Sunday 1 March 2015

MKE ASIYE WA NDOA NA MTOTO WA NJE YA NDOA HAWARITHI KISHERIA.

Image result for MTOTO WA NJE YA NDOA


NA  BASHIR  YAKUB-

Kumekuwepo  na utata  mkubwa  kuhusu  urithi  wa  mali  za  marehemu  hasa  inapotokea  kuwa  marehemu  alikuwa  na  mke   zaidi  ya mmoja  na  hapohapo  watoto  wanaotokana  na  mama  tofauti.  Tumeshashuhudia  magomvi  makubwa  misibani   lakini  pia  tumeshuhudia  na  tunaendelea kushuhudia  utitiri  wa mashauri  kuhusu  mkanganyiko  wa  mali za marehemu ambaye  familia  yake  ni  ya watoto  wanatokana  na  mama  tofauti. Kutokana  na  hayo  kuna umuhimu  mkubwa  wa kueleza sheria  inasemaje  kuhusu  mazingira  ya  namna  hiyo ili  anayemua kuchukua  hatua  au  kulalamika  alalamikie  kitu  ambacho  ni  haki  yake  kweli na  anayeamua  kuacha  aache  akiwa  ameridhika  kuwa  hajaonewa  isipokuwa  hicho  alichopata  ndiyo  haki   yake  kisheria.

1.NINI  MAANA YA MKE  WA  NJE  YA  NDOA.

Mke  wa  nje  ya  ndoa  ni  mke  ambaye  ameishi  na  mume  kama  mke  na  mume  lakini  akiwa  hajafunga  ndoa  yoyote  ya  kiislamu, ya  kanisani, ya  serikali au  ya kimila. Ndoa  ya kiislamu hufungwa  kwa taratibu  za kiislamu  ambazo huhusisha  masheikh, makadhi n.k. Ndoa  ya  kikiristo  hufungiwa  kanisani  na  yaweza  kufungishwa  na  mchungaji, askofu, padre n.k. Ndoa ya  serikali  hufungwa  katika  mamlaka  za serikali  kama  kwa mkuu wa wilaya  ubalozini n.k. Na  ndoa  za kimila  ni  ndoa  ambazo  hufungwa  kutokana  na mila  na  desturi  za jamii  fulani kwa mfano  ndoa  za kihaya, ndoa  za kichaga n.k. Kwa hiyo  kama  mwanamke  hana  ndoa  yoyote  katika  hizi  basi  yeye  ni  mke  wa  nje  ya ndoa.

2. NINI  MAANA YA  MTOTO  WA  NJE  YA NDOA.

Mtoto  wa  nje  ya  ndoa ni mtoto aliyetokana  na  ndoa  isiyohalali au  mahusiano  yasiyo  halali. Hapo juu  nimetaja  aina  za ndoa halali. Hii ina  maana  kuwa  iwapo  mtoto  amepatikana  nje  ya  ndoa  hizo  basi  huyo  ndiye  anayeitwa  mtoto   wa nje  ya  ndoa.

3.  MKE    ASIYE  NA  NDOA  HARITHI.

Kwa  mujibu  wa sheria  zetu  hapa  Tanzania  zikiwemo   tafsiri  mbalimbali  za  sheria  hizo  ambazo  hutolewa  na  mahakama  kuu pamoja  na  mahakama  ya  rufaa  mke wa  wa  nje  ya  ndoa  hutambulika  kama  kimada. Neno  kimada  sio  tusi  isipokuwa  ni  neno  la  kitaalam  linalomwakilisha  mwanamke  anayeishi  na  mwanaume  bila  ndoa  na  ndio  maana  neno  hilihili  limetumiwa  na  mahakama  katika  hukumu  zake  mbalimbali.

Kutokana  na  hilo  ieleweke  wazi  kuwa  mwanamke  asiye  wa  ndoa   hata  kama  anaishi  na  mwanaume  kwa  mtindo  ambao ukiungalia  utadhani  ni  mke  na  mume  bado  ikitokea  mwanaume  huyo  kufa  mwanamke  wa  namna  hiyo  hawezi  kudai  chochote  katika  mali  za  yule  mwanaume. Mke  halali  ni  mke ambaye  mahusiano  yake  na  mwanaume  yametokana  na  ndoa  halali. Nje  ya  ndoa  halali  hakuna  urithi. 

Hii  isimfanye  mtu  yeyote  ajisikie  vibaya  isipokuwa  kinachotakiwa  ni  kuhalalisha  mahusiano  ili  ndoa  halali  ipatikane.
Aidha  ieleweke  kuwa  wakati  ambao  sio  wa kifo  kwa  mfano  wakati  wa kuachana  baina  ya  mke  na mume  ambao  wameishi  kama  wanandoa  lakini  wakiwa hawana  ndoa  mwanamke  asiye  wa  ndoa  ana  haki  ya  kupata mgao  wa mali. Na  hii  ni ikiwa  wameishi  wote  kwa zaidi  ya  miaka  miwili  kama  mke  na mume  na  ikiwa  kuna  mali  waliyochuma  kwa pamoja . Kwa  maana  hiyo  kwa  mazingira  ya  kuachana  ya  kawaida mwanamke  asiye  na  ndoa  anaweza  kudai  mali  lakini  baada  ya  kifo  hawezi kudai  mali.

