Thursday, 6 August 2015

MAKOSA YA KISHERIA KATIKA KUNADISHA NYUMBA YA MKOPAJI.


Image result for MNADA WA NYUMBA

                
NA  BASHIR  YAKUB - 

Sheria  ya  ardhi  Sura  ya  113  imetoa  maelezo  kwa  upana  kuhusu  miamala    kati  ya  mtoa  mkopo , mkopaji na  dhamana  inayohusika katika mkopo  huo. Mara  kadhaa   watu binafsi,  taasisi  za  haki  za  binadamu, asasi  za kiraia, na  makundi  mengine  wamekuwa  wakitoa maelezo  mbalimbali   yanayotokana  na  sheria hii hasa  wakilenga  kupunguza vitendo  vya  ukiukaji  wa  taratibu  ambao  hufanywa  na  baadhi  yua  taasisi  za  mikopo   zikishirikiana  na  makampuni  ya  udalali  ( Brockers/auctioneers). 

Katika kipindi  hiki  ambapo  taasisi  za  fedha  zinazojihusisha  na  mikopo  zimeongozeka watu  wengi  wamekuwa  wakilalamikia  mienendo  yake hasa  pale  mtu  anaposhindwa  kurejesha  kwa  wakati. Pia wamekuwa  wakilalamikia  namna  taasisi  hizi  zinavyowakokotolea  mahesabu  hasa  yale  ya  riba. Jingine  ni  taratibu  zinazotumika  katika  kuuza/ kunadisha   dhamana  ya  mtu   hasa    nyumba  iwapo  mlengwa  ameshindwa kurejesha.

Wengi wamekuwa  hawaridhishwi  na uuzaji  wa  nyumba za  wakopaji  kwa namna ya  kuvizia. Ni  uuzaji  ambao  sura  yake  ni  kama  watoa mkopo   walikuwa wakisubiri  kwa  hamu  mkopaji  ashindwe  kulipa  ili  nao  waweze  kufaidika  na    dhamana iliyowekwa  iwe  kwa  kuiuza  na  kujipatia  faida  kubwa  au  kuibadilisha  matumizi  ikiwemo kujimilikisha.

Wakati  nilipoandika  makala  niliyoipa  kichwa  NAMNA  YA  KUOKOA  NYUMBA  ISIUZWE  IWAPO  UMESHINDWA  KULIPA  DENI  nilisema  kuwa  mkopaji  anazo  haki  zake  za  msingi   hata  kama  yuko nje  ya  mkataba(default)  kwa  kushindwa  kurejesha  kwa  namna  alivyoainishiwa.  Kushindwa  kurejesha kwa namna  yoyote  iwayo  katu hakuondoi  haki  za mkopaji  alizopewa na sheria, na  hili  lazima  lieleweke  hivyo. Sisemi  watu  wasilipe  madeni,hapana  isipokuwa  ninasema   walipaji  wa  madeni  nao  wanazo  haki  zao  ambazo  kukiukwa  kwake  kunaleteleza  haki  yao  ya  kufungua  shauri  na  kuzidai . Huu  ndio  msingi  wa  sheria.

1.MNADA  HARAMU  WA  NYUMBA  YA  MKOPAJI.

Ni  juzi  tu  nilisoma  gazeti  moja la  kila  siku   ambapo  sambamba  na  gazeti  hilo pia  niliona  katika  taarifa  ya  habari   uuzaji  wa nyumba   moja  iliyoko  maeneo  ya  Mbezi Salasala. Mnada  huo  ulifanywa  na  kampuni   fulani  ya udalali ( brockers)  kwa  maagizo  ya  benki  moja  kubwa  hapa  nchini  ambayo   nisingependa niitaje  kwa  leo. ( Hata  hivyo  ikiendelea  kukiuka  taratibu  kama  ilivyofanya  tutaitaja  kwenye  vyombo  vya  habari  bila  kujali  madhara  yake  kibiashara ). Kwa  namna  wahusika  walivyolalamikia  taratibu  za  uuzaji  ilinitia  shauku  ya  kufuatilia  na  kujua  uuzaji  ulifanyikaje . Bahati  nzuri  mwanasheria  mwenzangu  ndiye  aliyepewa  kazi   ya  kushughulikia  wahanga  hao  na  hivyo  ikanipa  nafasi  ya  kujua  mnada  ulivyofanyika  kwa  undani.

