Monday 20 July 2015

KESI YA MRAMBA MWANZO MWISHO


Image result for kesi ya mramba

NA BASHIR  YAKUB - 

Wiki  chache zilizopita  tarehe  6  JULY  2015  mahakama  ya  Kisutu  ilitoa  hukumu  katika kesi  maarufu  na  ya  muda  mrefu   iliyokuwa  ikiwakabili  mawaziri  wa  zamani  wawili  na  katibu  mkuu  mmoja.  Blog  hii  iliripoti  kwa  ufupi  sana  kuhusu  matokeo  ya  kesi  hiyo    na  kuahidi  kutoa  ufafanuzi  wa  kitaalam  hapo  baadae  kupitia  wanasheria  wake. Kwakuwa   blog  hii  imekuwa  mstari  wa  mbele  kueleza  masuala  ya  msingi   ya  kijamii yakiwemo  yale  ya  kisheria  ambayo  hayapatikani mitandao  mingine  ya  kijamii  imeona  ni  muhimu kuufafanulia  umma nini kilitokea  katika kesi  hii  mwanzo  hadi mwisho.  Tunaanza  hivi.

1.NANI  WALIKUWA  MAHAKIMU  KATIKA KESI  HIYO.

Walikuwa  mahakimu  watatu. Wa  kwanza  ni S,M Rumanyika  hakimu  mkazi  mwandamizi ( PRM), Wa  pili  ni  S. Kinemela hakimu  mkazi  mwandamizi  Na ndugu  Utamwa  kama  hakimu  mkazi  mwandamizi ( PRM)  japo  kwasasa  ni  jaji  wa  mahakama  kuu. Kesi  husika  ilikuwa  kesi  Namba  1200 ya  mwaka  2008. Mahakama  iliyosikiliza  kesi  hiyo  na  kuitolea  maamuzi ni mahakama ya hakimu   mkazi ( RM),kisutu.

2. NANI  WALIKUWA  WASHITAKIWA .

Mshitakiwa  wa  kwanza  alikuwa  ndugu  Basil  Mramba Pesambili   aliyeshitakiwa  kwa  nafasi  yake  ya   uwaziri  wa  fedha  na  uchumi   wakati  makosa  yanatendeka. Wa  pili  alikuwa  ndugu Daniel Aggrey  Ndhira  Yona  aliyeshitakiwa  kwa  nafasi  yake  ya  uwaziri  wa  nishati  na  madini  wakati    makosa  yalipotendeka. Na  wa tatu  alikuwa  ndugu Grey  Shwaibu  Mngonja  aliyeshitaiwa  kwa  nafasi  yake  ya  ukatibu  mkuu  wa   wizara  ya  fedha  na  uchumi  wakati  makosa  yakitendeka.

3. NI  MAKOSA  GANI  WALISHITAKIWA  NAYO.

( 1 ) Kosa  la  Kwanza,  ni  kuwa  ndugu  Mramba   akiwa  waziri  wa  uchumi  na  fedha  na  ndugu Yona  akiwa  waziri  wa  nishati  na  madini  wote  kwa pamoja  kati  ya  August 2002  na  June  2004   bila  kufuata  utaratibu  walitoa  zabuni  na  kuingia  mkataba  na  kampuni  ya MS  ALEX  STUWART kufanya  kazi  ya ukaguzi  wa  madini  yanayozalishwa  kinyume  na  sheria  ya  manunuzi  ya  umma  Sura ya 410  ya  2002,  na  kinyume  na  sheria  ya    madini Sura  ya  123  ya  2002  na  kuathiri  maslahi  ya  Jamhuri  ya  Muungano  wa  Tanzania.

