Monday 3 August 2015

IJUE NAMNA YA KUPATA MSAMAHA WA KODI NA USHURU BANDARINI.

Image result for BANDARINI

               
NA  BASHIR  YAKUB - 

Sheria  ya  Uwekezaji  ya  Mwaka  1977 imehamasisha  uwekezaji  kwa  wazawa  na  wasio  wazawa  kwa  kuweka  mazingira  rafiki  kwa  wajasiriamali katika  nyanja  zote.  Wapo  ambao  wanajua fursa hizi  na wamezitumia   kujipatia  maendeleo  na  wapo  ambao  hawajatumia  fursa  hizi.  Nataka  niseme  kitu  kimoja  kuwa  wazawa  wengi  wameshindwa  kufanikiwa  kwa  kutojua  uwepo wa fursa. Wengi  wangependa  kutumia  fursa   kama  zipo  lakini  hawajui ziko  wapi na  zinapatikana vipi.

Badala  yake  wageni  na  watu  wengine  ambao  si  wenye  asili  halisi  ya  Tanzania  ndio  wamekuwa  wakihabarishana  kuhusu  fursa  hizi  wanazitumia  na  wanafanikiwa sana.  Wenyeji  halisi   wa  nchi  hii  wanabaki  kutazama  mafanikio  ya  watu  hawa  wasijue  yanapatikanaje. Ziko  fursa  ambazo  zimetolewa  na  serikali  na  kuainishwa  na  sheria  mbalimbali  mojawapo  ikiwa  hii  ya  kusamehewa  kodi  kwa bidhaa  zinazoingizwa  nchini  kutoka  nje  ya  nchi. Wafanyabiashara  watakubaliana  na  mimi  kuwa  ikiwa  utapata  msamaha mzuri  wa  kodi bandarini  basi  unayo  nafasi  kubwa  ya  kutengeneza  faida  kubwa  katika  biashara  yoyote  utakayoamua  kufanya.

Mara  zote  kodi  ndio  huwa  tatizo. Makala  haya yataeleza  namna  ya  kupata  msamaha  wa  kodi.

1.KUHUSU  MSAMAHA  WA  KODI  NA  USHURU.

Sheria  ya  uwekezaji  ya  1997, sehemu  ya  ( iii ), kifungu  cha 17 ( 1 – 8)  kimeeleza  kuhusu  kujisajili  katika  kituo  cha  uwekezaji  Tanzania  na  kupata  cheti  kiitwacho  Certificate  of  Incentives.  Kinachotakiwa  ni  mjasiriamali  kujisajili  katika kituo    cha  Uwekezaji  Tanzania (TIC)  na  kupata  cheti  hiki  ambapo  kupitia   cheti  hiki  mjasiriamali   atakuwa  akipata   msamaha  wa  kodi  wakati  anapoingiza  bidhaa  kutoka  nje  ya nchi kwa  miaka  tatu.

Hapa kwetu, wageni  na  wafanyabiashara  wenye  asili  ya  Asia  wanatumia  fursa  hii  kwa  ufasaha na  sitaki  kueleza  mafanikio  yao  kwani  kila  mtu  anayajua. Katika  kuonesha  dhamira ya  dhati   katika  kuwapunguzia  watu  kodi  kituo  cha  uwekezaji (TIC ) kimeanzisha  kitengo  kiitwacho  TIC-TRA  ambacho  ndicho  hushughulikia  masuala  yote  yanayohusu   namna  ya   kupunguziwa  kodi  .

2.  NAMNA  YA  KUJISAJILI   TIC.

Tumesema  hapo  juu  kuwa  ili  uweze  kufaidika  na   msamaha  huu  ni   lazima  uwe  umejisajili  katika  kituo  cha  uwekezaji  Tanzania (TIC). Hii  ni  namna  ya  kujisajili   TIC.

( a ) Kwanza  lazima  uwe na  cheti  cha   kuzaliwa  kwa  kampuni( Certificate  of  Incorporation). Hii  ina  maana  kuwa    ni  lazima  uwe  na  kampuni  kwakuwa huwezi  kuwa  na  cheti  hiki  bila  kuwa  na  kampuni. Ulazima  wa  kuwa  na  cheti  hiki ni  kuthibitisha kuwa unayo   kampuni   na  imesajiliwa kwa  mujibu  wa  sheria.

( b ) Lazima  uwasilishe  katiba  na  waraka  wa  kampuni ( memorandum & article  of  association). Kimsingi  unapokuwa  umesajili  kampuni  hivi ni  vitu  ambavyo lazima  uwe  navyo. Hivyo  nakala  moja  ya  vitu  hivi  ndiyo  inayotakiwa  TIC.

