NA BASHIR YAKUB-
Kawaida unapokuwa umeingia katika
mkataba au makubaliano katika jambo lolote lile kunakuwa na masharti ambayo
unapaswa kuyatimiza au kutimiziwa. Na hapa nazungumzia mikataba yote uwe wa
kuuza mbuzi au ule wa kujenga ghorofa mia, yote ni mikataba. Masharti hayo huwa
ndio makubaliano yenyewe au twaweza kusema kuwa ndio mkataba wenyewe. Kila
upande unawajibika juu ya
utekelezaji wa masharti hayo. Yeyote anayefikia hatua ya kukiuka masharti hayo au hata kukiuka sharti moja tu, hana namna ila
kukubaliana na hatua na
utaratibu wa kisheria kuhusu uvunjwaji
au ukiukwaji wa mikataba.
1.KUKIUKA MKATABA AU MAKUBALIANO.
Uvunjaji wa mkataba unaweza kutokea katika njia
nyingi. Moja ni ile ya kawaida ambapo mtu huamua kujitoa kwa kusema,kutamka au kuandika kuwa sasa
sitafanya hili na lile hata kama lipo katika makubaliano yetu. Pili njia nyingine ya kuvunja mkataba ni pale ambapo mtu
hasemi kwa kutamka kwamba sasa sitafanya hili wala lile isipokuwa hatimiza wala
hatekelezi kile mlichokubaliana. Ifahamike kuwa mtu anapoingia mkataba na mtu
mwingine au kampuni na
kampuni au kampuni na mtu sheria inalazimisha kutekeleza kwa usahihi yale
yote yaliyokubaliwa katika
mkataba huo. Utekelezaji wa baadhi ya masharti na kuacha mengine au
kutotekeleza yote kabisa ni uvunjaji au ni kujitoa katilka mkataba kwa mujibu
wa sheria. Aidha nasisitiza kuwa ili mtu ajitoe katika mkataba sio lazima aseme
kuwa nimejitoa katika mkataba. Kitendo cha kutofuata makubaliano kama yalivyokubaliwa ni kujitoa katika mkataba moja kwa
moja.
2.KUMDAI FIDIA ALIYEKIUKA
MKATABA AU MAKUBALIANO.
Si vyema mtu akafanya
makubaliano na mtu mwingine halafu
akapotea bila kutekeleza
kile kilichokubaliwa. Ni sababu
hii inayonifanya kuwaambia
watu kuwadai fidia wale wanaokiuka
masharti. Kudai kulipwa
fidia baada ya kuvunjwa
mkataba ni takwa la kisheria
na hivyo si
ukorofi kama ambavyo mtu anaweza kufikiri.
3.AINA ZA FIDIA UNAZOWEZA
KUDAI UKIVUNJIWA MKATABA.
( a ) Fidia zipo za aina nyingi. Kwanza kuna fidia ambayo utatakiwa
kulipa kutokana na makubaliano yenu ya awali wakati mnaingia mkataba. Hii ni
aina ya fidia ambayo wahusilka katika mkataba hukubaliana awali kabisa wakati wanaingia katika
mkataba ambapo hupanga
kiasi cha fidia ambacho watalipana iwapo mmoja kati yao atakiuka au kujitoa
katika mkataba. Kwa kuwa fidia hii huwa imeandikwa
na ipo ndani ya mkataba basi aliyekiuka au kujitoa katika mkataba hutakiwa
kulipa fidia hiyo kulingana
na makubaliano yao mara moja.
( b ) Fidia
nyingine ni ile ambayo mtu hutakiwa kulipa iwapo wakati wanaingia
mkataba hakuna fidia yoyote waliyokuwa wamekubaliana kulipa iwapo mmoja wao
atakwenda kinyume. Hii ni aina ya
fidia inayotathminiwa na mahakama. Mahakama hutathmini fidia hii kwa
kuangalia mambo mawili yaani kiwango cha
ukiukwaji wa mkataba na hasara zilizotokana
na ukiukwaji huo. Kupitia hayo mahakama huweza kutangaza kiwango cha fidia
anachotakiwa kulipwa mtu ambaye amevunjiwa mkataba.
4. FIDIA NYINGINEZO.
( a ) Aina nyingine
ya fidia inayoweza kuombwa mahakamani baada ya mkataba kuvunjwa ni ile fidia ambayo itamweka mtu
aliyevunjiwa mkataba katika nafasi fulani ambayo angekuwepo iwapo mkataba ule ungefanyika.
