Monday, 2 March 2015

USIFANYE MAKOSA, HUU NDIO UTARATIBU WA KUNUNUA NYUMBA ILIYOWEKWA REHANI/DHAMANA BENKI .


Image result for NYUMBA
NA  BASHIR  YAKUB-

Nimewahi kuandika  mara  kwa  mara  kuhusu  utaratibu  mzuri  wa  kumwezesha  mtu kununua nyumba  huku  akiwa ameepuka  mgogoro. Nilitahadharisha  sana  kuhusu  migogoro  ya  ardhi  ambayo  sasa  imekuwa  janga  la  kitaifa  hapa  kwetu. Nakumbuka  moja  kati  ya  mambo  niliyoeleza   ni  kuwa utaratibu  wa  manunuzi  ya  nyumba/viwanja unatofautiana.Nikasema kwamba  tofauti  zake  zinatokana  na  ukweli  kuwa   kila  nyumba  ina mazingira  yake. Hata  hivyo sikusema  utofauti  wa  mazingira  hayo ila  sasa  naweza  kueleza  kwa ufupi  utofauti  wa  mazingira  ya  kila  nyumba  unapokuwa  katika  taratibu  za ununuzi.

1.UTOFAUTI  WA KITAALAM  KATIKA  UNUNUZI  NYUMBA.

Usikurupuke   unapohitaji  kununua ardhi.  Unapaswa  kujua  kuwa   nyumba  na  viwanja  zina  taratibu  tofauti unapohitaji  kununua. Ukikurupuka utalipia  gharama  ya kukurupuka  kwako. Kutokana  na  hilo ni muhimu tujue  kuwa kuna  nyumba  inayouzwa  kwa  utaratibu  wa kawaida  wa mmiliki  mwenyewe    kumuuzia  mnunuzi. Hii  mara  nyingi  huwa  haina  shida sana kwakuwa  unahitaji  tu  kujiridhisha  na baadhi  ya  mambo  ya  msingi   kama  kufanya  upekuzi  rasmi
 ( official  search) katika  mamlaka  za ardhi n.k. 

Pili kuna  nyumba  inayouzwa  na  wasimamizi  wa  mirathi. Hii  uuzwaji  wake  hauko  sawa  na   ile  inayouzwa  na  mmiliki halisi.  Hawa  ni wasimamizi  wa  mirathi  hivyo  hata  uuzaji  wao  si  uuzaji  kama  wa mmliki  halisi. Utofauti  wao  upo  katika  namna  ya  kuandika  mkataba( sale agreement) na  nyaraka  ambazo  wanapaswa  kukuonesha  wewe  mnunuzi .  Pia  kuna  ununuzi  wa  nyumba  ya  mkopo  ambao  sasa  ndio  mada  ya leo. Ununuzi wa  nyumba  ya  mkopo  nao  si  ununuzi  kama  wa nyumba  ya  kawaida. Haufanani  na  nyumba  ya  kawaida  na haufanani  na wa  nyumba  ya  mirathi. Unazo  tarati  bu zake  tofauti  kabisa  na ununuzi  mwingine.

2.UMUHIMU WA  KUZINGATIA  UTARATIBU  UNAPONUNUA  NYUMBA YA DHAMANA.

Tatizo kubwa  linakuja  kuwa  unaponunua  bila  kuzingatia  utaratibu  pia  uwe  tayari  kupoteza.  Ieleweke  kuwa nyumba  au  ardhi   yoyote ni kitu  ambacho  hudumu  milele. Hivyo  kama  utakosea  utaratibu  hata   kwa  kiwango  kidogo basi  ya kutosha  kuishi  bila  amani  maisha  yako  yote. Kama  si  wewe  watakuwa  watoto  wako  na  kama  si  watoto  wako  watakuwa  wajukuu  wako.  Kati  ya  hawa   kuna mmoja   mgogoro  utamkuta kwa  makosa  uliyoyafanya  wewe. Na ubaya  wa  mgogoro  unapotokea  mahakama  kikubwa  inachokifanya  ni  kuangalia  nani  alikosea  taratibu.  Inaangalia  hilo  kwasababu  yenyewe  inakuwa  haipo   wakati  mnauziana  na hivyo  nyote  haiwajui  na  haijui  kati  yenu  nani  mkweli  na  nani  muongo.

Kwahiyo kama ni wewe  mnunuzi  uliyekosea taratibu  wakati  wa kununua  basi   hakuna  kingine  ila  kupoteza  bila   kujali  gharama   ulizotumia  katika  manunuzi. Lakini  ikiwa  ulifuata  taratibu   kwa  umakini  kwanza  ni  vigumu kuingia  katika  mgogoro  lakini   hata  bahati  mbaya uingie katika mgogoro  basi  ushindi  utakuwa  ni  wa  kwako. Huu  ndio umuhimu  wa  kuhakikisha  unafuata  taratibu.  Zingatia  maeneo  mawili  kwanza  uandaaji  wa  mkataba  na  pili ukaguzi  na uhakiki  wa  nyaraka.

3.NAMNA  YA  KUNUNUA  NYUMBA AMBAYO  MUUZAJI  AMEIWEKA  REHANI/DHAMANA   BENKI.

Unapotaka  kununua  nyumba  ambayo muuzaji  amebahatika  kukwambia ukweli  kuwa  ana  mkopo  benki  na  hivyo  nyaraka  zote  pia  zipo  benki  na  hivyo  anataka  auze apate  hela  ili  akalipe  mkopo  zingatia  sana  mambo  haya.