2.  KUKIUKA  TARATIBU  ZA  KISHERIA.

Hawa jamaa  ( brockers na  benki)  walikiuka  taratibu  nyingi  lakini   ninayoeleza  hapa  ni  ile  ya  namna  ya kupiga  mnada.  Kama  we ni mkopaji  au  nyumba  yako  iko  katika   mpango  wa  kuuzwa au  ilishauzwa basi  yafaa  hili ulielewe.  Mnada  unapokuja  kufanyika  ni  lazima  ufanyike  kwa  mtindo  wa  mnada  ulioainishwa na  sheria. Mtindo  wa  mnada  ulioanishwa  na sheria  ni  ule wa  kutangaza  ambapo   mnunuzi  anakuwa  zaidi  ya  mmoja  halafu  wanashindana  kwa bei. Huyu  akisema  kiasi  fulani  , yule  anasema  kiasi  fulani na  mwingine  anasema  kiasi  fulani  mpaka  mwisho  mnunuzi  anapatikana.  Isiwe  wanakuja   watu  kwenye  nyumba  wanaoneshana  na  kuondoka  halafu  wanasema mnada  umefanyika. Huo  sio  mnada  ni  utapeli.

Hiki  ndicho  kilichotkea  Mbezi  ambapo  kigogo  wa  benki  husika  alikuwa  akiitaka nyumba  hiyo  na  hivyo  walipofika  eneo  la  tukio  walioneshana  nyumba  kisha  wakaondoka halafu  baadae   wakopaji wanaletewa  taarifa  kuwa  mnada  ulifanyika. Hili  haliruhusiwi  kisheria  na likifanyika  kimsingi ni  hakuna  mnada.

3.  MNADA  ULIOKIUKA  TARATIBU  NI  SAWA  NA  HAKUNA  MNADA.

Ikiwa  mnada  umekiuka  taratibu  basi   jibu  lake  ni  kuwa  hakuna  mnada  uliofanyika  na  kisheria nyumba  inaendelea  kumilikiwa  na   mwenye  nayo.  Kama  watoa  mkopo  hawatataka  kulielewa  hili  basi   mkopaji  nenda  mahakamani  haraka  upate  haki  yako  iliyoporwa. Nakuhakikishia  utaipata.  Aidha  taratibu  nyingine  za  uuzaji  wa  nyumba  ya  mshindwa  kulipa  mkopo  ni  kumpa  notisi  ya  siku  sitini  ambayo  hutakiwa  kutolewa  baada  ya  mwezi  mmoja  tangu   mkopaji  ashindwe  kulipa deni.

4.  USHAURI  WA KITAALAM .

Kwa  namna  yoyote  ile   watoa  mkopo  wakishindwa  kutimiza  haki  yoyote  katika  kudai  deni  lao  ikiwemo  uuzaji  au  jaribio  lolote  la  kuuza  pasi na  kufuata  taratibu   ni  vema  mkopaji  kukimbilia  mahakamani . Amini  usiamini hii  ni  namna  ya pekee  ya kukuweka  salama wakati  ukisubiria  mambo  mengine. Tena  ni  vema  kukimbilia  mahakamani mapema  kabisa tangu  pale  unapoanza  kuona  dalili za kutoelewana na  wadeni  wako. Hili  ni  bora  zaidi  kwakuwa  kishauri /kikesi ni  rahisi  sana  kuzuia  nyumba  kuuzwa  kuliko  kukomboa  nyumba  ambayo  imeshauzwa. Zingatia

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

                                           TANGAZO   MUHIMU                                                
VIWANJA     NA     NYUMBA          ZINAUZWA.
·        
WANASHERIA   WETU   WATAKUANDALIA   MIKATABA  YOTE  BURE  NA    KUKUSIMAMIA  MPAKA   MANUNUZI    YAKAMILIKE   BURE.
·        
UHALALI   WA  NYARAKA   NA   UMILIKI   UMETHIBITISHWA  NA                        WANASHERIA  WETU.
·        
UTAPEWA  MTU  WA  KUKUSAIDIA  KUFANYA  TRANSFER   KWA  HARAKA         BURE.
·        
IKIWA   UTATOKEA   MGOGORO  NDANI   YA  MWAKA  TANGU  TAREHE  YA       MANUNUZI    UTAPEWA   WAKILI   WA   KUSIMAMIA  MGOGORO    BURE
                                                        0784482959.

 KUONA   BOFYA  HAPO  JUU    MWANZO  WA   BLOG.



2 comments:

  • memaidda says:
    18 February 2019 at 23:05

    habari,naomba kujua je ni taratibu zipi mkopeshaji anapaswa kuzifata kabla ya kuuza dhamana za ndani za mteja alieyeshindwa kulipa deni lake?

  • Unknown says:
    18 April 2019 at 06:10

    Nauliza kama nyumba imeuzwa siku hiyohiyo na mkopaji anayopesa ya kulipa hapohapo sheria inasemaje na mnada tayar umefanyika bila mwenye nyumba kuwepo na bila taarifa

Post a Comment