Tuesday, 29 September 2015

HAKI ZA MKOPAJI KABLA YA KUUZA MALI YAKE - 2




Image result for MNADA  WA NYUMBA
NA  BASHIR  YAKUB - 

Niliwahi  kuandika  kuwa , mkopo  sawa  lakini  haki  za  mkopaji  zilindwe. Nikasisitiza  kuwa  kushindwa  kurejesha  mkopo  wote  au  sehemu  yake  hakuondoi  haki   za  kisheria  alizonazo  mkopaji. Katika  hilo  nilizungumzia  taratibu  mahsusi  za  kisheria  zinazotakiwa  kufuatwa  wakati  taasisi  ya  fedha  inapofikia uamuzi  wa  kuuza  dhamana  ya  mkopaji, nyumba/kiwanja.  Mara  nyingi  ukiukaji  wa  haki  za  mkopaji  hutendwa  na  taasisi  iliyotoa mkopo  au  kampuni  za  udalali (brokers)  ambazo  hupewa  kazi  ya  kunadisha  mali  ya  mkopaji.

Wakati mwingine yawezekana  kabisa  taasisi  ya  fedha  ikawa  imefuata  taratibu  zote za  kisheria  lakini  tatizo  likajitokeza  kwa  dalali (brokers)  aliyepewa  kazi  ya  mnada. Na  hivi  ndivyo  ambavyo  imekuwa  ikijitokeza   na  hiyo  ni  kwasababu  moja  tu,  kuwa  hawa  hupenda  kujipatia  faida  kubwa  na  ya  haraka katika  mali  inayonadishwa. Ni  katika  kufanya  hivyo hujikuta wamekiuka  haki  na  taratibu  za  uuzaji  kwa  ujumla.   Kwa  ufupi  haki  na  wajibu  ni  vitu  vya  kuzingatia  sana katika  miamala  ya  mkopo  hasa  ikizingatiwa  kuwa  jambo  hilo  huhusisha  fedha  na  mali  kama  nyumba  ambamo  wakati  mwingine  ndimo  yalimo  makazi yetu.

1.WAJIBU  WA  MTOA  MKOPO.

Sheria ya  rehani  ya  mwaka 2008 imeeleza  vizuri  baadhi  ya  wajibu  walionao  watoa  mkopo. Tutaangalia  baadhi.

( a ) Kwanza  kabisa  ni  wajibu  wa  mtoa  mkopo kuhakikisha  anatafiti  na  kujua  iwapo  mtu  anayechukua  mkopo  ana  mke  au  ana mme. Hii  ni  kwasababu  kwa  mujibu  wa  sheria  ikiwa  nyumba  au  kiwanja  kinachowekwa  rehani  ili  kupata  mkopo  ni  cha  familia  kwa  maana  cha  wanandoa  basi  ni  lazima  wanandoa  wote  wawe  wameridhia  na  wote kwa  pamoja  watasaini waraka  maalum  kuthibitisha  ridhaa  zao.  Ikiwa  taasisi  ya  mkopo  haikufanya  utafiti  na  kujiridhisha  na  hili  basi  madhara  yatayopatikana   yatawaathiri  wao kwakuwa  utakuwa  ni  uzembe  kwa  upande  wao.  Hairuhusiwi  mwanandoa  mmoja kutumia  mali  ya  familia  kama  dhamana  bila  ridhaa  ya  mwingine.

( b ) Pia  mtoa  mkopo  ana  wajibu  mwingine  wa  kuhakikisha  mali  inayowekwa  kwake  kama  rehani  haijawekwa  rehani  sehemu  nyingine  yoyote,  haina  mgogoro  wowote  katika  mahakama  yoyote  ya  sheria, haina  zuio  lolote( caveat), na  wala  si  ardhi  ambayo  iko  katika  mpango  fulani wa serikali  ambao utatekelezwa  muda  mfupi  kabla  ya  deni  kuisha  au  hapo  baadae  kidogo. Hii  humuepusha  mtoa  mkopo  kutoingia  katika mgogoro  na  mamlaka  nyingine    hasa  za  serikali au  watu binafsi  ambao  wanaweza  kuwa  na  maslahi  katika  ile  ardhi  kabla  yake.

