Monday, 8 June 2015

JIHADHARI, HAYA NI MAZINGIRA KISHERIA AMBAPO ALIYEKUUZIA ARDHI ANAWEZA KUDAI TENA UMILIKI NA AKAUPATA.


 Image result for NYUMBA

NA  BASHIR  YAKUB -

Kisheria yapo  mazingira  ambapo  mtu  aliyeuza  ardhi  anaweza  kuidai tena  ardhi  ileile  aliyouza kutoka kwa mnunuzi na  akaipata. Na  hapa  haijalishi  kama  mnunuzi  ameiendeleza  ardhi  kwa  kiasi  gani au  amebadilisha hati na kuingia  jina  lake  na  vitu  vingine  kama  hivyo.  Sheria  imetoa  haki  hii  kwa  muuzaji  hasa  iwapo  masharti  katika   mkataba  wa  mauziano  yamevunjwa. Kwa  kawaida  kila  mkataba  wa  mauziano  ya  ardhi  huwa  na  masharti  ambayo  hupaswa  kutekelezwa na  kila  upande. Masharti  haya  huwa  ni  ya  msingi  na  hupaswa  kutekelezwa  vilevile  kama  ilivyokubaliwa. Kuvunjwa/kukiukwa  kwake  hutoa  haki  kwa  muuzaji  kuchukua  tena  kilicho  chake yaani  kujirejeshea  umiliki  wa  ardhi. Na  hii  mara nyingi  husababishwa  na  kuingia  mikataba  kiholela  bila  kupata  ushauri  au  kusimamiwa  na  wanasheria ambao hupanga masharti  haya  kwa ufundi  usio na madhara. Hapa  chini tutaona  jambo  hilio hufanyikaje  kisheria.

1.MUUZAJI  KUJIMILIKISHA  TENA  ARDHI  BAADA  YA  KUUZA.

Sehemu  ndogo  ya  tatu,  kifungu  cha 73 – 76 cha  Sheria  ya Ardhi   ndivyo  vifungu  katika sheria  ya  ardhi  vinavyoeleza  kwa  urefu  namna  ya  kujimilikisha  tena  ardhi  baada  ya  kuiuza.  Kifungu  cha  73  kinaanza  kwa  kusema  kuwa.   mkataba  wa  mauziano  ya  ardhi  unapokuwa  umekamilika   na  mnunuzi  ameshakuwa  mmiliki  wa  ardhi  aliyonunua,  muuzaji  anaweza  kujitoa  katika  mkataba  huo   pale  ambapo  mnunuzi  atakiuka  au  kwenda  kinyume  na  masharti  au  makubaliano  katika  mkataba  huo. 

Maana  iliyo katika  kifungu hiki  ni  kuwa  tayari mkataba  umekamilika,  na mnunuzi  amemiliki  lile  eneo iwe  nyumba, shamba  au  kiwanja .
Na  amemiliki  kwa  kiwango  kuwa  mpaka hati/leseni  ya  makazi/ofa n.k   tayari  ina  jina  lake,  lakini  kuna  mambo  aliahidiana  na yule  aliyemuuzia  na  bado  hajayatekeleza  mpaka  sasa. Basi  huyu  aliyemuuzia  ana  haki ya  kudai  umiliki  au  kuchukua  tena  ile  ardhi. Anachukuaje  ile  ardhi  tutaona  hapa  chini.

2.  SABABU  ZA  KUJIREJESHEA  UMILIKI  BAADA  YA  KUUZA.

Sababu  kubwa za  kisheria  za  muuzaji  kujitoa  katika  mkataba  na  kujirejeshea  umiliki  ni  kutokufuatwa  kwa  masharti  au  makubaliano  yaliyo  katika  mkataba  wa  mauzo( sale  agreement).  Kwa  mfano  kutomaliziwa  kwa hela . Unakuta  mnunuzi  ameahidi  kuwa  atamalizia  kiwango  cha  hela  kilichobaki  ndani  ya  miezi  mitatu  tangu  siku  ya  kusainiwa  kwa  mkataba. Muda  huo  unafika  mpaka  unapita mnunuzi  hataki  kulipa  hela  na  tayari  anamiliki  eneo. Au  ni  ardhi  ya kijiji  na  ameahidi  kuiendeleza  ndani  ya muda  fulani  lakini  bado  hajafanya  hivyo na  muda  umepita sasa.  Haya  ndio  mazingira na kwa  ufupi  hii  huhusisha  kutotekelezwa  kwa yale  aliyoahidi  mnunuzi   katika  mkataba  wa mauzo si  lazima  yawe hayo  tu  niliyotaja.