Mfano uliingia mkataba fulani na mtu au kampuni na iwapo mkataba ule ungetekelezwa
kwa ukamilifu ulipaswa kupata faida ya shilingi milioni mia moja. Kutokana na hilo
unaweza kuiomba mahakama ili ulipwe kiasi cha pesa hizo kama faida ambayo
ulitakiwa kupata iwapo mkataba usingevunjwa.
( b ) Pia fidia nyingine anayoweza kudai mtu ni ile ya kutaka alipwe kutokana ma
kiwango cha kazi iliyokuwa imefanyika tu na si vinginevyo. Mfano umeingia mkataba wa kumpelekea
mtu gunia mia za mchele.
Wakati umefikisha gunia khamsini mkataba unavunjwa na unaambiwa usilete nyingine.
Kwa maana hii utakapokwenda mahakamani kuomba fidia unaweza kuomba mahakama itathimini fidia kutokana
na mkataba mzima yaani gunia mia au unaweza kuomba fidia itathminiwe kutokana
na gunia khamsini tu
yaani fidia kutokana na
kazi ambayo ilikwisha fanyika tu.
5.KAMA UMEVUNJIWA MKATABA NA HUTAKI FIDIA WAWEZA PIA KUOMBA HAYA .
Yatupasa pia kujua kuwa sio lazima kila mkataba
unapovunjwa uombe fidia. Yapo mambo mengine ambayo unaweza kufanya kama tutakavyoona hapa.
( a ) Kwanza unaweza kwenda mahakamani kuomba lifanyike lile lililokuwa linapaswa
kufanyika ndani ya mkataba,
Mfano uliingia
mkataba wa kuletewa vitabu
miambili ambapo
vimeletwa mia tu na vingine
havikuletwa. Unaweza kwenda mahakamani ukiomba mahakama kumlazimisha mhusika
kumalizia vile vitabu mia ambavyo alikuwa hajamlizia na si vinginevyo. Au ulimlipa hela katika tenda ya
kukujengea nyumba ambapo alijenga kidogo na hakumalizia. Unaweza kwenda
mahakamani ukiiomba mahakama itoe agizo la kumtaka mhusika amalizie ile sehemu
iliyobaki na si vinginevyo. Hii sio fidia na ni tofauti kabisa na fidia.
( b ) Kitu kingine ambacho unaweza kukiomba mahakamani
baada ya mtu kuwa amekiuka au amevunja
mkataba ni kuiomba mahakama itoe agizo la kurejeshwa katika hali yako ya
kawaida kama ulivyokuwa kabla ya
mkataba, Mfano kama mkataba ulikuwa wa kujenga
na kumaliza nyumba utaomba
urejeshewe hela yako na
ikiwezekana eneo lile
lisafishwe kwa kuvunja yale yote aliyokwisha jenga ili eneo
libaki kama lilivyokuwa awali kabla ya mkataba. Hii nayo sio fidia na ni
tofauti kabisa na fidia.
(
c ) Kitu kingine ambacho unaweza kuomba uwapo mahakamani baada ya kuvunjwa
au kukiukwa kwa mkataba ni
kuzuia kuendelea kwa utekelezaji wa mkataba, Mfano uliingia mkataba na mtu au kampuni ikujengee
nyumba au barabara ndani ya muda fulani. Lakini kutokana na makubaliano yenu
ujenzi ule unasuasua kiasi kwamba hauendi kama mlivyopanga. Kwa hali hii
unaweza kuiomba mahakama isitishe
utekelezaji wa mkataba kwasababu
ya kutoridhika na utekelzaji wa masharti. Halikadhalika hii nayo sio fidia na
ni tofauti kabisa na fidia.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA
GAZETI LA SERIKALI
LA HABARI LEO
KILA JUMANNE , GAZETI
JAMHURI KILA JUMANNE
NA GAZETI NIPASHE
KILA JUMATANO. PIA NI KATI YA WANASHERIA WAANZILISHI WA BLOG HII. 0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com
TANGAZO MUHIMU
VIWANJA NA NYUMBA ZINAUZWA.
-WANASHERIA WETU WATAKUANDALIA MIKATABA YOTE BURE NA KUKUSIMAMIA MPAKA MANUNUZI YAKAMILIKE BURE.
-UHALALI WA NYARAKA NA UMILIKI UMETHIBITISHWA NA WANASHERIA WETU.
-UTAPEWA MTU WA KUKUSAIDIA KUFANYA TRANSFER KWA HARAKA BURE.
-IKIWA UTATOKEA MGOGORO NDANI YA MWAKA TANGU TAREHE YA MANUNUZI UTAPEWA WAKILI WA KUSIMAMIA MGOGORO BURE
0783851726.
0 comments:
Post a Comment