( 2 ) Kosa  la  pili,  May  2005 kwa nyadhifa  zao  hizohizo  bila  kufuata  utaratibu waliiongezea  mkataba  wa  ukaguzi  wa  madini  kampuni  hiyohiyo ya  Alex  kwa  miaka  miwili zaidi  kuanzia  tarehe  14 JAune 2005  hadi  tarehe  23 June 2007. Na  kuwa  nyongeza  ya  muda  ilifanywa   na  watuhumiwa  kwa  kuizunguka  kamati  malum  ya  serikali ( Government  Negotiating  Team GNT)   iliyokuwa  imeteuliwa  kusimamia  mchakato  huo.

( 3 ) Kosa  la  tatu, ni  kuwa kati  ya   March  na  May 2005  mawaziri  hao  wawili kwa  nia  mbaya  walizuia  taratibu  halali  za  kimkataba  zilizopendekezwa  na  mwanasheria  mkuu  pamoja  kamati  ya  serikali  ( Government  Negotiating  Team GNT)  iliyokuwa  imeteuliwa  kwa  kazi  hiyo.

(4 ) Kosa  la nne, December  2003  mshitakiwa  wa kwanza  Mramba  na  watatu Mgonja  bila  kufuata   utaratibu walitoa  tangazo  la  serikali GN No. 423/2003  wakitoa  msamaha  wa  kodi  kwa  kampuni  ya  Alex Stuwart  na baadae  tangazo  namba  424/2003  yote  kwa  kuipendelea  kampuni  hiyo isilipe  kodi.

( 5 ) Kosa  la  tano,  ni  kuwa Mramba  na Mngonja  bila  kufuata  utaratibu  tarehe 15/ 10/ 2004 walitoa  tangazo  jingine  la  msamaha  wa  kodi  kwa  kampuni  hiyohiyo  GN No. 497/2004  na  GN NO. 498 /2004

( 6 ) Kosa  la  la  sita,   ni  kuwa  watuhumiwa  wote  watatu  kati  ya  mwaka  2003  na 2007 kwa  nafasi  zao  waliisababishia  serikali  hasara  ya  Tshs 11, 752, 350, 148/=  ikiwa kama  kodi( income & withholding tax) .
Kwa ujumla  makosa  yalikuwa  kumi  na  moja  lakini   kwakuwa  mengi yanafanana  ukiyaunganisha  unapata  hayo sita  niliyoeleza.

4. NI  MAWAKILI  GANI  WALISIMAMIA  KESI  HIYO.

Upande  wa  mashtaka kulikuwa  na  Wakili  wa  serikali  Mwandamizi Osward Tibabyekomya  akisaidiwa  na  wengine  wakiwemo  wa  Taasisi  ya  kuzuia  na  kupambana  na  rushwa. 
Upande  wa  wa  utetezi  Mramba  alitetewa  na  mawakili  wawili H.H.H Nyange  na P. Swai. Ndugu  Yona  alitetewa  na  na  mawakili  wawili  pia C. Tenga  na  E. Msuya wakati  Mngonja  naye  akitetewa  na  mawakili  wawili  Profesa  Shaidi  na Malimi.

5. NANI  WALIKUWA MASHAHIDI  UPANDE  WA  MASHITAKA  NA  WALISEMA  NINI ?.

Mashahidi  upande  wa  mashitaka  ni  mashahidi  ambao hutoa  ushahidi  ili  kumtia  hatiani/kumfunga  mtuhumiwa.

( A ) SHAHIDI  WA KWANZA. Huyu   ni  ndugu  Nyelo  Martin  Hiza. Kipindi  makosa  yanatendeka  alikuwa  mkuu  wa  idara ya  sheria  na  baadae  kamishna  wa  madini  katika  wizara  ya nishati  na  madini. Anasema  yeye  alikuwa mmoja  wa wana timu iliyokuwa  ikishughulikia  mchakato  wa kupatikana  kwa  kampuni  ya  ukaguzi  wa  madini. Anasema  kwamba  kampuni  iliyopatikana ilikuwa Alex Stuwart. Anasema  pamoja na  kupatikana  kampuni hiyo  lakini ilikuwa  haina  mtaji na  yeye  haraka  aliripoti  jambo  hilo  kwa  mtuhumiwa  wa  pili Daniel  Yona. Anasema  pia   viwango  vya  tozo  za  kampuni  hiyo  vilikuwa  vikubwa na  walitoa  mapendekezo  kuhusu  hayo yote  ambapo  hata  hivyo mapendekezo  yao hayakuzingatiwa na  watuhumiwa. 

