Wednesday 12 August 2015

JE TRAFIKI ANARUHUSIWA KUKUNYANG”ANYA LESENI ?.


Image result for askari wa barabarani

         
NA  BASHIR  YAKUB -

Kumekuwepo  na  sintofahamu   nyingi  kwa  madereva  na  watumiaji  wengine  wa  vyombo  vya  usafiri. Sintofahamu  hii  imekuwa  ikiletwa  na   baadhi  ya  mambo  ambayo  hayaeleweki  sawasawa  katika  suala  zima  la  usalama  barabarani   na  sheria  zake. Wadau   wa  barabarani wamekuwa  wakilaumiana,  madereva  wakiwalaumu  askari  wa  barabarani  kwa  uonevu  huku  askari  wa  barabarani  wakiwalaumu  madereva  kwa  ukorofi   na  ukosefu  wa  utii  wa sheria  bila  shuruti. Lakini  swali  hapa  ni  kwanini  iwepo  mivutano  na  hali  kuna  sheria. Sheria  inasemaje  kwa  kila  jambo  ambalo  wadau  hawa  wanatofautiana?.

1.UBABE  WA  ASKARI  WA  BARABARANI.

Baadhi  ya  askari  wa  barabarani  wamekuwa  ni  wababe  sana. Wanahoji  mambo  ambayo   si  wajibu  wao  kuyahoji  na  hawataki  dereva  aulize  lolote  kuhusu  kuhoji  kwao  mambo  hayo. Wanataka  kila  wanachosema  dereva atii  hata  kama anaona  hakipo  kwa  mujibu  wa  sheria. Matokeo  yake  mtu  anaandikiwa  faini  za  makosa  mengi  ilimradi  tu  kumkomoa. Askari wengine  wamefikia  hatua  ya  kuwapiga madereva  vibao.  Binafsi  nimewahi  kushuhudia  askari  wa  usalama  barabarani  akimnasa  kibao  dereva wa  daladala. Ni  ubabe  uliovuka  mipaka  na  hakika  ni  uvunjaji  wa  sheria  uliopitiliza .

2.  JE  TRAFIKI  ANARUHUSIWA  KUMNYANGANYA  DEREVA  LESENI.

Masuala ya usalama  barabarani   yanaainishwa  ndani  ya  Sheria  ya  Usalama barabarani ( The  Road  Traffic Act) ambayo  ndio  hueleza  wajibu   na  haki  za  kila  mdau  na  mtumiaji  wa  barabara. Katika  sheria  hii  hakuna  pahala pameandikwa  kuwa  trafiki  achukue  leseni  ya  dereva  kwa  kuwa  dereva  ametenda  kosa   fulani. Maana  fupi  ya hili  ni  kuwa  trafiki  haruhusiwi  kuchukua  leseni  ya  dereva.  Anachoweza kufanya  trafiki  ni  kile  kilichoainishwa  na  kifungu  cha  17  cha  sheria hiyo  ya  usalama  barabarani. Kifungu  hicho  kinampa  trafiki  mamlaka  ya  kukagua  na kujiridhisha   na  uhalali  wa  leseni  ya  dereva. Hakisemi  aichukue. Kinasema  aikague  basi.  Kukagua  na  kuchukua  ni  mambo  mawili  tofauti. 
Kama  hivyo  ndivyo  basi  yafaa  kueleweka  kuwa   kitendo  cha  askari  kumsimamisha  dereva  na  kisha  kumpokonya  leseni  yake  ni  kinyume  cha  sheria.  
Dereva  anao  wajibu  wa  kulinda   haki  hii  kwa  kulikataa  hili na kuhakikisha trafiki  hamfanyii  kitendo  hiki.  Kumbuka  kuwa  wakati  askari  wa barabarani  akitekeleza  wajibu  wake  wa kisheria  na  wewe  dereva  unayo  haki  ya  kutetea  haki  zako  za  kisheria. Hakuna  aliye  juu  ya  mwingine kwani  anatekeleza  wajibu  nawe  unalinda  haki.

3.   SAID  MWEMA   AKATAZA  KUNYANGANYWA  LESENI.

Mkuu   wa  jeshi  la  polisi  mstaafu ndugu Saidi  Mwema  aliwahi  kuandika  kukemea  hatua  ya  madereva  kunyanganywa  leseni. Katika  kijarida  alichokiita  UMESIMAMISHWA  NA  POLISI  UKIWA  UNAENDESHA ?, ZIJUE  HAKI  NA  WAJIBU  WAKO,  ndugu  mwema  ameandika  akisema   kuwa  ofisa  wa  polisi  hana  haki  ya  kuchukua  leseni  ya  dereva.

