NA BASHIR YAKUB-
Mara nyingi
nimeandika kuhusu mirathi
lakini zaidi nimegusia habari ya usimamizi wa mirathi . Leo nimeona
ni muhimu kueleza mgao
wa mirahi kwa kuangalia nani
anapata nini kupitia Sheria ya mirathi ya serikali. Fuatana nami.
( A ) MGAO UKOJE IKIWA MUME AMEFARIKI AKAACHA MJANE, WATOTO
NA NDUGU ZAKE.
Kama mume amefariki na akaacha mjane na watoto basi moja ya tatu (
1/3) ya mali za marehemu zilizo kwenye mirathi anatakiwa apewe mke
wake. Mbili ya tatu( 2/3) ya mali hizo itaenda
kwa watoto wake.
( B ) MGAO UKOJE KAMA MAREHEMU
HAKUACHA WATOTO LAKINI KUNA MJANE.
Kama hakuna watoto walioachwa
na marehemu katika familia husika
lakini kuna mjane ,mali ya marehemu hugawanywa katika mtindo ambao ndugu
hupewa nusu (1/2), na mjane hupewa nusu
ya mirathi ya marehemu(1/2). Hii ni sawa kwa sawa.
(C)MGAO UKOJE IWAPO MAREHEMU
HAJAACHA NDUGU WALA MTOTO ISIPOKUWA MJANE TU.
Kama marehemu hajaacha ndugu wala
mtoto au watoto basi mali yote huchukuliwa na mjane.Ndugu kwa maana
ya hapa ni kaka, dada, mama mzazi
wa marehemu au baba n.k.
( D ) KAMA MKE AMEFARIKI
NA KAMUACHA MUME NA WATOTO
JE MGAO UKOJE.
Hapo juu tumeona mume akifariki akamuacha mke na watoto mke huchukua moja ya tatu na watoto au mtoto mbili ya
tatu. Hali iko hivohivo kwa mume naye
ana haki kama alizo nazo mke wake yaani kupata mirathi kutoka katika mali za
marehemu.Kwa maana hiyo mume hupata moja ya tatu(1/3) ya mali
za marehemu mkewe na mbili ya tatu (2/3)
huenda kwa watoto.
( E ) MGAO UKOJE IKIWA MKE KAFARIKI
NA KUMUACHA MUME BILA WATOTO.
Kama mke amefariki amemuacha mume
lakini hakuna watoto inaangaliwa
kama kuna ndugu. Ikiwa kuna ndugu basi ndugu hao wa mke hutakiwa kupata nusu ya mali(1/2) na nusu
inayobaki (1/2) huenda kwa mume. Kwa hiyo ndugu wa mwanamke ambaye ni marehemu
hupata sawa kwa sawa na mume
wake aliyeachwa.
( F ) MGAO UKOJE IKIWA
MKE AMEFARIKI NA
HAKUACHA NDUGU ISIPOKUWA KUNA MME
WAKE TU.
Ikiwa mwanamke ndiye amefariki na hakuacha
ndugu yeyote wala mtoto yeyote isipokuwa kamuacha mume wake tu basi
mume huyo huchukua mali zote za
mkewe.
( G ) MGAO WA MALI UKOJE
IWAPO WAZAZI WOTE
WAMEFARIKI ILA WAMEBAKI WATOTO /MTOTO
TU.
Sheria inasema kwamba kama wazazi wote wawili wamefariki,basi mali za marehemu
hupewa watoto wao. Kama mtoto ni mmoja na yuko peke yake mtoto huyo mmoja hutakiwa
kuchukua mali zote peke yake. Nasisitiza
hapa kuwa haijalishi mali
ni nyingi kiasi gani ,kama mtoto yupo peke
yake atachukua yote. Hapo hakuna ndugu wala wazazi wa marehemu. Pia kama wapo wengi,basi watoto hao hugawana mali hizo
sawa kwa sawa bila kujali ni mwanamke au
mwanaume.
( H ) MGAO UKOJE IKIWA
BABA NA MAMA WOTE
WAMEFARIKI NA
HATA WATOTO WAO WOTE WAMEFARIKI.
Kama wazazi wote baba na mama wamefariki, lakini pia na watoto wao wote
nao wamefariki mali huenda
kwa wajukuu. Haijalishi mjukuu wa
kike au wa kiume mgao hutakiwa kwenda sawa kwa sawa.
( I ) MGAO
UKOJE IKIWA
MTOTO MWENYE MALI AMEFARIKI AKAWAACHA WAZAZI.
Wakati mwingine huwa
inatokea wazazi wana mtoto hajaoa/kuolewa na wala hana
mtoto lakini ana mali. Mtoto huyu akifariki mali zote
huenda kwa wazazi wake.
( J ) ZINGATIA SANA
HAYA.
Tanzania kuna sheria
nne ambazo hutumika kugawa mirathi. Kwanza
sheria za kimila, pili sheria
za kiislamu , tatu sheria ya urithi ya serikali ( Indian
Sccession Act), na nne sheria ya mirathi
ya watu wenye asili ya Asia. Swali la
sheria gani kati ya
hizo itumike katika kugawa mirathi
hutegemea na mambo yafuatayo, kwanza maisha aliyoishi
marehemu. Marehemu kama aliishi
maisha ya dini labda alikuwa mwislamu safi na ,maisha
yake yalikuwa ya kiislamu
basi sheria itakayotumika
kugawa mali ni ya
kiislam.
Halikadhalika kama aliishi maisha
ya kimila sheria
ya kimila itatumika. Kwa hali ya
sasa maisha ya kimila yako zaidi vijijini. Kama aliishi kikristo na alikuwa mkristo safi sheria
ya urithi ya serikali ( Indian
Succession Act) ndiyo itakayotumika. Pia
wenye asili Asia kama wote
tunavyojua hupenda kuishi maisha
kama ya wenzao wa Asia japo huwa tuko nao nchini humu. Basi nao ikitokea hivyo sheria mirathi
ya Asia itatumika kugawa mali.
Makala haya yameangalia
mgao wa mali za marehemu
kwa kutumia sheria ya mirathi ya
serikali ( Indian Succession Act) ambayo hutumiwa kwa wakristo na wale
wote walioacha maisha ya kimila.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA
GAZETI LA SERIKALI
LA HABARI LEO
KILA JUMANNE , GAZETI
JAMHURI KILA JUMANNE
NA GAZETI NIPASHE
KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com
TANGAZO MUHIMU
VIWANJA NA NYUMBA ZINAUZWA.
-WANASHERIA WETU WATAKUANDALIA MIKATABA YOTE BURE NA KUKUSIMAMIA MPAKA MANUNUZI YAKAMILIKE BURE.
-UHALALI WA NYARAKA NA UMILIKI UMETHIBITISHWA NA WANASHERIA WETU.
-UTAPEWA MTU WA KUKUSAIDIA KUFANYA TRANSFER KWA HARAKA BURE.
-IKIWA UTATOKEA MGOGORO NDANI YA MWAKA TANGU TAREHE YA MANUNUZI UTAPEWA WAKILI WA KUSIMAMIA MGOGORO BURE
0783851726.
Naomba usaidizi wa swali langu.
Baba yangu alizaa watoto wanne kabla yy hajafariki,dada yetu akafariki na kuacha mtoto mmoja,baadae baba yetu nae akafariki,je huyu mtoto wa Dada etu ana haki ya kurithi Mali za babu yake kupitia kwa mama yake?