Wednesday 4 March 2015

KUTOTOA MATUNZO YA MTOTO NI KOSA LA JINAI, HII NI NAMNA YA KUCHUKUA HATUA.

Image result for WATOTO WAPWEKE


                   
NA  BASHIR  YAKUB.

Kumekuwa  na  shida  sana  hasa  kwa  upande  wa  wanaume  kuwatelekeza  watoto. Mara  nyingi  wanaume  ndio   hutelekeza  watoto  kuliko  wanawake. Zipo  baadhi  ya  kesi  zimeripotiwa  zikihusisha  wanawake  kuwatelekeza  watoto   lakini hizi  si  nyingi  kama  ilivyo  kwa  wanaume. Hii  ni kwasababu  uwezekano  wa  mwanaume  kumkimbia  mtoto  ni  mwepesi  kuliko mwanamke  kumkimbia  mtoto/watoto.  Jambo  hili  ni  baya  na  limeshakemewa  na  sheria  mbalimbali.  Nataka   niwaeleza  kuwa  kumtelekeza mtoto   ni  kosa  la  jinai. Nikisema ni  kosa  la  jinai   maana  yake  ni kuwa  kulifanya  kwake  kunahitaji   adhabu  ya  kifungo  jela au adhabu  nyinginezo. Wapo watu  hasa  wanawake  ambao  wamekuwa  wakitupiwa  watoto  na  wanaume  kwa makusudi.  Ni  ushauri  wangu  kwamba  muda  ni huu  sasa kama  ulikuwa  hujui  kuanzia  leo  ujue  na  uchukue  hatua.

1.NINI  MAANA  YA  KUTELEKEZA  WATOTO/MTOTO  KISHERIA.

Kutelekeza mtoto/watoto   ni  pamoja  na  kutotoa  matumizi  kama  chakula, mavazi , matibabu, makazi,  na  mahitaji  ya  msingi( necessity) kama  ada  za shule, vifaa  vya  shule  na  kila  kitu  ambacho  ni mahitaji  ya  msingi  kwa  makuzi  na ustawi  wa  mtoto.  Kwa hiyo  mzazi  asiyejihusisha  kwa  namna  yoyote  na  huduma  hizi  nilizotaja kwa  mujibu  wa sheria  huyu  ndiye  aliyetelekeza  mtoto/watoto.

2.KUTELEKEZA  WATOTO/MTOTO  NI  KOSA  LA  JINAI.

Sura  ya  16  Sheria  ya Kanuni  ya  Adhabu  kifungu cha  166  kinasema  kuwa  Mtu yeyote ambaye, ni  mzazi  au  mlezi  au mtu  mwingine  mwenye  uangalizi    halali  wa mtoto  yeyote  mwenye  umri  usiozidi  miaka   kumi na nne, hali  ana  uwezo, wakumuhudumia  mtoto, kwa  kuamua  au kinyume  cha sheria, au  bila ya sababu za msingi akakataa  kumhudumia, na akamtelekeza  mtoto  bila  msaada, atakuwa  ametenda kosa. Kwahiyo  kumbe  kutokana  na  sheria  hiyo  kumtelekeza  mtoto   ni  kosa  la  jinai  kama  zilivyo  jinai  nyingine  kama  kuiba, kuua , kubaka n.k.
Aidha  ni muhimu  walioarhirika  na  matendo  ya  kutupiwa  watoto  wachukue  hatua  za  kufungua  kesi  za  jinai  ili  wahusika  wawajibishwe. 

3.NAMNA  YA  KUMFUNGULIA  KESI  YA  JINAI  ALIYEMTELEKEZA  MTOTO.

Mara  nyingi  kesi  za jinai  hufunguliwa  katika  vituo  ya  polisi. Utaenda  kituo  chochote  kilicho  karibu  nawe  utaeleza  kuwa  umekuja  kumfungulia  kesi  ya  jinai  fulani  fulani  kwa  kosa  la  kumtelekeza  mtoto  kinyume  na  sheria  ya Kanuni  ya Adhabu  kifungu  cha  166.  Ukisema  hivi  ni  rahisi  sana  kueleweka  na  kusaidiwa  kufungua  kesi  hiyo.  Kesi  ya  jinai  haina  gharama  yeyote  kwako  kwakuwa   itaendeshwa  na  na waendesha  mashtaka  wa  serikali. Nasema  hivyo  ili  mtu asihisi  uzito  kuchukua  hatua  kwa  kuhofia  gharama. Hakuna  gharama  yoyote  nenda  ukachukue  hatua  uokoe  watoto/mtoto. 