Pia  anasema alipewa  kazi  ya  kutafiti  utendaji  wa  kampuni  hiyo  ambapo  anasema  aligundua utendaji  wake  ulikuwa  chini  ya 15%  na  alitoa  taarifa  hiyo  ambayo  hata  hivyo nayo  ilipuuzwa  na  watuhumiwa. Anasema  baadae  kampuni  hiyo ilielemewa na  kushindwa  kabisa  kutekeleza  majukumu yake  ambapo  walitoa  mapendekezo  kuachana  nayo  na  kutafuta  mzabuni  mwingine.  Hata  mapendekezo  hayo  nayo hayakuzingatiwa  ambapo  mawaziri  hao  waliamuru  mchakato  kuendelea.

( B ) SHAHIDI  WA PILI. Huyu  ni Betha. H. Soka.Yeye  alikuwa  mkurugenzi  wa  kitengo  cha  manunuzi  ya  umma(PPRA) na mmoja wa  wanatimu  iliyokuwa  ikiratibu  mchakato  huu  wa  kampuni  ya kukagua  madini. Anasema  aliitwa benki  kuu  kujadili mchakato  wa  mkataba wa kampuni  ya  ukaguzi  wa  madini.  Anasema jambo    la  kushangaza   masharti  ya  mkataba  yalikuwa  sio  ya  kujadili ila  yalikuwa tayari  yameandaliwa na  sharti  mojawapo  ndani yake likiwa  msamaha wa  kodi. Anasema alipofika katika  kikao  hicho  wakurugenzi  wa  kampuni  ya  Alex  walikuwa  tayari  nao  wapo pale. Hivyo yeye  alipewa  tu  mkataba kupitia   na  hivyo hakuchangia  katika  kuuandaa.  

Anasema  kwa kuupitia  alishauri  kutokuwepo  kwa msamaha  wa kodi. Anasema  alishauri  hivyo kwa  kutambua   kuwa  watuhumiwa  hawakuwa  wanasheria  na  hivyo walistahili  kushauriwa kuhusu  hilo.  Hata  hivyo  pamoja  na  ushauri  huo  wa  kitaalam  bado  kifungu  cha  msamaha  wa kodi  kiliendelea  kubaki. Anasema TRA  nao  walishauri  kuwa hakuna  msamaha  wa  kodi. Anasema baadae alikuja  kugundua  kuwa  ushauri  wao  uliombwa  wakati  ambapo  mtuhumiwa  wa  Mramba  na  Yona  walikuwa  tayari  wameingia  mkataba  na  kampuni  ya Alex. Waliingia mkataba  kwanza  halafu  ndio  wakaomba  ushauri, kitu ambacho kiliufanya  ushauri  wao kuwa  sawa  na  bure.

( C ) SHAHIDI  WA  TATU. Huyu  ni Aggrey  Temba. Yeye  alikuwa  mwanasheria  mkuu  wa  TRA. Anasema  aliombwa  ushauri  kuhusu  msamaha  wa  kodi  kwa  Kampuni  ya  Alex.  Anasema  walishauri  hakuna  msamaha  wa kodi  na  hata  kamishna  mkuu  wa  TRA  alishauri  hivyo. Anasema  wizara ya  fedha   kupitia  Mramba  ilikubali  kuondoa  kipengele  cha  msamaha  wa  kodi  ambacho  baadae  kumbe  kilirudishwa  kinyemela  na  Mramba  pamoja na  wenzake. Anasema  baadae  hata  wao  TRA  waligundua  kitu kingine kuwa  hata  ushauri  walioombwa ilikuwa ni  baada  ya  watuhumiwa  kuwa  tayari  wamekamilisha  mkataba  hivyo ushauri  
wao  ilikuwa  bure.

