Thursday, 4 June 2015

NAMNA YA KUZUIA HATI ISIBADILISHWE IWAPO KUNA MTU ANATAKA KUKUZUNGUKA

Image result for TITLE DEED SAMPLE

NA  BASHIR  YAKUB -

Upo wakati ambapo unaweza kuwa katika mazingira  ambapo   hati  ya nyumba/kiwanja ipo  katika  hatari  ya  kubadilishwa kutokana  na  mauzo. Na  hapa  si  lazima  ile  hati  iwe na  jina  lako  hapana. Yawezekana  hati  ina  jina  la  mume na  mume   ndiye  anayetaka  kuuza na  wewe  mwanamke  hutaki  auze  kwakuwa  nyumba/kiwanja  hicho  ni  cha  familia au  si  cha  famlia  lakini una  maslahi  fulani  katika nyumba/kiwanja  hicho. Na  si  lazima  katika kuuza  tu  hata  katika  kuchukua  mkopo. Yawezekana  mwanaume  anataka  kuchukua  mkopo  kwa  kuweka dhamana  nyumba  ya  familia na  mwanamke  hataki  afanye  hivyo.
Si  mwanaume  tu  bali  pia  mwanamke  anaweza  kuwa  anataka  kuuza  au  kutumia  nyumba  ya  familia kwa  ajili  ya  mkopo  na  ikawa  mwanaume  hataki  jambo  hilo. Na  bahati  mbaya sana hataki wakati  si  tu hati  haina  jina  lake  bali pia  haiko  mikononi  mwake. Anayo  huyo  anayehofiwa kutaka  kuuza/kukopea. Unafanyaje  iwapo  hayo  yamekutokea au  yanaelekea  kukutokea .

1.  KUTUMIA  HATI  KWA  MKOPO/KUUZA  BILA  IDHINI YAKO.

Kwa  kawaida  ikiwa  nyumba/kiwanja  kina  hati, leseni  ya  makazi  au  ofa  si  rahisi  kwa  mtu  yeyote kununua  bila  kufika  mamlaka  za  ardhi  kujiridhisha  kuhusu umiliki  na  mambo  mengine  kuhusu  mali  hiyo. Mnunuzi  kawaida  huchukua  nakala ya  ile  nyaraka  na  huenda  nayo  makao  makuu  ardhi  au  manispaa kwa  ajili   ya  kupata  taarifa  kabla  ya kununua. Ikiwa  umeweka  zuio  nitakaloeleza  hapa  chini  basi  moja  ya  taarifa  watakazompa  yule  mnunuzi  ni  pamoja  na  kumueleza  kuwa  eneo  analotaka  kununua  si  salama  kwakuwa  kuna  mtu  ameliwekea  zuio. Hii  ni  taarifa  ambayo  lazima  wampe. Kwa  taatrifa  kama  hii  mnunuzi  hawezi  tena  kuendelea  na ununuzi  na  ikiwa ataendelea  basi  ni  lazima  apate  ridhaa  yako.

Halikadhalika  kwa  mkopo. Si  rahisi  taasisi  ya  fedha  itoe  mkopo kwa  dhamana ya nyumba/kiwanja bila  kwenda  mamlaka  za  ardhi  kujiridhisha iwapo  eneo  hilo ni kweli  ni  la  mkopaji  na  ikiwa kuna  zuio  lolote. Wanapofika  ardhi  kujua  hadhi  ya  eneo  ni  lazima  kama  umeweka  zuio wataambiwa  kuwa  kuna  zuio  na  hiyo  inawatosha  kutokubali  kutumia  eneo  hilo  tena  katika  kutolea  mkopo au  kutafuta  ridhaa  yako  kwanza.

Zuio  hili  hufanya  kazi  hata  kama  eneo  limeshauzwa. Kama  limeuzwa  lakini  hati  haijasbadilishwa basi  waweza  kuzuia  isibadilishwe mpaka  muafaka  upatikane. Zuio  hilo huitwa “Caveat”. Hili  si  zuio  la  kwenda  mahakamani hapana  ni  hapohapo  ardhi  tu.
2.   NINI  MAANA  YA  ZUIO “CAVEAT”.

