Tuesday 10 March 2015

JE UMEACHISHWA KAZI AU WE NI MFANYAKAZI, ZIJUE HAKI ZAKO ZA MSINGI - 2.




Image result for WAFANYAKAZI WAANDAMANA
          
NA  BASHIR  YAKUB-

Jumatatu  ya  wiki  hii nilianza  na  makala  iitwayo   je  umeachishwa  kazi  au we  ni  mfanyakazi,  zijue  haki  zako. Nilizungumzia  masuala  kadhaa  yahusuyo  haki  za  mfanyakazi. Naligusia  kuhusu  aina  za  mkataba wa ajira, muda wa mkataba  wa ajira,  sehemu  ya  kufanyia  kazi, kipindi  cha  mpito katika  kazi (probation period) na mengine  mengi kuhusu  ajira. Nilisema  na  leo  tena  nasisitiza  kuwa  ili  upate  ujira  unaostahili   ikiwa  ni  pamoja  na  mafao kwa  kiwango  kinachotakiwa baada  ya kumalizika  kwa  ajira  yako  huna  budi kuwa  unajua  haki  zako.  Usisubiri  mwajiri  akwambie  nini  unastahili  isipokuwa  wewe  ndio  umwambie  mwajiri  nini  unastahili.  Mwajiri  hawezi  kukufundisha  haki  zako  kwakuwa  utazitumia kumnyima  amani. Nilisema  pia  kuwa  yawezekana unachopata  na  ukaona  kingi  sicho  unachostahili  kupata  usipokuwa tu  hujui. Kwahiyo  niseme  tu  kwamba  ni  muhinmu  mfanyakazi  kujishugulisha  kujua  haki zako  japo  chache. Leo  tunaangalia  tena  baadhi  ya  haki  nyingine  lakini  kabla  ya  hapo  ni  ushauri.

USHAURI  KWA  WAFANYAKAZI.

Haki  za  mfanyakazi  ninazoeleza  hapa  yawezekana  wakati  ukiwa  kazini  unaogopa  kuzidai  kutokana  na  woga  wa  kuonekana  umekuwa mjuaji  na  hivyo kukaribisha uwezekano wa  kupoteza  ajira. Pia  waweza kuwa uliacha  kuzidai  kwakuwa  huzijui. Kama  moja kati  ya  haya   limekutokea  basi  ushauri wangu  ni  kuwa haki  hizi zote  waweza  kuzidai  baada  ya  kuwa  umeachishwa  kazi  au wakati  wa  kustaafu  kwani  sheria  inaruhusu. Kama  hukupewa overtime,ulifanyishwa  kazi  muda  wa sikukuu, hukupewa  likizo kama  inavyostahili  na  yote  nitakayoeleza  hapa  chini basi  baada  ya  kazi  kuisha  waweza  kudai  fidia  yake.

1.  HAKI  YA  KUJUA  MASAA  YA  KAZI.

Mfanyakazi  hafanyi  kazi  muda  wote. Akifanya kazi  muda  wote  basi  uwe  ni uamuzi binafsi  lakini  lisiwe  ni agizo  la  mwajiri. Kazi  ina  muda  wake  na  hii  ni  kwasababu ili  mwanadamu  aishi  pia anahitaji kuhusika  katika  mambo  mengine  ya  kimaisha  nje  ya  kazi. Kutokana  na  hilo  ni  lazima  mkataba  wa ajira  uoneshe masaa  anayotakiwa  mtu  kufanya  kazi.  Kama  ni  masaa  12, masaa  8, masaa 9 yajulikane. Na  ni hayo hayo  tu  mfanyakazi  anayotakiwa  kufanyia  kazi.  Faida  ya  kuainisha  masaa  ya  kazi  ni kuwa  humsaidia  mfanyakazi  kupata  malipo  ya  ziada  iwapo   masaaa  yaliyoainishwa  yamepita. Hii wengi  wanaijua  huitwa  overtime. Overtime  ni  haki  ya  msingi  ya  mfanyakazi 

2.  KUFANYA  KAZI  SIKU  ZA  MAPUMZIKO.

Wapo  wafanyakazi  wanafanyishwa  kazi siku  za mapumziko  bila  malipo yoyote  ya  ziada. Kisheria  siku  za  mapumziko  sio  siku  za  kazi.  Ikiwa  ulifanya  kazi  siku  za  mapumziko  basi  ulistahili  malipo  ya  ziada   nje  ya  mshahara.  Siku za  mapumziko  si  jumamosi  au  jumapili  tu    isipokuwa  siku  za  mapumziko  hujumuisha  sikukuu  zote  za  kitaifa  kama  nyerere  day, karume  day, Iddi, Pasaka, mei  mosi  na  nyingine  zote. Malipo  ya  mfanyakazi  anayefanya  kazi  ndani  ya  siku  hizi  nayo  kisheria  yanahesabika  kama  malipo ya  ziada (overtime).  