( D  ) SHAHIDI  WA NNE. Huyu  ni George A.C Ntigiti. Yeye alikuwa  mhasibu  mkuu  wa serikali .  Anasema  alipata  taarifa  kutoka  TRA   kuhusu  jambo  hilo  naye  mara  moja  akawashauri  watuhumiwa  kuwa  hakuna  msamaha  wa  kodi  kwa  kampuni  hiyo.

( E ) SHAHIDI  WA  TANO. Huyu  ni Grey  Lazaurus  Mwakalukwa. Yeye  ni mkurugenzi  mkuu  wa  STAMICO. Anasema  yeye  alishauri  kuhusu  tozo  za  kampuni  hiyo. Anasema  alihoji  watuhumiwa  kuhusu   kuikubali  kampuni  hiyo  iendelee   kuitoza  serikali  tozo  kubwa  kuliko  inavyofanyika sehemu  yeyote  duniani. Alishauri  kuwa  ili kujiridhisha  wafanye  utafiti  katika  nchi  nyingine  ambapo  walifanya  utafiti  nchi  za Australia, Peru, Chile  na  South  Africa  na kugundua  kuwa  tozo  ziko  chini  kuliko   kampuni  hiyo ilivyokuwa  ikiitoza serikali  ya  Tanzania.  Kutokana na  hilo  waliwashauri  watuhumiwa  kuachana na  kampuni  hiyo na  kutangaza  tenda  upya  jambo ambalo  halikufanyika.

( F  ) SHAHIDI  WA SITA. Huyu ni  Kambona  kutoka  mamlaka  ya  kuzuia  na  kupambana  na  rushwa(TAKUKURU).  Anasema  kuwa   katika  upelelezi  wake  aligundua  kuwa  watuhumiwa  walishauriwa  karibia  na  kila idara  kuwa  kusiwepo na  msamaha wa kodi  kwa  kampuni  ya Alex.  Anasema  hata  hivyo  katika  upelelezi  wake  aligundua  kuwa  mmoja  wa wanahisa  wa kampuni  ya  Alex  aitwaye  GEORGE  alikuwa  MTOTO  WA MRAMBA.

Mashahidi  jumla  walikuwa  13   lakini   hao  niliotaja  ndio  walikuwa  wa msingi  zaidi. Pamoja  na  hayo  hata  hao  ambao sikutoa  maelezo  yao nao walitoa  ushahidi  unaofanana  na  wa  hawa ambapo   walieleza  kutokuwepo  msanaha  wa  kodi, uwezo  mdogo  wa kampuni  hiyo,   kukiukwa  kwa taratibu  katika  kuipata  kampuni  hiyo  na  kuiongezea  mkataba  mpya kinyemela.
Zingatia, mashahidi  waliyaeleza  haya  kwa  kutoa  nyaraka  kusapoti kila wanachosema.

6. ALIVYOJITETEA  MRAMBA.

Kwa  tuhuma  hizo  na  ushahidi huo  mramba  alijitetea  kwa  kusema  kuwa,  kwanza  yeye kama  waziri  wa  fedha na uchumi sheria  imemruhusu  kutoa  msamaha wa  kodi  na  hivyo  alitumia  sheria hiyo  kutoa  msamaha huo. Pili  alisema          alipata   maelekezo  kutoka  ikulu   kwa  rais  Mkapa  yakimtaka   kuendelea  na  mchakato  mara  moja  na  hivyo  alikuwa  akitekeleza maagizo  ya  mkubwa  wake.  Tatu  pesa  ya  awali  iliyolipwa  kwa  kampuni  hiyo  kutoka  benki  kuu  kiasi cha  dola  milioni  moja   anadai  hakuhusika  kuishinikiza  benki  kuu  kulipa  fedha  hiyo  kwa  kuwa  hana  uwezo   wa kuishinikiza    benki  ambayo  wakuu  wake  hawawajibiki  kwake  isipokuwa   kwa  rais  .  Pia  anakubali  kuomba  ushauri  TRA  kuhusu  msamaha  wa  kodi  lakini  anasema  kuwa  hakuwahi  kupokea  ushauri  wao  kama  wao  wanavyodai.

