Thursday 26 February 2015

JE WAJUA NENO LIMITED (LTD) HUMAANISHA NINI KATIKA KAMPUNI .







Image result for BODI YA KAMPUNI

NA  BASHIR   YAKUB-

1. UTANGULIZI
Ni kawaida unapopita mitaani au  sehemu mbalimbali mijini au vijijini  hasa kwa wingi kabisa katika miaka ya hivi karibuni  kuona maneno kama …………COMPANY  LTD. Sijui kama uliwahi kujiuliza  maana ya neno hili limited (LTD). Pasi kuwaongelea  raia wa kawaida wa wamitaani ambao husoma neno hili katika mbao za matangazo na kwenye mabango mbalimbali ya kibiashara ambayo hubandikwa mitaani au nje ya ofisi mbalimbali, wapo watu ambao  wana makampuni na wanalitumia pia neno hili lakini  ikawezekana wakawa  hawajui hata maana yake.

Ni wakati sasa wa kufahamu  maana na matumizi ya neno hili. Awali ya yote ni vyema kufahamu kuwa neno hili lina maana kisheria na limewekwa kwa mujibu wa sheria na matumizi yake ni ya kisheria. Unapolikuta pahala ujue halijakaa bahati mbaya au halijawekwa kwa ajili ya urembo au kupamba matamshi.


2. NINI  MAANA  YA  NENO  LIMITED ( LTD )

Kwa tafsiri ya moja kwa moja ya kiswahili  twaweza kusema  Limited ni kikomo, ukomo, au mipaka. Zote ni maana za neno hilo na hutumika kwa utofauti kutokana na kinachoelezwa. Katika makala haya tutatumia neno ukomo ili kumaanisha Limited.
Katika sheria hasa sheria ya  Makampuni  ambayo hasa ndio inaangaziwa leo  neno limited linapotumika  humaanisha ukomo wa hatia au ukomo wa uwajibikaji wa wanachama  katika kampuni( Limited Liability ). Ni kwa namna gani kuna ukomo wa uwajibikaji kwa wanachama katika kampuni na katika lipi wanawajibika  tutaona baadae.

3. AINA  ZA  LIMITED (  LTD  ) .

Ni vyema kufahamu kuwa Limited nazo zina aina. Si kila limited unayoiona inafanana na nyingine. Mara nyingi hutegemea  kampuni imeundwa kwa limited ipi.  Zipo aina mbili za limited.
Kwanza  kuna  limited ya Hisa,  hii hujulikana kwa jina la kitaalamu kama ( Company Limited by shares ). 

 Pili  kuna limited ya makubaliano  ambayo kwa kitaalamu huitwa ( Company limited by guarantee). Pamoja na aina hizo kutofautiana lakini bado  zote katika matumizi huwakilishwa na neno moja tu yaani ( LTD ). Hii ni kumaanisha kuwa utofauti wake hauondoi msingi wa Limited . Katika kuandika matangazo au mabango zote tutaandika, Mfano ……CO.  LTD  au ……… & CO. LTD na si vinginevyo. Tofauti hujionesha katika  katiba .Uchambuzi kuhusu  aina hizi za Limited nitaonesha  kipengele kinachofuata.

4. NENO  LIMITED  HUMAANISHA NINI  LITUMIKAPO  KATIKA KAMPUNI.

Utaratibu wa Limited upo kulinda  maslahi ya baadae ya kampuni  hasa kipindi kampuni  inapokuwa inakufa au inafilisika. Kwa kawaida kampuni  inapokuwa inakufa au kufilisika hujikuta ikiwa `na madeni mengi kutoka kwa wadai mbalimbali. Kufa kwa kampuni hakumaanishi kufa kwa deni la wadai, hapana. Wadeni wanatakiwa kupata haki zao .Katika kuhakikisha wadeni wanapata haki zao ndipo  huu mpango wa limited ukaanzishwa.Hapo juu tumeona aina  za limited  kuwa kuna  limited ya hisa  (limited by shares) na tukaona kuwa kuna limited ya makubaliano (limited by guarantee). Sasa kwa undani kiasi tuangalie mojamoja.

( a ) Limited ya hisa ( Company  limited by shares ). Maana yake ni ukomo uliofungamana na hisa. Katika kampuni  kila mwanachama(member)  anakuwa na hisa zake.Hisa hizo huwa unaomba na unapewa. Kila hisa anayopewa mwanchama huwa inalipiwa na ina thamani yake. Kwahiyo  mwanachama anaweza kuwa na hisa ambazo anazimiliki akiwa tayari amezilipia au hajazilipia au amezilipia nusu. Katika hali hii kama inatokea kuwa kampuni inakufa  aidha kwa kufilisika au sababu nyingine yoyote , zile hisa  za wanachama ambazo walikuwa wanazimiliki lakini hawajazilipia  ndizo zitakazokamatwa na kuingizwa katika kampuni ili zitumike kulipia madeni. Aidha zile hisa ambazo  mwanachama alikuwa amezilipia haziwezi kutumika kulipa madeni ya kampuni na kanmwe haziwezi kukamatwa.

