Tuesday, 21 July 2015

NI MUHIMU SANA MFANYABIASHARA/MJASIARIAMALI/MNUNUZI WA BIDHAA KUYAJUA HAYA.


Image result for BIDHAA


NA  BASHIR  YAKUB - 

Ipo  sheria moja  iitwayo  Sheria  ya Uuzaji  wa  bidhaa Sura  ya 354. Ni  sheria  ambayo  hutoa majibu  ya  miamala ya  kibiashara  hasa  kwa namna  ya  kimikataba. Ni  muhimu  sana  kwa  wajasiriamali  kujua  mambo  yaliyo  kwenye sheria  hii  ili  kuepuka  migongano  na  migogoro  ya  kibiashara.Sheria  hii hueleza  jambo  fulani likitokea  hivi  kati  ya  muuzaji  na  mnunuzi  nani  ana  haki  na mengine  mengi  kama  nitakavyoonesha  hapa.Ili  ujumbe  kufika  vyema  nitaeleza  kwa  mtindo  wa  masomo.

1.SOMO  LA  KWANZA.

Umefanya  mkataba  na  mtu  wa  kukuuzia  magunia 20  ya  karanga na mmesaini  mkataba  tayari. Bila  kujua  kumbe  wakati mnasaini mkataba  magunia  matano  yameibiwa  kule  mlikoyaacha  stoo baada  ya  kuyakagua. Wakati  mkitokea  kusaini  mkataba ili  ukachukue  mzigo  wako  mnakuta  gunia tano  kati  ya  ishirini zimeibiwa.Kwakuwa  mlishakagua hapo mwanzoni na  ukaridhika na  kwakuwa tayari mkataba  umesainiwa   muuzaji  anasema  hawezi kurudisha hela  na  hawajibiki  na  lolote  kwakuwa  mkataba  umekamilika   na  wewe  ulishakagua  na  kuridhika. Nani  ana  haki gani  na  sheria  inasemaje.

Kifungu  cha  18  cha  Sheria  ya  Mauzo  ya Bidhaa kinasema  kuwa  mkataba  wa  namna  hiyo  hata  kama  umekamilika  unageuka  na  kuwa haramu(void). Hii  ina  maana  kuwa ikiwa  mnunuzi  alikuwa  hajamlipa  muuzaji  basi  hawezi  kulazimishwa  kulipa  isipokuwa  akitaka  mwenyewe  kwa hiari yake. Lakini  pia  kama  tayari  amelipa  hela  basi  muuzaji  analazimika  kumrudishia  hela  yake.  Mnunuzi  hawezi  kulazimishwa  kuchukua  mali  iliyo  chini  ya  idadi  kwa  kisingizio  cha mkataba  kukamilika. Kuibiwa  hakumhusu  mnunuzi  katika  mazingira  hayo kwakuwa  yeye  alisaini  idadi  kadhaa  na  anatakiwa  kupata  idadi  hiyo.

2.  SOMO  LA  PILI.

Umeagiza  gari  au  kifaa  chochote  kutoka  nje ya  nchi kupitia  mtandao.  Kutokana  na  maelezo  yaliyo  katika  mtandao gari  hilo  limetembea  kilomita 2000 na  halijafanyiwa marekebisho  yoyote  kwenye  injini. Kutokana  na maelezo hayo  unakubali  kutuma  hela  na  gari  linatumwa  ambapo  baada  ya  kulipokea  unagundua  kuwa  limetembea  kilomita 9000  na  tayari  limefanyiwa  marekebisho  kwenye  injini.  Sheria  inasemaje  kuhusu  hali  hiyo.

Kifungu  cha  15  cha  Sheria ya  Mauzo  ya  bidhaa  kinasema  kuwa   mnunuzi  anayo  haki  ya  kuamua  kukaa  na  gari  hilo  au  kulikataa  na  kuomba  kurudishiwa  pesa. Ni  kweli  mkataba  unakuwa  umekamilika  kwakuwa  tayari  umelipa  hela  na  wao  wamekutumia  mali  lakini  kifungu  hicho  kinasema  kwasababu  bidhaa  imeshindwa  kufanana  na  maelezo (description) yaliyotolewa  basi mnunuzi  anayo  haki  ya  kujitoa  katika  mkataba  huo na  kurudishiwa  hela  yake.  Na  hii  si  kwa  kuagiza  gari  nje  ya  nchi  tu  bali  hata  hapa nchini  ukinunua  bidhaa  ambayo  ina  maelekezo  kuwa  ina  hiki  ina  hiki  na  kile  halafu  baada  ya  kununua   unagundua  kuwa  muuzaji  alivyosema au ilivyoandikwa    haiko hivyo basi  sheria  inakuruhusu  kurudisha  bidhaa  hiyo na  kupewa  hela  yako  au  bidhaa  nyingine  ikiwa  utataka  hivyo.

3. SOMO  LA  TATU.

Umenunua  gari  kwa  mtu  na  baada  ya  kununua  unaamua  kulifanyia  marekebisho  makubwa   kwa  kutumia  kiasi  kingine kikubwa  cha  fedha .      Baadae  inakuja  kugundulika  kuwa  gari  hilo  lilikuwa  limeibiwa  na  wenye  nalo  wanamtaka  mnunuzi  kuwarudishia  gari  lao  haraka na anawarudishia.  Swali  hapa ni  mnunuzi  ana  haki  gani  kwa  aliyemuuzia  kuhusu  gari lenyewe  na  ana  haki  gani  kuhusu gharama   za  matengenezo   alizokuwa ametumia .

Kifungu  cha             14(a)  cha  Sheria  ya  Mauzo  ya  Bidhaa  kinasema  kuwa muuzaji   alikiuka  masharti  ya  umiliki. Kutokana  na  hilo  kwanza  anatakiwa  kumrudishia  mnunuzi  hela  yake ya  ununuzi  wa  gari  na  pili  anatakiwa  kumrudishia  gharanma  zote  za  matengenezo  alizotumia  kurekebisha  gari  hilo.
Kwa  leo  masomo   matatu  yanatosha .  Nimetolea  mifano  ya  magari  na  magunia  ya karanga  lakini   ifahamike  kuwa maelezo  haya yanatumika  katika  bidhaa  yoyote  ile .  Na zaidi ifahamike  kuwa ikiwa  anayetakiwa  kurudisha  haki  ameshindwa  kufanya  hivyo  basi  sheria  itamlazimisha  kufanya  hivyo  kwa  kutumia  vyombo  vyake. Itaendelea  tena.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com
                                           TANGAZO   MUHIMU                                                
VIWANJA     NA     NYUMBA          ZINAUZWA.
·        
WANASHERIA   WETU   WATAKUANDALIA   MIKATABA  YOTE  BURE  NA    KUKUSIMAMIA  MPAKA   MANUNUZI    YAKAMILIKE   BURE.
·        
UHALALI   WA  NYARAKA   NA   UMILIKI   UMETHIBITISHWA  NA                        WANASHERIA  WETU.
·        
UTAPEWA  MTU  WA  KUKUSAIDIA  KUFANYA  TRANSFER   KWA  HARAKA         BURE.
·        
IKIWA   UTATOKEA   MGOGORO  NDANI   YA  MWAKA  TANGU  TAREHE  YA       MANUNUZI    UTAPEWA   WAKILI   WA   KUSIMAMIA  MGOGORO    BURE
                                                        0784482959.

 KUONA   BOFYA  HAPO  JUU    MWANZO  WA   BLOG.

0 comments:

Post a Comment