7. ALIVYOJITETEA  DANIEL  YONA.

Naye  kubwa  zaidi kwake  ni  kuwa  rais  Mkapa  aliwaambia  kutekekeleza  mchakato  huo  kwa  haraka   na  ndio  maana  waliamua  kuendelea  nao  haraka. Utetezi  wake  ni  sawa  na  wa Mramba  katika  nukta  nyingi kwakuwa  wote walishitakiwa  kwa  makosa  yanayofanana.

8. ALIVYOJITETEA  GRAY  MNGONJA.

Anasema  kuwa  kipindi  akiwa  katibu  mkuu  kulikuwa na  makatibu  wakuu  wa tatu  kwa wakati  mmoja  ambao  walifanya  kazi  bila  mipaka  maalum  ya majukumu. Anasema  ushiriki  wake  katika  kuandaa  matangazo ya  serikali  yaliyotoa  msamaha  wa  kodi     alikuwa  akitekeleza  maagizo  ya  bosi  wake  Mramba.  Anasema yeye  aliagizwa  kuandaa na  akafanya  hivyo. Na  kusingekuwa  na  namna  ya  kutofanya  hivyo.

Zingatia, hawa nao  waliyaeleza  haya  kwa  kutoa  nyaraka  kusapoti kila wanachosema.

9. MAWASILISHO  YA  MWISHO  YA  MAWAKILI  WA  WA AKINA  MRAMBA.

Wakati  wakifunga  utetezi  mawakili  wa  washitakiwa  walitumia  kesi  ya  JONAS NKIZE v R (1992) TLR 213  inayosema  kuwa  lolote  ambalo  limefanyika  au  kutofanyika(commission & omission) lazima  liwe  limeelezwa  katika  sheria.  Wakasema  kutokana  na  hilo   sheria inasema  kuwa kodi  ambayo  haijalipwa  huwa  haiitwi  hasara   na  hivyo  ni  makosa  na  sio  kweli kusema  watuhumiwa  waliingizia  serikali  hasara.Wakasisitiza  kuwa kodi iliyosamehewa  na  watuhumiwa  ilikuwa  haijaingia  mikononi  mwa  serikali  na  hivyo  sio  hasara na  ni  makosa  kusema watuhumiwa  wameiingiza  serikali  hasara.

Pili  kuhusu  matumizi mabaya  ya  ofisi  mawakili  wakatunmia   kesi  ya PETER  PROTASE v R (1970) HCD 169  ambayo  inasema  kuwa  matumizi  mabaya  ya  ofisi  ni    tendo  ambapo  mtumishi  wa  umma  kwa  nia  mbaya,  bila  kufuata  sheria  na  kwa  malengo  binafsi  anakiuka  haki  za  wengine na  kusababisha   hasara. Kwahiyo  wakasema  kuwa  kwa  tafsiri  hiyo  hakukuwa  na  ushahidi  kuwa  watuhumiwa walikuwa  na  nia  mbaya,  na  wala  ushahidi kuonesha  maslahi  binafsi  na  wala  hakukuwa  na  hasara yoyote.  Kwa  tafsiri  hii  wakasema  kuwa  matumizi  mabaya  ya  ofisi  hayakuwepo na  wakaiomba  mahakama  isilikubali  kosa  hilo.

