Thursday, 27 August 2015

KUMSHITAKI ASKARI ALIYEKUBAMBIKIZA KESI.


Image result for askari polisi

                   
NA  BASHIR  YAKUB  - 

Kumbambikiza   mtu kesi  ni  kosa. Si  tu  ni  kosa  bali  pia  ni  kinyume  kabisa cha  haki  za  binadamu  na ustaarab wa  dunia. Inawezekanaje  mtu  akashtakiwa  kwa  kosa  ambalo   si  tu  hakulitenda  bali  pia  halijui  kabisa. Ni  matendo  yanayofanywa  na  watu  makatili  na  mabazazi.  Niseme  tu  mapema  kuwa  kosa  hili  haliwahusu  tu  askari  isipokuwa  kila  mtu   ambaye  anaweza  kumshtaki  mwingine  kwa  kosa  ambalo  anajua  kabisa  halikutendeka  au  lilitendeka  lakini  anayeshitakiwa  siye  aliyelitenda.

1.NINI  MAANA  YA  KUBAMBIKIZA  KESI.

Kwa  jina  la  kitaalam  kubambikiza  kesi  huitwa  “malicious  prosecution”. Kwa  tafsiri  ya  kiswahili  ya  moja  kwa  moja  ni  “kushitaki  kwa  hila”. Linatumika  neno  kubambikiza  kesi  kwakuwa  ndilo  lililozoeleka  na  kufahamika.  Maana  ya  kubambikiza  kesi  ni  kumfungulia  mtu  kesi  ya  jinai  kwa  hila  na  bila  sababu  za  msingi  lakini  mtu  huyo  aliyeshitakiwa akashinda hiyo kesi. Kwa  tafsiri hii  tunapata  kujua  kuwa  kubambikiza  kesi  kunahusisha kushtakiwa  kwa  kesi  za  jinai. 

Kwahiyo  kusingiziwa  kutenda  jinai  ndio  kubambikizwa  kesi.  Jinai  ni  kama  kushtakiwa  kwa  wizi,  ukabaji, ubakaji, udhalilishaji, kutusi, kuharibu  mali, kupigana, kukutwa  na/au  kujihusisha  na  dawa  za  kulevya  ikiwemo  bangi, kuua,  kujaribu  kuua  au  kujiua, kula  njama , utapeli,  na  mengine  mengi. Ukisingiziwa  kutenda  haya   na  ukashitakiwa  basi  unakuwa  umeingia  katika  maana  ya  kubambikizwa  kesi.

2.  TABIA  YA  ASKARI  KUWAMBIKIZIA  KESI  RAIA.

Jamii  imelalama  sana  kuhusu  hili. Leo  si  ajabu  bodaboda   akazozana  na  askari  kuhusu  labda  ukiukaji  wa  taratibu  za  barabarani   lakini  akafikishwa  kituoni  akaambiwa  aoneshe  bunduki  ilipo. Au  mtu  akakamatwa  kwa  kosa  la  ugomvi   akafikishwa  kituoni  akaandikiwa  kosa  la  kukutwa  na bangi. Na  mambo  mengine  yanayofanana  na  hayo. Jamii  imekuwa  haina  amani  na hili  limelegeza  sana  uhusiano  wa  jeshi   la  polisi  na  wanajamii. Utafiti  unaonesha  kuwa   hali  hii  imekuwa ikijitokeza  hasa  pale ambapo askari  amekosana  na  mtu   pengine  umejitokeza  ubishi   wakati  raia  akikamatwa au vinginevyo ambapo  askari  hufanya hivi  kuonesha  kwamba   anaweza.  Zaidi  baadhi  ya  watu  hasa  wenye  fedha  wamekuwa wakitumia  njia  hii kuwakomoa  au  kuwatia   adabu  wabaya  wao. Askari  anatanguliziwa  kidogo  linatengenezwa  kosa,  mtu  anakamatwa  na  kushitakiwa.

3.   ASKARI  SASA  NAO  WASHITAKIWE.

Kwa  kumbabikiza  mtu  kesi  askari  anaweza  kushitakiwa. Anashtakiwa  kwa  kosa  la  kushitaki/kufungua  kesi   kwa  hila. Hila  ni  nia  mbaya. Wapo  wanaojua  askari  hawezi  kushtakiwa,  sio  kweli  kabisa. Anashtakiwa   na  atatakiwa  kulipia  hasara  na  madhara  aliyokusababishia. Kwa  kosa  hili  askari  atashitakiwa  katika  kesi  ya  madai  na  mahakama   anayotakiwa  kushitakiwa  itategemea  na  kiwango  cha fedha  ya fidia  unayodai. Ila  zaidi  itakuwa  ni  mahakama   za  wilaya. Ili  umshitaki  askari  katka   kesi  hii  utatakiwa  ujiandae  na  mambo  yafuatayo  ambayo  nitaeleza  hapa  chini.

