda  cha  COTEX
2. Ina  vyumba 3 , bafu 2.
3. Iko kwenye  fensi  ya  kuingia  magari 3.
4. Bei milioni 120 inapungua.

0784482959




2 comments:

  • Unknown says:
    12 March 2016 at 08:37

    Hapo kwny makubaliano si lzm yawe maandishi hata ya mdomo ynakubalika....je mm na ww tunadaiana....lkn bdae mm nataka unilipe nikasema nakudai tulikubaliana tulipane ndan ya muda fulan....na ukapita mm nikaamua kudai haki yangu mbele ya sheria....mm ntalindwaje kupata haki yng ikiwa ww utaniruka kuwa sikudai sababu hatukuandikishana.....kinga yng kupata haki yng iko wapi hapo???

  • Waiman mkondya says:
    24 September 2020 at 23:03

    Swali langu hesabu kishelia hufungwa kwa muda gani kila siku mwisho wa mwezi baada ya mwaka au miaka unakuja kupiga hessbu baada ya miaka 4 nihalali

Post a Comment