Na kama kuna mwanachama ambaye alikuwa amelipia hisa zake zote kwa ukamilifu basi hakuna  hisa zake zitakazokamatwa atabaki salama  na hawezi hata kidogo  kulazimishwa kutoa mali yake nyingine yoyote ili kuchangia deni la kampuni. Hapa ndipo tunapopata maana ya kwanza  ya neno limited ikiwa na maana ya  ukomo wa uwajibijikaji. Katika kuweka sawa zaidi  hapa tunaona kuwa ukomo au ulimited wa kuwajibishwa kwa mwanachama umehusisha kukamatwa kwa hisa zake ambazo hajalipia.Kwa maana kama kampuni isingekuwa na ukomo kwa maana isingekuwa LIMITED ingewezekana kukatwa hisa zote ambazo zimelipiwa na ambazo hazijalipiwa na hata ikiwezekana mali zake nyingine binafsi, lakini kwa sababu kuna ukomo ( ulimited) basi  kikomo kinalazimisha kukamata zile hisa ambazo hazijalipiwa tu na si vinginevyo.

 Msisitizo ni kuwa uwajibijikaji  wa mwanachama katika kulipa deni la  upo kwenye hisa na  maalum kabisa hisa ambazo hazijalipiwa. Mwanachama hawezi kuitwa kuchangia chochote isipokuwa zitatumika hisa zake ambazo alikuwa hajalipia na kama amelipia zote  hachangii kingine chochote.Na hii ni hata kama deni la kampuni ni kubwa kuliko hata mali zote ilizobaki nazo  aliyelipia hisa zake zote kwa ukamilifu  hachangii kingine chochote. Ndio maana huitwa uwajibikaji wenye ukomo ( Limited Liability).

( b ) Limited ya makubaliano ( Limited by Guarantee ). Kwa  ufupi hii humaanisha kuwa  kampuni itaendesha shughuli zake kama kawaida ila itakapotokea kuwa  kampuni  imekufa kwa sababu ya kufilisika  au sababu nyingine, wanachama (members )  watatoa michango yao  kila mmoja ili kuiwezesha kampuni kukidhi  mahitaji yake ikiwemo madeni. Uwajibikaji wa wanachama katika kampuni za namna hii upo  katika kuchangia. Pesa wanayochangia huitwa “guarantee fund”. Katika limited hii wanachama  hawachangii chochote mpaka  kampuni  isemwe kuwa imefilisika kabisa. Ikiwa kampuni inaelekea kufilisika lakini haijafilisika wanachama hawawezi kuchangia. 

Limited hii huwa haipendwi sana na  ni mara chache kukuta kampuni  imesajiliwa namna hii. Kampuni za aina hii ni chache. Na hazipendwi. Kampuni za namna hii mara nyingi hazina mtaji wa hisa ( share capital) na hivyo wakati wa kufilisika inapotakiwa kulipa deni panakuwa hamna cha kukamata  na hivyo  wanachama kutakiwa kuchangia.

5. JE  YAWEZEKANA  KUWAPO KAMPUNI   BILA  LIMITED ( LTD )

Tumeona hapo juu maana hasa limited  na mazingira yake  na tukasema kuwa hiyo ni kwa mujibu wa sheria. Pia tunaona makampuni mengi ni limited na kila anayeanzisha kampuni  lazima aandike……LTD. Swali ni je lazima kampuni iwe limited.

Jibu ni hapana,  si lazima kila kampuni iwe limited. Yawezekana ikaundwa kampuni bila kuwa limited.  Kampuni za aina hii huitwa UNLIMITED COMPANY. Hivyo basi kama limited company maana yake ni kampuni zenye ukomo basi  unlimited company ni kampuni isio  na ukomo. Tumeona kuwa neno limited linatumika kueleza uwajibikaji wa wanachama pindi kampuni inapokuwa katika msukosuko wa kufa. 

Hivyo basi ukomo wa uwajibijkaji katika kampuni za namna hii hauna mipaka(unlimited). Hii ina maana kuwa hata mali binafsi za wanachama zinaweza kutumika kulipa deni  la kampuni. Wakati katika limited hilo haliwezekana  na hiyo ndiyo mipaka yake. Hii haina mipaka wanachama  wanalazimika  kulipia kampuni deni.
Kampuni za aina hii  nazo hazipendwi sana.

Nimalizie kwa kusema kuwa neno LIMITED  unapoliona limeandikwa huwa limaanisha nilichoeleza hapa juu . Halitumiki kunogesha matamshi au kuelezea ufahari.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.  PIA  NI  KATI  YA  WANASHERIA  WAANZILISHI  WA  BLOG  HII    0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com
TANGAZO   MUHIMU

VIWANJA     NA     NYUMBA          ZINAUZWA.

-WANASHERIA   WETU   WATAKUANDALIA   MIKATABA  YOTE  BURE  NA                    KUKUSIMAMIA  MPAKA   MANUNUZI    YAKAMILIKE   BURE.

-UHALALI   WA  NYARAKA   NA   UMILIKI   UMETHIBITISHWA  NA   WANASHERIA     WETU.

-UTAPEWA  MTU  WA  KUKUSAIDIA  KUFANYA  TRANSFER   KWA  HARAKA                 BURE.

-IKIWA   UTATOKEA   MGOGORO  NDANI   YA  MWAKA  TANGU  TAREHE  YA              MANUNUZI    UTAPEWA   WAKILI   WA   KUSIMAMIA  MGOGORO    BURE
                                                        0783851726.

 KUONA   BOFYA  HAPO  JUU    MWANZO  WA   BLOG.







0 comments:

Post a Comment