4. HAIRUHUSIWI  KUBANDUA  BIMA/ AU  KIBANDIKO( STICKERS)  KINGINE  CHOCHOTE.

Wakati  mwingine  askari  wa  barabarani  huamua  kubandua  bima  au  vibandiko  vingine ( stickers) kwa  lengo  la  kumfanya  dereva amfuate  au  malengo  mengine  yoyote. Hili  nalo  ni  kosa  kwakuwa  haliainishwi  popote katika  sheria.  Jambo  ambalo   halikuruhusiwa  na  sheria  kulitenda  kwake  ni  kosa. Ieleweke  kuwa  askari  wa  barabarani  haruhusiwi kubandua  stika  yoyote  katika  gari  lako  wala  kuichukua.

5.  UKIONEWA  NA  ASKARI  WA  BARABARANI CHUKUA  HATUA  HIZI.

Ili  uweze  kumchukulia  hatua  vizuri  askari   ni  vema  ukijua  jina  lake, cheo  chake, na  kituo  anachotokea. Katika  kuyajua  haya  ni  lazima  watu  wajue kuwa  ni  haki  yako  kumuuliza  askari  taarifa  hizi.  Sio  dhambi  wala  kosa  ila  ni  haki  kumuuliza  askari  taarifa hizi.  Na  kwa  askari  ni  wajibu  kukueleza  taarifa  hizi. Haijalishi  mmeshatofautiana  wala   nini  isipokuwa  ni  wajibu  akupe  taarifa  hizi. Lakini  ushauri  ni  kuwa  ni  vema  zaidi  askari  anapokusimamisha  tu  kabla  ya  kujadili  lolote  kumuuliza au kumuomba ajitambulishe  ili  hata  mkishatofautiana  mbeleni  iwe  rahisi  kwako  kuchukua  hatua.

Kiutaratibu  inatakiwa  askari  ajitambulishe  kwako  bila  wewe kumuuliza na kabla  ya  kuzungumza  lolote  lakini  kwakuwa  hawafanyi  hivyo  ndio  maana  wewe  unalazimika  kumuuliza.  Baada  ya  kupata  taarifa  hizo  peleka  malalamiko  yako  kwa  mkuu  wa  kituo  anachotokea  halafu  fuatilia. Atachukuliwa  hatua  wala huna  haja  ya  kulihofi  hilo. Jeshi  la  polisi  ni sehemu ambako  nidhamu  inazingatiwa  kuliko  pahali  pengine  popote  hivyo    unapomripoti  askari  ni  lazima  ashughulikiwe.

Kwa taarifa yako  askari  wanaogopa  sana  kuripotiwa kwa  wakubwa  zao  kuliko watumishi  wengine  wowote  wa umma unaowajua, hili  nakupa. Na  askari  yoyote  mwenye  kujitambua  akijua  unalenga  kumripoti  ni  lazima  akubali  myamalize. Basi usiishie  kulalamika kwani  kulalamika  hakusaidii  chukua  hatua  ili  iwe  funzo  kwa  wengine  kesho  na  mbeleni.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

                                           TANGAZO   MUHIMU                                                
VIWANJA     NA     NYUMBA          ZINAUZWA.
·        
WANASHERIA   WETU   WATAKUANDALIA   MIKATABA  YOTE  BURE  NA    KUKUSIMAMIA  MPAKA   MANUNUZI    YAKAMILIKE   BURE.
·        
UHALALI   WA  NYARAKA   NA   UMILIKI   UMETHIBITISHWA  NA                        WANASHERIA  WETU.
·        
UTAPEWA  MTU  WA  KUKUSAIDIA  KUFANYA  TRANSFER   KWA  HARAKA         BURE.
·        
IKIWA   UTATOKEA   MGOGORO  NDANI   YA  MWAKA  TANGU  TAREHE  YA       MANUNUZI    UTAPEWA   WAKILI   WA   KUSIMAMIA  MGOGORO    BURE
                                                        0784482959.

 KUONA   BOFYA  HAPO  JUU    MWANZO  WA   BLOG.



0 comments:

Post a Comment