10. MRAMBA  NA  YONA  WATIWA  HATIANI.

Kwakuwa  watuhumiwa  walijitetea  na kubwa  zaidi  wakisema  wao  hawakuwa na  mamlaka  katika   kusamehe  kodi  bali  walipokea  maelekezo  kutoka  kwa  rais  Mkapa  mahakama  ilitakiwa  ilijibu  hilo kwanza.
Mahakama  ilisema  hivi, watuhumiwa  wamekiri  kuwa  wao  ndio  walioteua  kamati   ya  kutafuta  mzabuni,  na kamati  hiyo  iliwajibika  na  kuripoti  kwao   kila  hatua. Kwa  nukta  hiyo  mahakama  ikakataa  kuwa  si  kweli  kuwa  hawakuwa  na  mamlaka  katika  mchakato  kama  walivyodai.  Mahakama  ikasema  zaidi  kuwa  ni  kweli  rais  Mkapa  aliruhusu   kuendelea  kwa  mchakato  haraka  lakini  alifanya  hivyo  baada  ya  watuhumiwa  kuwa  wamemshauri   kuhusu  jambo  hilo  kama  washauri  wake. Na  mbaya  zaidi  ushahidi  unaonesha  kuwa  taarifa aliyopelekewa  mkapa  na  watuhumiwa  kuhusu  kampuni  hiyo   haikugusia  lolote  kuhusu  msamaha  wa  kodi   wala  tozo  za  juu  zilizokuwa  zikitozwa  na  kampuni  hiyo. 

Hivyo  kutokuwepo  kwa  taarifa  hizo  kulimfanya  mkapa  kuamini  kuwa  ni kampuni  safi  na  hivyo  kutoa  maagizo  ya  kuendelea    haraka  na  mchakato.
Lakini  zaidi  mahakama  inasema  kuwa ushahidi  unaonesha  kuwa  rais  Mkapa alipelekewa  taarifa  kuhusu  mchakato na  kutoa  amri  ya  kuendelea  wakati  tayari   mkataba  ukiwa  umeshafanyika  na  kampuni  imeshasamehewa  kodi. Kwa  hiyo  taarifa hiyo  na  ruhusa  ya  Mkapa  ya  kuendelea  haraka  haikuwa  na  maana  yoyote.
Swali  jingine  lililojibiwa  na  mahakama ni    iwapo  msamaha  wa  kodi  ulikuwa  halali  kwa  kampuni  hiyo.

Mahakama  ilisema  kuwa  ni  kweli  waziri  ana  mamlaka  kisheria  ya  kusamehe  kodi  lakini  ikaongeza kuwa mamlaka  hayo  yana  ukomo. Ikasema  kuwa  haimaanishi  kuwa  kwa  kuwa sheria  hiyo   inamruhusu  waziri asemehe  kodi  basi atasemehe  kodi  kila  atakapojisikia  kufanya  hivyo   au  akili  yake  atakavyomtuma. Ikasema  hata  watuhumiwa  wanalifahamu  hilo  na  ndio  maana walikuwa  wakiomba  ushauri  kuhusu jambo  hilo  japo  hawakuuzingatia.  Ikasema  suala  la  kodi  ni  suala la kiufundi  si  la  kuamuliwa  kwa  utashi. Kwa nukta  hiyo  mahakama  ikasema  hakukuwa  na sababu  za  kutoa  msamaha  wa  kodi kama  watuhumiwa  walivyofanya.

Kuhusu  tozo  kubwa  iliyokuwa  ikitozwa na  kampuni  hiyo  mahakama  imesema  kuwa watuhumiwa  napo  walikataa  kuzingatia  ushauri  waliopewa  na  wataalam  pamoja  na  utafiti  uliofanyika  katika  nchi  nyingine  na  kuona  taifa  linanyonywa  na  kampuni  ya Alex.