Zuio ”caveat” ni usitishwaji wa muda ambao huwekwa ili kuzuia mabadiliko yoyote   katika hati. Kama maana  yenyewe inavyojieleza  huu unakuwa ni usitishwaji wa muda  ambao unalenga  kulinda  maslahi ya  mtu aliyeomba  zuio.Kuitwa  zuio  la  muda haimaanishi  kuwa  mtu akizuia   itakuwa  ni mwezi mmoja  au  miwili basi, hapana. Ni  zuio  la  muda  kwakuwa  haliwezi kukaa milele  lakini  mtu akishaliweka  linaweza  kukaa  hata  miaka  mingi  kutegemea  na  sababu  za  zuio  hilo.

3. NANI NA NANI WANA HAKI  YA  KUZUIA  HATI  ISIBADILISHWE.

Yeyote  mwenye maslahi ya  kisheria  katika  nyumba/kiwanja  husika ana  haki  ya  kuzuia  mauzo, na  hati  isibadilishwe. Mwenye maslahi  ni  nani. Mwenye  maslahi  ni  kama  mke  au  mume  iwapo  eneo  ni  la  familia Pia taasisi  yoyote ya  fedha  iwapo eneo  hilo  inalimiliki  kwa  dhamana  na  sasa  wenye  nalo  wanataka  kulitumia kuuza au  kukopea  pengine  kabla  ya  kumaliza  deni  lao, Pia msimamizi  wa  mirathi na  warithi wote wana  maslahi  katika  mali  za marehemu na  kila mmoja  kwa  nafai  yake  anaweza kuweka, kwa  kutaja  ni  machache. Hawa  wote  wana  maslahi  na  wanayo  haki  ya  kuweka  zuio kuzuia amtu  asinunue,asikopee au  aliyenunua  asiwe  na  uwezo  wa  kubadili  hati.

4.  WAPI  UPELEKE  MAOMBI   YA  KUZUIA  HATI  ISIBADILISHWE.

Mamlaka  za ardhi  ni mamlaka  ambazo  hutakiwa  kupelekewa  maombi  haya  ya  zuio.  Mara nyingi  mamlaka  za ardhi  huwa zipo  katika  ofisi  za wilaya  au  manispaa katika mkoa wako isipokuwa  kwa walio  Dar  es salaam  maombi  hupelekwa   makao  makuu  pale  wizara  ya ardhi  kama  ni hati.

5.   MAOMBI  YA KUZUIA  HATI  ISIBADILISHWE  HUANDALIWAJE.

Maombi  haya  si  maombi  kama  maombi  mengine  yalivyo. Maombi  haya  ni maombi  ya  kisheria  na  huandaliwa   katika  ofisi  za wanasheria   na  hupelekwa  yakiwa  na  muhuri  wa mwanasheria. Karika  maombi  hayo  mwombaji  hueleza  jina  lake  kwa urefu, anuani  yake,  uhusiano  wake  na  yule ambaye  jina  lake  ndilo  liko kwenye  hati yaani anayemwekea zuio   huku  akieleza  sababu  za  msingi  kwanini   anataka  kuzuia  hati  isibadilishwe.

6.   LAZIMA  MAOMBI  YAAMBATANE  NA  NYARAKA  HIZI.

Kwanza,  picha  2  za mwombaji  huku kila picha  moja  ikibandikwa kwenye  nyaraka  moja.

Pili, risiti  za malipo ya ada ya usajili. Maombi  haya hulipiwa  kiasi  cha  fedha lakini si kikubwa sana kwahiyo  lazima uambatanishe  na risiti  za malipo.

Tatu, mwombaji aambatanishe vielelezo vinavyompa haki juu ya kiwanja husika kwa  mfano  cheti  cha  ndoa, mkataba  wa mkopo n.k.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

                                           TANGAZO   MUHIMU                                                
VIWANJA     NA     NYUMBA          ZINAUZWA.
·        
WANASHERIA   WETU   WATAKUANDALIA   MIKATABA  YOTE  BURE  NA    KUKUSIMAMIA  MPAKA   MANUNUZI    YAKAMILIKE   BURE.
·        
UHALALI   WA  NYARAKA   NA   UMILIKI   UMETHIBITISHWA  NA                        WANASHERIA  WETU.
·        
UTAPEWA  MTU  WA  KUKUSAIDIA  KUFANYA  TRANSFER   KWA  HARAKA         BURE.
·        
IKIWA   UTATOKEA   MGOGORO  NDANI   YA  MWAKA  TANGU  TAREHE  YA       MANUNUZI    UTAPEWA   WAKILI   WA   KUSIMAMIA  MGOGORO    BURE
                                                        0784482959.

 KUONA   BOFYA  HAPO  JUU    MWANZO  WA   BLOG.







0 comments:

Post a Comment