( c ) Uwasilishe  hati  ya  nyumba   kama  unamiliki  nyumba  ambayo   ndio  umeifanya  kama  ofisi  yako  au  mkataba  wa  pango  ikiwa  nyumba  unayofanyia  biashara  umeipanga.

( d ) Barua  kutoka  benki .  Ukienda  benki  ukawaambia  nimetumwa  barua  ya  TIC  wao  wanajua  ni  barua  ya  aina  gani  inahitajika.

( e ) Nakala  mbili  za  mpango  kazi (feasibility  study) .  Mpango  kazi   ni  maelezo  kwa  urefu  yanayoeleza  aina  ya  biashara   inayofanywa  na  muombaji,  mategemeo  yake  katika  biashara  hiyo,  wafanyakazi  anaotegemea kuajiri, mategemeo  ya  faida au  matumizi  na  kila  kitu  kuhusu  biashara  ya  muombaji.

( f ) Maelezo  ya  maafikiano  ya  kikao  cha  bodi  ya  kampuni ( board  resolution) nakala   moja. Haya ni  maelezo  kwa  ufupi  yanayothibitisha  bodi  ya  kampuni  kuridhia  kampuni  kusajiliwa  na  kituo  cha  uwekezaji  TIC.

( g ) Barua  ya  maombi  nakala  moja. Hii  ni  barua   rasmi  inayolenga  kuonesha  nia  ya  mhusika  ya kutaka  kusajiliwa  na  kituo  cha  uwekezaji.

( h ) Pia  kuna  fomu  ya  maombi  ambayo  hutolewa  na  TIC  wenyewe. Hii  ni  tofauti  na  barua  ya  maombi . Fomu  hii  hulipiwa  dola  100 kupitia  akaunti  namba  A/C 8702006002000  Standered  Chrtered Bank.

3.  BAADHI  YA  BIDHAA  AMBAZO   UTAPATA  PUNGUZO  LA  KODI.

Punguzo  la  kodi unaloweza  kupata  ni  kubwa  kwa  mfano  lipo  la  asilimia  37.5, 25%, 20%,12%  mpaka 100%  n.k.  Baadhi  ya  bidhaa  ni  vifaa  vya  umeme, mabasi yanayobeba  kuanzia  abiria  30 na  kuendelea, vifaa  vya  ujenzi, malori  tela, fenicha, kompyuta, vifaa  vya  uvuvi  na  madini, vifaa  vya  elimu  na  vitabu, vifaa  vya  kilimo vifaa,  vya  mawasiliano kama  simu  na  vile  vya  utangazaji  kama  studio , vifaa  vya  usafirishaji  na  utalii  na  vingine  vingi  ambavyo  sikutaja.

Hii  ni  namna  ya pekee  ya  kufaidi  fursa  ambayo  baadhi  ya  wafanyabiashara  hasa  wenye  asili   ya  Asia  wamekuwa  wakifaidi. Aidha  kuhusu  nyaraka  nilizoeleza  hapo  juu kuwa zinahitajika  katika usajili  wapo  watu  ambao  huziandaa   zote na hivyo hamna  usumbufu  wowote katika kukamilisha  usajili.

Baada  ya  kukamilisha  nyaraka hizo basi   zitawasilishwa  Kituo cha  Uwekezaji  Tanzania ( TIC)  kilichpopo  mtaa  wa  Shaaban Robert plot No 9, opposite  na  Shule  ya  bunge, Dar  es  salaam.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

                                           TANGAZO   MUHIMU                                                
VIWANJA     NA     NYUMBA          ZINAUZWA.
·        
WANASHERIA   WETU   WATAKUANDALIA   MIKATABA  YOTE  BURE  NA    KUKUSIMAMIA  MPAKA   MANUNUZI    YAKAMILIKE   BURE.
·        
UHALALI   WA  NYARAKA   NA   UMILIKI   UMETHIBITISHWA  NA                        WANASHERIA  WETU.
·        
UTAPEWA  MTU  WA  KUKUSAIDIA  KUFANYA  TRANSFER   KWA  HARAKA         BURE.
·        
IKIWA   UTATOKEA   MGOGORO  NDANI   YA  MWAKA  TANGU  TAREHE  YA       MANUNUZI    UTAPEWA   WAKILI   WA   KUSIMAMIA  MGOGORO    BURE
                                                        0784482959.

 KUONA   BOFYA  HAPO  JUU    MWANZO  WA   BLOG.



0 comments:

Post a Comment