Thursday 18 June 2015

SHERIA INAMRUHUSU MKOPAJI KUJIUZIA MWENYEWE KIWANJA/NYUMBA YA DHAMANA.

Image result for MKOPO

NA  BASHIR  YAKUB - 

Wiki  kadhaa  zilizopita   nilipigiwa  simu  na  mama  mmoja  akitaka  nimpe  ushauri  wa  sheria  kuhusu  jambo  fulani. Nilifanya  miadi  naye   na tukafanya  mazungumzo. Kubwa  kuhusu  shida  yake  ilikuwa  ni  tatizo  la  mkopo ambapo  benki  moja imeuza  nyumba  yake  maeneo  ya  Kinondoni  Dar  es  saaam.  Wasiwasi  wake  ulikuwa  ukiukwaji  wa  taratibu  za  mauzo  ya  nyumba  yake  na  hivyo  akitaka  kujua  afanye  nini. Maswali  yake  yalikuwa  mengi  na  nilimjibu  kwa  kiwango  cha  juu.

Pamoja  na  hayo  kilichokuwa  kikimpa  shida  sana   na  kuamini  kuwa  kulikuwa  na  mchezo  mchafu  umefanyika  katika  uuzwaji  wa  nyumba yake  ilikuwa  ni   hatua ya  benki  inayomdai  kujiuzia  nyumba  yake   katika  mnada  wa  hadhara. Alidai  hakuwahi  kuona  mdai  deni  anajiuzia  mali  iliyowekwa kwake kama   dhamana. Alidai  anavyojua   ni  mnada  kutangazwa  na  wenye  nia  hujitokeza  kununua  na  kati  ya  hao  mdai  hawezi  kuwa  mnunuzi.  Aliamini  hatua  ya  mdai  kuwa  ndiye  mnunuzi  ulikuwa  ni  mchezo  uliopangwa  ili   kuchukua  nyumba  yake. 

 Nilimuuliza  kilichomuudhi  zaidi  nini  kwani  sioni  tofauti  kati  ya  mtoa  mkopo  kujiuzia  mwenyewe na  kununua  mtu  mwingine  kwani  kuuza  ni  kuuza  tu.  
Akanieleza ukweli  kuwa  wao  walishampanga ndugu  yao  ambaye  angeweza  kununua  na  kwakuwa  ni  ndugu  kuna  mipango  yao  kama  familia   walishaipanga.  Kwa  hiyo  alihisi  ilifanyika  hila  ili  wao  wasiichukue  tena  nyumba  hiyo  kwakuwa  mdai  naye  alikuwa  akiitaka kwa  udi  na  uvumba . Nilimpa  ushauri  ambao  ningependa  pia  kuushiriki  na  watu  wengine   kupitia  makala  haya   ili  faida  iwe  kubwa.

1.TARATIBU  ZA  KUUZA  NYUMBA KWA  KUSHINDWA  KULIPA  MKOPO.

Nitaeleza  kwa  ufupi  sana .

( a ) Kwanza,  kabla  ya  kuuza nyumba/kiwanja  cha  mtu    ni  lazima  iwe  kweli   mkopwaji   ameshindwa  kulipa mkopo katika  muda  uliopangwa  na  pengine  amepewa  hata  muda  wa  ziada  nao  ameshindwa  kulipa.  Hii  huitwa “DEFAULT”.

( b ) Pili  ni  lazima  taarifa  ya  maandishi  iwe  imetolewa  kwa  mkopaji  aliyeshindwa  kulipa  mkopo  ikieleza  deni  halisi  analodaiwa  namna alivyoshindwa  kulipa  na  kiasi ambacho  hajalipa   pamoja  na  hatua  ambazo  zinalenga  kuchukuliwa. Hii  huitwa  “NOTICE”.

( c ) Tatu uuzwaji  hufanyika  kwa  njia  ya mnada  na  hii  ni  baada  ya  matangazo  kwa  umma. Matangazo  yatatolewa  kwa  umma  na  mwenye nia  atajitokeza  siku  ya  mnada  kwa  ajili  ya  kushindana.