Hoja  kuwa  serikali  haikupata  hasara  nayo  ilijibiwa .     Mahakama  ilisema  kwamba  ni  kweli  kodi  iliyosamehewa  kisheria  haiitwi  hasara.  Lakini  ikasema  kuwa   isiyoitwa  hasara  ni  ile  kodi  iliyosamehewa   kihalali  na  kwa  kufuata  utaratibu.  Ikasema  kuwa  kodi  iliyosamehewa  bila  uhalali  na  bila  kufuata  utaratibu  hiyo  ni hasara  na  hivyo   ni  kweli  watuhumiwa  waliliingizia  taifa  hasara.  Kwa hoja  hizi  Mramba  na  Yona  wakakutwa  na    hatia.

11. KUACHIWA HURU  KWA  GRAY  MNGONJA.

Sababu  kubwa  za  kuachiwa  Mngonja  ni,  kwanza  wakati    akiwa  katibu  mkuu   hakuwa  peke yake  kwani  walikuwepo  makatibu  wakuu  wengine  wawili  yeye  akiwa  watatu. Wote  mmoja  mmoja  kuna  namna  walivyoshiriki  katika  mchakato  huu  na  hivyo  kesi haikumgusa  moja  kwa  moja.  Pili yeye  kama  alivyojitetea  alikuwa  akitekeleza  maagizo  ya  Mramba  aliyekuwa  bosi  wake  na  hakuwa  na  namna  ya  kukataa. Tatu  hakuhusika    katika  kusamehe  kodi, hakuhusika katika  kuongeza  muda  wa  mkataba na   wala  hakuhusika katika  kuipa    kampuni  hiyo  mkataba  mwanzoni.  Yeye  alipewa  maagizo  ya  kuandaa  matangazo  ya  serikali  ya msamaha  wa  kodi na  akafanya  hivyo. Hii ndiyo pona  yake

12. ADHABU  WALIZOPEWA MRAMBA  NA  YONA.

( 1 ) Mramba  alipatikana  na  hatia   katika  kosa  la  kwanza  hadi  la  kumi  na  moja  . Amehukumiwa  kifungo  cha  miaka  mitatu  kwa kila  kosa.  Hata  hivyo   mahakama  imetoa  amri  ya  adhabu  hiyo  kutumikiwa  kwa  pamoja  (concurrently) na  hivyo  kumfanya  Mramba kutumikia  miaka  mitatu tu  kwa  ujumla badala  ya  kila  kosa  miaka  mitatu.
Kosa  la  11  atatakiwa  kulipa  faini  ya  Tshs  milioni  tano  na  akishindwa atumikie  miaka mingine mitatu  jela.

( 2 ) Katika  kosa  la 1 -4 Daniel  Yona  amehukumiwa  kifungo  cha  miaka  mitatu  kwa  kila  kosa  ambazo  zitatumikiwa  kwa  pamoja (concurently)  yaani   miaka  mitatu  tu.  Kosa  la  11  naye  atalipa  kiasi cha Tshs  milioni  tano  au  akishindwa  atumikie  miaka  mingine mitatu  jela. Hivyo  ndivyo  ilivyotokea.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

                                           TANGAZO   MUHIMU                                                
VIWANJA     NA     NYUMBA          ZINAUZWA.
·        
WANASHERIA   WETU   WATAKUANDALIA   MIKATABA  YOTE  BURE  NA    KUKUSIMAMIA  MPAKA   MANUNUZI    YAKAMILIKE   BURE.
·        
UHALALI   WA  NYARAKA   NA   UMILIKI   UMETHIBITISHWA  NA                        WANASHERIA  WETU.
·        
UTAPEWA  MTU  WA  KUKUSAIDIA  KUFANYA  TRANSFER   KWA  HARAKA         BURE.
·        
IKIWA   UTATOKEA   MGOGORO  NDANI   YA  MWAKA  TANGU  TAREHE  YA       MANUNUZI    UTAPEWA   WAKILI   WA   KUSIMAMIA  MGOGORO    BURE
                                                        0784482959.

 KUONA   BOFYA  HAPO  JUU    MWANZO  WA   BLOG.






0 comments:

Post a Comment