Monday, 15 June 2015

MMILIKI WA ARDHI FAHAMU PUNGUZO JIPYA LA KODI,TOZO, ADA, ZA ARDHI .


Image result for LUKUVI BUNGENI
NA  BASHIR  YAKUB -

Juzi  mheshimiwa  William Lukuvi  alikuwa  akiwasilisha  hotuba  yake  ya makadirio ya  mapato  na  matumizi  ya  mwaka  fedha  2015/16 mbele  ya  Bunge. Alizungumzia  mambo  mengi  sana  ambayo  ni  muhimu  kwa  mdau  au  mmiliki  yeyote  wa  ardhi  kuyajua.  Kati  ya  mambo  muhimu  aliyozungumza  mambo  mawili  yaligusa  hisia  za  wengi. Kwanza  ni  punguzo  katika  kodi,ada  na  tozo  za  ardhi.  Pili  ni suluhu  kuhusu  suala  la  muda  mrefu la  uendelezaji  wa  mji mpya wa  kisasa  wa  Kigamboni.  Yumkini  suala  la  mji  wa  Kigamboni   ni  suala  lililokuwa  likisubiliwa  kwa  hamu  sana  hasa  kutokana  na  sintofahamu  na  danadana  kwa  muda  mrefu.  Makala  haya  yataeleza  baadhi  ya  mambo muhimu  kutoka  hotuba   ya  serikali  kuhusu  mambo  mbalimbali  ya  ardhi  awamu  kwa  awamu.
Leo  makala  yataeleza kuhusu  kodi,  tozo  na  ada  zilizopunguzwa  ili  watu wafahamu  hasa  kutokana  na  ukweli  kuwa  ni  wachache  sana ambao hufuatilia  hotuba  hizi.        Na  baadae  makala  yatakayofuata  siku  nyingine yataeleza  msimamo  wa  serikali  kuhusu  ardhi  ya  kigamboni.

ADA, KODI   NA TOZO  ZILIZOPUNGUZWA.

( A ) PUNGUZO  ADA  YA UPIMAJI ARDHI.

Kwa  kawaida  unapohitaji  hati   huwa ni  lazima  eneo  lako  liwe  limepimwa. Upimaji  ni  hatua  ya  awali  kabisa   unapohitaji  hati.  Hata  hivyo   hatua  hii  huwa  ni  lazima  kwa  wale  wenye  maeneo  ambayo  hayajapimwa  kabisa . Aidha ifahamike  kuwa suala  la  kupima  ardhi  si  lazima  tu  uwe unahitaji  hati  bali  waweza  kupima  eneo  lako  ikiwa  kama  hatua  ya  kurasimisha(officialize)  eneo  lako  ili  litambuliwe  katika  mamlaka  za  ardhi. Ada  ya  kupima  iliyokuwepo  ilikuwa  ni  Tshs 800,000/=( laki  nane tu ) kwa  hekta .  Imepungua  mpaka  kufikia  300,000/=(laki tatu) kwa  hekta . Ni  punguzo  la  asilimia  62.5.  Ni  punguzo  kubwa  lakini   kwa misingi  ya  umiliiki  ardhi  hata  hiyo   bado  ni  kubwa.Ikumbukwe  kuwa  ardhi  inayoongelewa  hapa haihusishi  mashamba. Ni  ardhi  ya  kawaida  ya  makazi au  viwanja.

( B )PUNGUZO  KODI  YA  UPIMAJI  WA MASHAMBA  YA  BIASHARA .

Kawaida  mashamba  ya  biashara  hulipa  kodi  tofauti  na  mashamba  ya  kawaida  katika  upimaji.  Kwahiyo  kodi  hii  hapa  ni  kwa  ajili  ya  kupima  mashamba  ya  biashara  tu. Awali  kodi  hiyo  ilikuwa  10,000/=( elfu kumi) kwa  ekari.  Na sasa   ni  Tshs 5,000/=( elfu  tano ) kwa  ekari. Ni  punguzo  la  asilimia 50.

( C ) PUNGUZO KODI  YA  UPIMAJI  MASHAMBA  YA  KAWAIDA.

Mashamba ya  kawaida  ni  mashamba  ambayo  si  ya  biashara. Ni  mashamba ambayo ndiyo  yanayomilikiwa  na  Watanzania kwa  asilimia  kubwa. Karibia wakulima  wote  tunaowasikia  huko  mikoani  humiliki  mashamba ya  namna  hii.  Awali  kodi  ya upimaji  kwa  ekari  ilikuwa  Tshs 1,000/= ( elfu  moja) na  sasa  ni Tshs 400/=(mia nne) kwa  ekari. Ni  punguzo  la  asilimia 60.