3.  LIKIZO  YA  MFANYAKAZI  YA  MWISHO  WA  MWAKA.

Hii  hujulikana  kama  annual  leave.  Hii  huhesabiwa  kwa  mzunguko maalum  uitwao  mzunguko  likizo( leave  cycle). Mzunguko    huu  hutakiwa  kumfikia  kila  mfanyakazi  kwa  kiwango  cha  chini  mara  moja  kwa  mwaka. Mzunguko  huu  huhusisha  siku  28  za  kalenda   ikiwa  na  maana  ya  jumamosi  na  jumapili pia.  Kwakuwa  sheria  inasema siku  28  za  kalenda na  jumamosi  na  jumapili  nazo  ni  siku  katika  kalenda ndio maana  huhesabiwa.  Mzunguko  hutakiwa  kuhesabiwa  tangu  siku  ya  kuanza  kazi  mpaka  miezi  12.  Hii  ina  maana  ndani  ya  muda  huo  mfanykazi  anatakiwa  awe amepata  kwa  kiwango  cha  chini siku  28  kwa  ajili  ya  mapumziko.  Haya  ni  mapumziko  ya  kisheria  na  wala  si  hiyari  wala  hisani  ya  mwajiri. Kwa  ufupi  ili  kulielewa  hili  ni  kuwa  kila  mwaka  au  ndani  ya  miezi 12  mfanyakazi  anstahili  likizo  ya  mwezi  mmoja.  

4.LIKIZO   YA  UGONJWA .

Kwa upande wa  malipo katika likizo  ya  ugonjwa huwa  hivi, Siku  63  za  mwanzo  tangu  mfanyakazi  augue  anastahili kulipwa  mshahara  wake   wote.  Siku  63  zinazofuata  ndani ya  ugonjwa  mfanyakazi anatakiwa kuendelea  kulipwa  ikiwa  ugonjwa  utaendelea lakini sasa  atalipwa   nusu    ya  mshahara  wake.  Aidha  fidia  nyingine  kama  za  kuumia  kazini  huongozwa na  na  Sheria  ya  Fidia  ya  Mfanyakazi ( Workmans compensation Act), siwezi kueleza  yote  hapa  kutokana  na nafasi.

5.LIKIZO  YA  UZAZI.

Hii  yaweza  kuwa  likizo  ya  uzazi  upande  wa  mwanamke   au  mwanaume. Upande  wa  mwanamke  huitwa  martenity  leave  na  upande  wa mwanaume  huitwa  partenity  leave.  Wote  mwanamke  na  mwanaume  wanastahili  likizo   anapopatikana  mtoto. Tofauti  ni  siku  za  kupumzika  ambapo  mwanamke  anatakiwa  kupata  siku  84.  Siku  84  ni  ikiwa  amejifungua  mtoto  mmoja  na  ikiwa  amejifungua  mtoto  zaidi  ya  mmoja   basi  anastahili   likizo  ya siku  100.  Mwanaume  anastahili  kwa kiwango  cha  chini  siku  tatu  za  mapumziko   ndani  ya  siku  saba  tangu  mke  wake  ajifungue.  Kwa hiyo  kama  we ni  mwanaume  unahesabu siku  saba  tangu  mke wako  ajifungue  halafu  ndani  ya  siku hizo   kabla  hazijaisha ndimo  likizo  ya  siku  tatu  ipatikane.

 6. MAPUMZIKO   YA   MSIBA.

Kisheria  mfanyakazi  hustahili  likizo  anapofiwa.  Siku  nne  ndizo  siku  za  mapumziko  ya  msiba. Mapumziko  ya  kufiwa  hutolewa  iwapo aliyekufa  ni  mama, baba, mtoto, dada, kaka,  baba  mkwe, mama  mkwe  yaani  wale  ambao  ni  ndugu  wa  karibu.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.     0784482959,  0714047241
bashiryakub@ymail.com                 TANGAZO   MUHIMU

VIWANJA     NA     NYUMBA          ZINAUZWA.

-WANASHERIA   WETU   WATAKUANDALIA   MIKATABA  YOTE  BURE  NA                    KUKUSIMAMIA  MPAKA   MANUNUZI    YAKAMILIKE   BURE.

-UHALALI   WA  NYARAKA   NA   UMILIKI   UMETHIBITISHWA  NA   WANASHERIA     WETU.

-UTAPEWA  MTU  WA  KUKUSAIDIA  KUFANYA  TRANSFER   KWA  HARAKA                 BURE.

-IKIWA   UTATOKEA   MGOGORO  NDANI   YA  MWAKA  TANGU  TAREHE  YA              MANUNUZI    UTAPEWA   WAKILI   WA   KUSIMAMIA  MGOGORO    BURE
                                                        0784482959.

 KUONA   BOFYA  HAPO  JUU    MWANZO  WA   BLOG.
  
                                                                       





0 comments:

Post a Comment