Pili  waweza  kufungua kesi  hii  moja  kwa  moja  mahakamani  bila  kupitia  polisi. Waweza  kwenda  mahakama  ya  mwanzo  iliyo ndani   ya  kata  yako  au  ndani  ya  wilaya  yako. Unapofika  hapo  utaeleza  kuwa  unataka  kumfungulia  kesi  ya  jinai fulani  fulani  kwa  kosa  la  kutelekeza  watoto/mtoto. Utasaidiwa  kufungua  kesi  na  ikiwezekana  waweza  kupewa  wito  siku hiyohiyo  ili  muda  uliopangwa  ukifika uliyemshtaki  afike  mahakamani kujibu.  Mahakama  ya  mwanzo  nako  shauri  hufunguliwa  bure  hivyo  usihisi  uzito  kwenda  kuchukua  hatua   kwa  kuhofia  gharama. Hakuna  gharama  yoyote  katika  hili.


4. PIA  WAWEZA  KUMDAI  FIDIA   ALIYETELEKEZA WATOTO/MTOTO.

Maelezo  ya  juu  nimeeleza  kumfungulia  kesi  ya  Jinai  mtelekeza  watoto. Ni  vyema  sasa  kujua  kuwa  sheria  imekuruhusu  pia kufungua  hata  kesi  ya  madai  ya kudai  fidia dhidi  ya  aliyetelekeza  watoto. Tofauti  ya  kesi  ya  jinai  na  madai  katika  hili  ni  kuwa  katika  kesi  ya  jinai  hukumu  ikitoka  ataadhibiwa  kwa  kifungo  au  vinginevyo.  Lakini  kesi  ya  madai  hukumu  ikitoka  ataamrishwa  kulipa  fidia  ikiwemo  gharama  zako zote  ulizotumia  mpaka  kesi  inaisha  kama  nauli n.k.  Atafidia  usumbufu  aliokusababishia    na atatakiwa  kukurudishia  gharama ambazo  uliwahi  kutumia  huko  nyuma  katika  kumtunza  mtoto/watoto  jukumu  ambalo  ni  lake. Hivyo  ni chaguo  lako  umfungulie  kesi  ipi  kati  ya madai  au  jinai.  

5.USHAURI   KWA   WALIOTUPIWA   WATOTO/MTOTO.

Wanawake  ndio  waathirika  zaidi  wa hili  na  ndio  ninaowaongelea  hapa. Nashauri  badala  ya kulalamika  huku  watoto  wakizidi  kukosa  mwelekeo  au  mkizidi  kuishi  maisha  ya  taabu  hebu  chukua  hatua  sasa. Kwa  uzoefu  wangu  hakuna  mwanaume  anayehimili  kufikishwa  mahakamani  kwa  kesi  ya  jinai  halafu  akaendelea  kuwa mgumu. Hakuna  mgumu  katika  kesi  ya jinai. Hawezi  kuwa   mgumu  wakati  akichungulia  kwenda  jela. Kama  huamini  jaribu  kufanya  hivyo  halafu  utaona  dawa hii  ilivyo  mwarobaini. Sishauri  haya  kwa  ubaya  isipokuwa  ni  katika  hali  ya  kuokoa  mtoto.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.     0784482959,  0714047241
bashiryakub@ymail.com
                                                                       TANGAZO   MUHIMU

VIWANJA     NA     NYUMBA          ZINAUZWA.

-WANASHERIA   WETU   WATAKUANDALIA   MIKATABA  YOTE  BURE  NA                    KUKUSIMAMIA  MPAKA   MANUNUZI    YAKAMILIKE   BURE.

-UHALALI   WA  NYARAKA   NA   UMILIKI   UMETHIBITISHWA  NA   WANASHERIA     WETU.

-UTAPEWA  MTU  WA  KUKUSAIDIA  KUFANYA  TRANSFER   KWA  HARAKA                 BURE.

-IKIWA   UTATOKEA   MGOGORO  NDANI   YA  MWAKA  TANGU  TAREHE  YA              MANUNUZI    UTAPEWA   WAKILI   WA   KUSIMAMIA  MGOGORO    BURE
                                                        0784482959.

 KUONA   BOFYA  HAPO  JUU    MWANZO  WA   BLOG.
  
                                                                       


3 comments:

  • Unknown says:
    29 October 2019 at 08:05

    Asante sana...mana mi ni mhanga...na ndugu zangu wanasema wanisaidie kufungua kesi mahakamani.

  • Unknown says:
    26 July 2020 at 12:40

    Asante sana Mungu akubariki nilikuwa sijui wapi kwa kuanzia

  • Unknown says:
    3 November 2020 at 07:33

    Ahsanteni Sanaa kwa kutuelimisha mungu awabariki

Post a Comment