( d ) Wajibu  mwingine  muhimu  ni  kuhakikisha  wanamweleza  mchukua  mkopo  hali  halisi  kuhusu  huo  mkopo,  ikiwa  ni  pamoja  na  athari  zake  atakaposhindwa  kulipa, taratibu  za  marejesho,  uhuru  wa  kuongeza  mkopo na  ukomo, na  kila  kitu ambacho  ni  sehemu  ya  muamala  wa  mkopo.

2.  HAKI  ZA  MCHUKUA  MKOPO/MKOPAJI.

( a ) Iwapo  kuna  badiliko  lolote  katika  taratibu  za  ulipaji  deni  husika, riba  yake au  mabadiliko  yoyote  katika  tarehe  ya  marejesho  ni  haki  ya  mchukua  mkopo  kujulishwa  kwa  maandishi  maalum. Taasisi  kubwa  za  fedha  zimekuwa  zikilitekeleza  hili tofauti  na  taasisi  ndogo   ambazo  ndio  nyingi  kwa  sasa. Katika  taasisi  ndogo  isikushangaze siku  ya  kurejesha  mkopo  ukaambiwa kuwa  deni  limeongezeka  kwasababu  hii  na  hii  na  hivyo  hii  pesa  uliyoleta  haitoshi. Wanakiuka  sana  haki  za wakopaji.

( b ) Ardhi  iliyowekwa rehani  inaendelea  kuwa  haki  ya mchukua  mkopo  ikiwa  yule  aliyenunua  ardhi   hiyo kwa  njia  ya mnada  hajamalizia  hela  ya  malipo  ya  mnada  kama ilivyokubaliwa. Wako  watu  huweza  kulipa 25% tu  wakati  wa  mnada  na  kushindwa  kumalizia  salio. Hii  ikitokea  maana  yake  ni  kuwa  umiliki  bado  unakuwa kwa  mchukua  mkopo  na  muda  wowote  humo katikati   anaweza  kutafuta  hela  na /au  kufanya  vinginevyo  kukomboa  nyumba  yake.

( c ) Haki  ya  kupewa  taarifa  ya  siku  sitini  kabla  ya  mauzo  ni  haki  ambayo  huwa nairejea  mara  kwa  mara  kutokana  na  umuhimu  wake . Si tu  kutokana  na  umuhimu  wake  bali  pia  kutokana  na  namna  ambavyo  huwa  haizingatiwi  na  wengi hasa  wanadishaji (brokers).

( d ) Mkopaji  ana  haki  ya  kulipa  rejesho na  riba  kwa  viwango  vya  fedha  vinavyotambulika  na  kukubaliwa  kisheria. Baadhi  ya  taasisi fedha  hasa zile  ndogo  zimekuwa  zikijipangia  viwango  vya  marejesho  na  riba  ambazo  ni  kubwa  kupita  kiasi  huku  zikiwa  zimekiuka  taratibu za viwango  vya  fedha.  Hii  ni  pamoja  kuongeza  viwango  hivyo  kinyemela  huku  wakilenga  kujipatia  faida  kubwa .
Kwa  leo  ni  hayo.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

                                           TANGAZO   MUHIMU                                                
VIWANJA     NA     NYUMBA          ZINAUZWA.
·        
WANASHERIA   WETU   WATAKUANDALIA   MIKATABA  YOTE  BURE  NA  KUKUSIMAMIA  MPAKA   MANUNUZI    YAKAMILIKE   BURE.
·        
UHALALI   WA  NYARAKA   NA   UMILIKI   UMETHIBITISHWA  NA                  WANASHERIA  WETU.
·        
UTAPEWA  MTU  WA  KUKUSAIDIA  KUFANYA  TRANSFER   KWA HARAKA  BURE.
·        
IKIWA   UTATOKEA   MGOGORO  NDANI   YA  MWAKA  TANGU  TAREHE  YA       MANUNUZI    UTAPEWA   WAKILI   WA   KUSIMAMIA  MGOGORO    BURE
                                                        0784482959.

 KUONA   BOFYA  HAPO  JUU    MWANZO  WA   BLOG.



0 comments:

Post a Comment