( a ) Kwanza  usikubali  hata  kidogo  kauli  ya  kwamba  umpe  hela  halafu  yeye   muuzaji  ndio  akalipie  benki. Usifanye  mchezo  huo  kisheria  haukubaliki  utakuletea shida  kubwa  baadae.

( b ) Pili  kama  unaamua  kwenda  naye  benki  ili  akamalizie  deni  halafu  akuletee  nyaraka  usikubali  akuache  nje  au  mapokezi  halafu  yeye   ndio  aingie  ndani  eti  akamalizie  deni  halafu  ndio  arudi  na  nyaraka  akupe. Hilo  nalo  usilikubali.

4.FUATA  UTARATIBU  HUU NDIO  UNAOKUBALIKA.

( a ) Kwanza  hakikisha  unakwenda  naye  mpaka  benki   na  nyote  kwa  pamoja  mnaingia kumuona  afisa  mikopo  na  hakikisha  afisa   mikopo  anakudhibitishia  kuwa  muuzaji  kweli  anadaiwa  na  anadaiwa  kiwango  alichokwambia  na  anathibitisha  kuwa  ni  kweli  kabisa  utakapolipa   hiyo  hela  anayodaiwa  hati au  nyaraka  ya  nyumba  itatoka. Hakikisha  unapata  majibu  kama  hayo  kutoka kwa afisa  mikopo  wa taasisi  ya  fedha  husika  na si  kutoka kwa muuzaji.

( b ) Pili  baada  ya  kuridhika  na  kuamua   kununua, hatua  inayofuata  ni  kuandaa  mkataba  ambao  utakuwa  unaeleza  kitu kilekile  yaani  kuwa  muuzaji  ana  deni  na  wewe  unakwenda  kumlipia  deni   ili ununue  nyumba  yake.  

( c ) Baada  ya  kuandaa mkataba  hamtasaini  popote  katika  ule  mkataba  isipokuwa  mtaambatana  mpaka  benki  pamoja  na  mwanasheria  wenu huku   mkataba  ukiwa haujasainiwa  na  yeyote, muuzaji au  mnunuzi .

( d ) Muda wote  huo  hutakiwi   katika  hatua  yeyote  kuwa umempa yule  muuzaji    hela  yeyote. Usimtangulizie  chochote.Mtakapofika   sehemu  anapodaiwa  pia  hautampa  hela  isipokuwa  utatoa  kiwango  anachodaiwa  utalipa  kwa  yule  afisa  mikopo  kisha  atatakiwa  akukabidhi  ile  hati  au  nyaraka  nyingine yoyote  iliyopo  mkononi. Hakuna  hatua ambapo  hati  hiyo  itatakiwa  kuingia  mikononi  mwa   muuzaji.

(e ) Baada  ya  hapo  ndio  sasa  mnaweza  kusaini  mkataba  mbele  ya  mwanasheria kama  hatua  ya  kuuziana   na kama  kuna  akiba  ya hela  unaweza  kumkabidhi   muuzaji  na  utaondoka  na  nyaraka  yako  na  kila  mtu ataendelea  na  maisha  yake. Huu ndio  utaratibu  wa kununua  nyumba  au  viwanja  vilivyowekwa  rehani/dhamana.

Nasisitiza  tena    kuzingatia  taratibu  za kisheria  katika  manunuzi  ya  ardhi  ili  kuepuka  kupoteza. Kama  hujui  uliza tutakusaidia kuliko  kukurupuka  ukaingia  hasara.  

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO. PIA NI  KATI   YA  WANASHERIA  WAANZILISHI  WA  BLOG  HII    0784482959,  0714047241
bashiryakub@ymail.com
TANGAZO   MUHIMU

VIWANJA     NA     NYUMBA          ZINAUZWA.

-WANASHERIA   WETU   WATAKUANDALIA   MIKATABA  YOTE  BURE  NA                    KUKUSIMAMIA  MPAKA   MANUNUZI    YAKAMILIKE   BURE.

-UHALALI   WA  NYARAKA   NA   UMILIKI   UMETHIBITISHWA  NA   WANASHERIA     WETU.

-UTAPEWA  MTU  WA  KUKUSAIDIA  KUFANYA  TRANSFER   KWA  HARAKA                 BURE.

-IKIWA   UTATOKEA   MGOGORO  NDANI   YA  MWAKA  TANGU  TAREHE  YA              MANUNUZI    UTAPEWA   WAKILI   WA   KUSIMAMIA  MGOGORO    BURE
                                                        0783851726.

 KUONA   BOFYA  HAPO  JUU    MWANZO  WA   BLOG.


1 comments:

  • Noel Assenga says:
    4 March 2015 at 00:14

    nashkuru kaka kwa kutuletea blog hii ya mambo ya sheria. sasa sisi walala hoi nadhani tutakuwa na pa kuanzia. Swali langu tu naomba kuuliza. Hivi ukiwa na eneo,umelinunua kutoka serikali ya kijiji afu ukalipima na kupata haki. baadae wananchi wanavamia maeneo ya jirani na kuuziana viwanja vidogo vidogo. wakati wanaanza ujenzi wanagundua kuwa hakuna njia ya kupitisha lori la mchanga wala cement. sasa wanakuja na ideo ya kuacha hatua mbili za bara bara kila upande. kwa kuwa mim ni jirani upande mwingine, wananiambie niamishe beconi hatua mbili ndani ili tuache barabara. wanakuja na mwenekiti kuomba pia ku-push utakelezaji wa adhma hiyo. Je, ni sahihi mwenyekiti wa serikali ya mtaa kutoa mwongozo kama huo? Je, upimaji wa eneo unamaanisha nini,bado linakuwa chini ya mipango ya kijiji? asante sana

Post a Comment