3.  NAMNA  MBILI  ZA  MUUZAJI  KUCHUKUA  TENA  ARDHI  YAKE  ALIYOKWISHA UZA.

( a ) KUJIREJESHEA  MWENYEWE ARDHI  BILA  KUHUSISHA  CHOMBO  CHOCHOTE  CHA  KISHERIA.

Kwa  jina   la  kitaalam  hatua hii  huitwa  “resuming possession peaceably”. Ni  hatua  ambapo  muuzaji    huamua  kuchukua  ardhi  yake  aliyouza  kwa amani  bila ugomvi  wala kuhusisha  chombo  chochote cha  kisheria  ikiwamo  mahakama. Hatua  hii  mara  nyingi  huwezekana  pale  ambapo  mnunuzi  haishi  kwenye  eneo hilo au  halitumii  kwa  matumizi  yoyote.  Au  hata  kama  anaishi  au  analitumia amekubaliana  na  hatua  ya  muuzaji  kujirejeshea  eneo husika . Na  zaidi  huwezekana  iwapo   hati/nyaraka ya  eneo  bado  iko mikononi  mwa  muuzaji  pengine  kukisubiriwa  kutekekezwa  kwa  masharti kadhaa.  Ikiwa  katika  mazingira  kama hayo  muuzaji  kwa  amani  kabisa atajirejeshea eneo  lake na  biashara  itaishia  hapo.

( b ) KUJIREJESHEA  ARDHI  KWA  KUPITIA  MAHAKAMA.

Mahakama  hutumika  kuomba  kuchukua  tena ardhi  aliyouza muuzaji ikiwa  muuzaji  ameamua  kwa  hiari tu kuitumia  mahakama  au  iwapo  mnunuzi  amekataa  kurejesha  ardhi  kwa  amani  hata  baada  ya  kukiuka  masharti. Pia muuzaji  ataitumia  mahakama ikiwa  kwa  maoni  yake   anaona  kuwa  si  rahisi  kujirejeshea  eneo hilo bila  kupitia  mahakama  pengine  kwa  namna  mnunuzi  alivyokwishaliendeleza  eneo  hilo  au  ndimo  anamoishi  na  hivyo  si  rahisi  kukubali  kutoka  bila  kusababisha  uvunjifu  wa  amani. Basi  kwa  mazingira  haya  muuzaji  atapeleka  maombi  maalum  mahakamani  kuomba  kumiliki  tena  eneo  alilokwisha uza  kwa  sababu  mnunuzi  amevunja/kiuka  makubaliano   na  pia  atadai  fidia   kwasababu ya kukiukwa  makubaliano ambayo  ni  sawa na kuvunja  mkataba.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

                                           TANGAZO   MUHIMU                                                
VIWANJA     NA     NYUMBA          ZINAUZWA.
·        
WANASHERIA   WETU   WATAKUANDALIA   MIKATABA  YOTE  BURE  NA    KUKUSIMAMIA  MPAKA   MANUNUZI    YAKAMILIKE   BURE.
·        
UHALALI   WA  NYARAKA   NA   UMILIKI   UMETHIBITISHWA  NA                        WANASHERIA  WETU.
·        
UTAPEWA  MTU  WA  KUKUSAIDIA  KUFANYA  TRANSFER   KWA  HARAKA         BURE.
·        
IKIWA   UTATOKEA   MGOGORO  NDANI   YA  MWAKA  TANGU  TAREHE  YA       MANUNUZI    UTAPEWA   WAKILI   WA   KUSIMAMIA  MGOGORO    BURE
                                                        0784482959.

 KUONA   BOFYA  HAPO  JUU    MWANZO  WA   BLOG.




0 comments:

Post a Comment