4. MTOTO  WA  NJE  YA  NDOA  HARITHI.

Hapo  juu  nimetaja  aina  za  ndoa  ambazo  hutambuliwa  na  sheria  zetu hapa  nchini. Nikasema  kwamba  watoto  waliotoka  nje  ya  ndoa  hizo  ndio  watoto  wa nje  ya  ndoa. Ni  watoto  haohao  ambao  hawaruhusiwi  kurithi.  Katika  kutafsiri  sheria hii  mahakama  nyingine  zimekwenda  mbali  kwa  kusema  kuwa  mtoto  wa  nje  ya  ndoa  haingii  katika  tafsiri  ya  neno  mtoto   lililo  katika  sheria  ya  ndoa.

5. KUMHALALISHA  MTOTO  WA  NJE  YA  NDOA.

Sheria  inasema  kwamba  mtoto  aliyezaliwa  nje  ya  ndoa anaweza  kuhalalishwa  kwa  kufuata  taratibu  za  mila  na desturi za  jamii  husika  na  hatimaye  kuwa  mtoto  halali  ambaye  anaweza  hata  kurithi. Kwa  mfano  hapa  kwetu  kila  kabila  wanazo  taratibu zao  katika  kulitekeleza  hili.  Kwa  kutumia  taratibu  hizo mtu anaweza  kumhalalisha  mtoto  wa  nje  ya  ndoa  na  hatimaye  akawa  na  hadhi  ya  kurithi .

6. MTOTO  WA  NJE  YA  NDOA  KURITHI  IWAPO KUNA  WOSIA.

Maelezo  niliyotoa  hapo  juu  kuhusu  mtoto  wa  nje  ya  ndoa  kutokurithi  yanahusu  pale  tu  marehemu  anapokuwa  hajaacha  wosia. Kawaida marehemu anapokuwa  hajaacha  wosia  familia  ya  marehemu au ndugu  ndio  hushughulika  na  kugawana  mali za marehemu  na  ndipo  hapo  mtoto  wa  nje  ya  ndoa  hatakuwa  na  nafasi  ya  kurithi. Lakini  iwapo  kuna  wosia  na marehemu  amemtaja  mtoto  wa  nje  ya  ndoa  kama  mrithi  basi  atapewa  hiyo mali  aliyoamrishwa aipate katika wosia . Hii  ndio  sababu  kubwa  ya  kuhimiza  watu  kuandika  wosia  ili  kuondoa  utata  wa  vitu  kama  hivi.

7.USHAURI  WA NAMNA  YA KUMSAIDIA  MTOTO WAKO  KAMA NI   WA  NJE  YA  NDOA .

Kama  unataka  mtoto  wako  uliyempata  nje  ya ndoa  asipate  taabu  baada  ya  kufa  kwako  basi andika  wosia  naye  umpe  chake. Nje  ya wosia  mtoto  wako  hatopata  kitu  na  wewe  waweza  kuwa  sababu  ya  kumfanya  mwanao  kuwa mtoto wa mitaani( chokoraa)  kwa  kukosa  msingi  wa  kipato. Nimesema  hapo  juu  kuwa sheria  haina  shida  kama  mtoto  wa nje  ya  ndoa  amepewa  mgao  katika  wosia.  Lakini nje  ya  wosia  sheria  inamzuia  kupata  mali.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO. PIA  NI  KATI  YA  WANASHERIA  WAANZILISHI  WA  BLOG  HII    0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com


TANGAZO   MUHIMU

VIWANJA     NA     NYUMBA          ZINAUZWA.

-WANASHERIA   WETU   WATAKUANDALIA   MIKATABA  YOTE  BURE  NA                    KUKUSIMAMIA  MPAKA   MANUNUZI    YAKAMILIKE   BURE.

-UHALALI   WA  NYARAKA   NA   UMILIKI   UMETHIBITISHWA  NA   WANASHERIA     WETU.

-UTAPEWA  MTU  WA  KUKUSAIDIA  KUFANYA  TRANSFER   KWA  HARAKA                 BURE.

-IKIWA   UTATOKEA   MGOGORO  NDANI   YA  MWAKA  TANGU  TAREHE  YA              MANUNUZI    UTAPEWA   WAKILI   WA   KUSIMAMIA  MGOGORO    BURE
                                                        0783851726.

 KUONA   BOFYA  HAPO  JUU    MWANZO  WA   BLOG.





0 comments:

Post a Comment