4.   JIANDAE  NA  MAMBO  YAFUATAYO.

( a ) Hakikisha  unamjua  askari  aliyekufungulia hiyo kesi . Kuna  tofauti  kati  ya  mwendesha  mashtaka  na  aliyefungua  kesi . Aliyefungua  kesi ni  yule  aliyekukamata  na  kukutuhumu  kuwa  nimekuona  ukitenda  kosa  fulani. Kwa  ufupi  ni  yule  mpeleka  mashtaka. Hili  ni  lazima  kwasababu  mahakama  itakutaka  kuonesha  aliyekushtaki  kwa  hila/kukubambikiza  kesi.

( b ) Utatakiwa  uoneshe  kuwa  umefunguliwa  kesi  bila  sababu  za  msingi. Hili  ni  kuonesha  tu  mazingira uliyokamatiwa  na  aina  ya  kosa  unalotuhumiwa  nalo.

( c ) Utatakiwa  uoneshe  kuwa  askari  alifanya  hivyo  kwa  hila/nia  mbaya.Hili  ni  pamoja  na  kuonesha kilicho nyuma  ya  kesi  hiyo  labda  askari  unatumiwa  na  fulani   au  alifungua  kesi hiyo  baada  ya  kubishana na  sasa  amefanya  hivi  kuonesha  ushindi/ kuwa  anaweza  n.k.

( d ) Utatakiwa  uoneshe  kuwa  kesi ya  jinai  aliyokufungulia  uliishinda,  iwe  kwa  hukumu  au kesi  hiyo  kushindwa  kuendelea kwasababu  nyingine .Kumbuka  hapa  utakuwa  umefungua  kesi  mpya  ya  madai  ukilalamikia kesi  ya  jinai uliyofunguliwa na iliyokwisha. Kwahiyo  utaonesha kuwa kesi  hiyo  ilikwisha  kwa  hukumu au  illishia  njiani   na  hivyo kuachiwa  huru.

( e ) Utatakiwa  uoneshe  kuwa  kutokana  na  kubambikizwa kesi   ulipata  madhara  kadha  wa  kadha. Hili  linatakiwa  kwa  lengo  la  kutathmini  kiwango  cha fidia  ambayo  unatakiwa  kulipwa. Madhara  ni  mengi  kwanza  ulitumia  gharama mpaka  kumaliza hiyo  kesi, pili uliacha  kazi  zako kushugulikia  hiyo  kesi  na  pengine  ulipoteza  kazi  a  mipango  yako  ya  hela,  tatu ulidhalilishwa  jamii  ikajua  we  ni  mjinai  kumbe  siyo,  nne umeteseka  ulipokuwa  rumande, tano  watoto  na  famillia   yako  wameshindwa  kupata  mahitaji  muhimu  ulipokuwa mahabusu, n.k. Utaonesha  kila  tone  la  athari  ulilopata  ili  lilipwe.

Kuwafungulia  mashtaka ni moja  ya  namna ya  pekee  ya kukomesha  ubazazi  huu.  Haya  niliyoeleza  wala hayana ugumu  wowote isipokuwa  tu  hapa  ni  katika  maelezo  lakini  kivitendo  ni  mambo  ambayo hufanyika  kwa  muda  mfupi. Nasema  hivyo  ili  watu  wasiogope  kuuchukulia  hatua  ubazazi  huu  kwa  kuhofia  kuwa  kuna  mchakato mrefu. Chukua  hatua  tuishi  salama.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

                                           TANGAZO   MUHIMU                                                
VIWANJA     NA     NYUMBA          ZINAUZWA.
·        
WANASHERIA   WETU   WATAKUANDALIA   MIKATABA  YOTE  BURE  NA    KUKUSIMAMIA  MPAKA   MANUNUZI    YAKAMILIKE   BURE.
·        
UHALALI   WA  NYARAKA   NA   UMILIKI   UMETHIBITISHWA  NA                        WANASHERIA  WETU.
·        
UTAPEWA  MTU  WA  KUKUSAIDIA  KUFANYA  TRANSFER   KWA  HARAKA         BURE.
·        
IKIWA   UTATOKEA   MGOGORO  NDANI   YA  MWAKA  TANGU  TAREHE  YA       MANUNUZI    UTAPEWA   WAKILI   WA   KUSIMAMIA  MGOGORO    BURE
                                                        0784482959.

 KUONA   BOFYA  HAPO  JUU    MWANZO  WA   BLOG.



0 comments:

Post a Comment