( d ) Bei  itakayouzwa  isiwe  chini  ya  asilimia  25  ya  bei  ya  soko  ya  eneo  husika. Hii  ni  kuzuia  mali  za  watu  kuuzwa  kwa  bei  za  kutupwa
Taratibu  zipo  nyingi  na  nimezieleza  mara  kwa  mara,  kwa  anayetaka  kuona  aandike  neno  SHERIA  YAKUB  BLOG  kwenye  mtandao  afungue  blog  hiyo  atafute  humo  atapata  makala  hizo  na  nyingine  nyingi  za sheria.

2.MTOA  MKOPO  KUJIUZIA MWENYEWE  NYUMBA/KIWANJA  CHA  DHAMANA.

( a ) Kifungu  cha  135( 1 – 5 )   cha  Sheria  ya  Ardhi  kinatoa  maelezo  kuhusu  mkopaji  kujiuzia  ardhi  ya  dhamana.  Kinasema  kuwa  mtoa  mkopo  anayo  haki  ya  kujiuzia  mwenyewe  eneo  ambalo  aliwekeshwa  kama  dhamana  iwapo  mkopwaji  ameshindwa  kurejesha. Hata  hivyo  sheria imetoa  sharti  kuwa  kabla  ya  kufanya  hivyo  anatakiwa  kupata   ridhaa/hiari  ya  mahakama ( Court leave).

( b ) Mkopaji  anapoiomba  mahakama  kujiuzia  eneo  la  dhamana  atatakiwa kuthibitisha  kuwa  hiyo  ndiyo  njia  yenye  manufaa  zaidi  katika  kutimiza  wajibu  alionao  kama  mkopaji.

( c ) Mkopaji  atakapojiuzia  kwa  njia  ya  mnada  inatakiwa  ashindane  kwa  bei  kama  washindani  wengine  na  kama  ananunua  basi  bei  yake  iwe  ndiyo  iliyoshinda   bei  nyingine. Isiwe  kwakuwa  anajiuzia  akajiuzia  kwa  bei  ndogo  huku  akiwaacha  wanunuzi  wengine  ambao  walikuwa  na bei  kubwa  kuliko  yeye. Hili  likitokea utakuwa  mchezo  mchafu.

( d ) Pia  sheria  inatoa  angalizo  kwa  msajili  wa  ardhi  kujiridhisha  kuwa  taratibu  zote za  masharti  ya  mtoa  mkopo kujiuzia  zimefuatwa  kabla  ya  kubadili  hati  na  kuiingiza katika  jina  lake.
Kwa  ufupi  sheria  inaruhusu mtoa  mkopo/mkopaji    kujiuzia  ardhi  iliyowekwa  kwake kama dhamana  na  masharti  ndiyo  kama  hayo  tulivyoona.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

                                           TANGAZO   MUHIMU                                                
VIWANJA     NA     NYUMBA          ZINAUZWA.
·        
WANASHERIA   WETU   WATAKUANDALIA   MIKATABA  YOTE  BURE  NA    KUKUSIMAMIA  MPAKA   MANUNUZI    YAKAMILIKE   BURE.
·        
UHALALI   WA  NYARAKA   NA   UMILIKI   UMETHIBITISHWA  NA                        WANASHERIA  WETU.
·        
UTAPEWA  MTU  WA  KUKUSAIDIA  KUFANYA  TRANSFER   KWA  HARAKA         BURE.
·        
IKIWA   UTATOKEA   MGOGORO  NDANI   YA  MWAKA  TANGU  TAREHE  YA       MANUNUZI    UTAPEWA   WAKILI   WA   KUSIMAMIA  MGOGORO    BURE
                                                        0784482959.

 KUONA   BOFYA  HAPO  JUU    MWANZO  WA   BLOG.



0 comments:

Post a Comment