( D ) PUNGUZO  GHARAMA ZA  KUWEKA  VIZUIZI( CAVEAT).

“CAVEAT” ni  kizuizi ambacho  huwekwa  na yeyote  mwenye maslahi  fulani  katika  ardhi  ili  kuzuia hati  isibadilishwe  kutoka   kwa  mmiliki  mmoja kwenda  kwa  mwingine  pengine  kutokana na  mauzo  au  mkopo.  Kizuizi  hiki  hakiwekwi  mahakamani  isipokuwa huwekwa  mamlaka  za  ardhi.  Ada  ya  kuweka  kizuizi  awali  ilikuwa  Tshs 120,000/=(laki  moja  na  elfu  ishirini),  na  sasa  ni  Tshs 40,000/=(elfu  arobaini).  Ni  punguzo  la  asilimia 66.7.

( E ) PUNGUZO  NYARAKA  ZA  KUBADILISHA  MAJINA ( DEED POLL).

“DEED POLL” ni  waraka  maalum ambao  hutumika  endapo  mtu  anataka kubadilisha  jina. Kwa  mfano  mtu  anaitwa AUDAX lakini  amebadilisha  jina  na  sasa  anaitwa PETER  basi  nyaraka  ya  kisheria  inayotumika  huitwa  deed poll.  Waraka  huu serikali  iliuweka  mamlaka  za  ardhi  na   hushughulikiwa  na  mamlaka  hizo.  Ada  iliyokuwa inalipiwa  awali  ni  Tshs  80,000/=( elfu themanini tu)  na  sasa ni Tshs 30,000/=(elfu thelathini  tu). Ni  punguzo  la  asilimia 62.5.

( F ) PUNGUZO GHARAMA  ZA  KUPATA  NAKALA  ZA  HUKUMU  KATIKA  MABARAZA  YA  ARDHI(MAHAKAMA  ZA ARDHI).

Mabaraza  ya  ardhi  ndio  mahakama  za  ardhi . Yapo  ya  mabaraza ya  ardhi ya  kata    na  baadae  mabaraza  ya ardhi  ya  wilaya  ambayo  ndio  mahakama  za  ardhi  za   wilaya . Ili  kupata  nakala  ya hukumu  kesi  inapoisha  muhitaji  hutakiwa  kulipia.  Awali  malipo  ya  nakala  hizo  ilikuwa Tshs 16,000/= ( elfu  kumi  na  sita  tu),  na  sasa ni Tshs 6,000/= ( elfu  sita tu). Ni  punguzo  la  asilimia 62.5.

( G ) PUNGUZO  ADA  YA  MAOMBI  YA KUMILIKI  ARDHI.

Mara  nyingi  maombi  haya  hufanyika  iwapo  kuna ardhi  mahali   isiyokuwa na  mmiliki  au  ardhi  iliyo  katika  mamlaka  za  serikali na  sasa  serikali  inataka  kuwamilikisha  wananchi. Hapa  ndipo  hutakiwa  kufanyika  haya  maombi. Awali  ada  ya  maombi  kama  haya  ilikuwa  Tsh 80,000/= ( elfu themanini), na  sasa  ni  Tshs 20,000/=(elfu  ishirini  tu). Ni  punguzo  la  asilimia  75. Tutaendelea  kuwaletea  mapunguzo  mengine  katka makala  zijazo. Aidha  ni  vema  kuzingatia  kuwa  mapunguzo  haya  yataanza  kutumika  rasmi tarehe 1 / JULAI / 2015.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com

                                           TANGAZO   MUHIMU                                                
VIWANJA     NA     NYUMBA          ZINAUZWA.
·        
WANASHERIA   WETU   WATAKUANDALIA   MIKATABA  YOTE  BURE  NA    KUKUSIMAMIA  MPAKA   MANUNUZI    YAKAMILIKE   BURE.
·        
UHALALI   WA  NYARAKA   NA   UMILIKI   UMETHIBITISHWA  NA                        WANASHERIA  WETU.
·        
UTAPEWA  MTU  WA  KUKUSAIDIA  KUFANYA  TRANSFER   KWA  HARAKA         BURE.
·        
IKIWA   UTATOKEA   MGOGORO  NDANI   YA  MWAKA  TANGU  TAREHE  YA       MANUNUZI    UTAPEWA   WAKILI   WA   KUSIMAMIA  MGOGORO    BURE
                                                        0784482959.

 KUONA   BOFYA  HAPO  JUU    MWANZO  WA   BLOG.






1 comments:

  • Lightness Kweka says:
    21 March 2017 at 21:28

    Tafadhal naitwa lightness nataka kufahamu jinsi ya kumpata MTU wa kunipimia shamba language ekar 5 na gharama zake pls

Post a Comment