NA BASHIR YAKUB-
Hapa kwetu Tanzania habari ya
kubambakiziana kesi ni kama mtindo. Mara nyingi matendo haya yamekuwa
yakifanywa na watu wenye uwezo kifedha
dhidi ya wasio na fedha pia kati ya maofisa wa polisi na
raia. Mtu kwasababu ana pesa au cheo anaweza kuamua kumfungulia yeyote
mashtaka. Watu
wengi wako magerezani kwa kubambikizwa kesi, hili wala sio siri tena. Siseme
walio mahabusu, hao nao hawana idadi. Inasikitisha mno. Ni wazi kuwa wengi wao wamefikia huko aidha kwa
kusingiziwa kosa na askari au mtu mwenye cheo au fedha. Lakini zaidi wametoka mikononi mwa
askari kwakuwa hata huyo mwenye cheo au fedha hawezi kumbambikizia mtu kesi
bila kupitia kwa askari. Kwahiyo askari
ndio tatizo kubwa katika hili.
1.NINI MAANA YA
KUBAMBIKIZWA
KESI.
Kubambikizwa kesi au
kumshtaki mtu kwa hila maana yake ni kumfungulia mtu kesi ya jinai bila mafanikio , na
bila sababu za msingi za kufanya hivyo na mtu huyo akapata athari zozote kutokana na kumfungulia kesi
hiyo. Athari ni pamoja na kupotezewa muda, gharama, usumbufu, kudhalilishwa,
kupata hasara kibiashara au kikazi kutokana na kushikiliwa na kila kitu ambacho
kimekuwa kama matokeo ya kusingiziwa
kesi ni athari kwa maana hii.
2. SABABU ZA KUWABAMBIKIZA WATU KESI.
Sababu za kumuuzia mtu kesi huwa ni nyingi. Ni nyingi
kutokana na kuwa kila
aliyebambikizwa kesi huwa kuna mgogoro nyuma
uliosababisha jambo hilo na migogoro
kawaida inatofautiana. Pamoja na
hayo sababu kuu za kubambikizia mtu kesi huwa ni kwa ajili ya kumkomoa au kulipiza
kisasi kutokana na chuki zilizotokana na mgogoro kama
nilivyosema.
3. WELEDI WA ASKARI WETU NA KUWABAMBIKIZIA RAIA KESI.
Wakati mwingine
askari wetu huwabambikizia watu kesi
katika mazingira ya
kushangaza kabisa. Askari
anaweza kumbambikizia raia
kesi kwasababu tu
raia amehoji jambo
fulani. Kwa mfano mtu anaweza kumuuliza askari nioneshe kitambulisho
chako kabla hujanikamata.
Utasikia askari akimwambia mtu unajifanya mjuaji tutaona, mara unanifundisha kazi utanitambua n.k. Eti mazimgira kama hayo
kwa askari wetu utakuwa tayari ni mgogoro na mtu
atapofikishwa kituoni basi ni rahisi kupewa
kesi ambayo si yake ilimradi tu askari aoneshe
kuwa aliposema utanitambua,
utaona alikuwa na uwezo
wa kufanya hivyo kweli.
4. ATHARI ZA KUWABAMBIKIZA WATU KESI.
Kwanza upelelezi wa
kesi ambayo haipo unagharimu pesa za
serikali na muda ambao kimsingi ungetumika kushugulikia kesi nyingine za watu
wanaohitaji haki kiukweli. Pili kesi hizi za
kubambikizwa zinaongeza idadi ya kesi mahakamani pasi na sababu za msingi na hivyo
kusababisha kesi za kweli kuendelea kuchelewa. Tatu kesi hizi ni usumbufu kwa
waliobambikizwa na ndugu zao na zinaathiri
nguvu kazi katika taifa kwani badala ya watu kuendelea na uzalishaji mali hubaki
kushughulikia kesi hizi zisizowahusu na baadhi yao kufungwa kabisa na hivyo
kupoteza moja kwa moja nguvu kazi katika jamii.
5.NAMNA YA
KUMSHITAKI ALIYEKUBAMBIKIZA KESI.
Kushitaki ninakokuongelea hapa
ni kushtaki kwa madai yaani
kumdai aliyekubambikiza kesi akulipe kutokana na tendo hilo ovu. Hivyo hii itakuwa ni kesi
ya madai na hatua zake ni hizi.
( a ) Kwanza
inategemea unataka akulipe shilingi ngapi. Kuanzia shilingi
moja mpaka milioni
tano utaenda mahakama ya mwanzo. Ukifika hapo mahakamani utaeleza shida
yako pale na watakusaidia kufungua
kesi hiyo. Aidha kuanzia milioni tano
na kuendelea mahakama unayotakiwa
kufungua kesi ni ya wilaya
na Mahakama kuu. Napo
ukifika mahakamani utaelekezwa
utaratibu wa kufungua kesi lakini kwa mahakana
hizi ni vema ukamuona mwanasheria
kabla ya kwenda mahakamani.
( b )Kwa ajili ya kufungua
shauri hilo utaratibu ni mwepesi kihivyo
na bila shaka baada
ya kufanya hayo
utakuwa umefungua kesi ya kulipwa
kutokana na kubambikizwa.
6.MAMBO UNAYOTAKIWA KUJIANDAA
NAYO ILI USHINDE KESI YA
KUBAMBIKIZWA.
( a ) Kwanza
hakikisha unatunza makaratasi yote yanayohusu ile
kesi ya jinai
uliyofunguliwa kwa kubambikizwa. Makaratasi( documents) hayo ndiyo
yatakayotumika kuonesha kuwa kweli kesi ya jinai
dhidi yako ilifunguliwa.
( b ) Zingatia sana
kuwa kubambikizwa kesi ni pale
tu unapofunguliwa mashtaka polisi na haijalishi mashtaka
hayo yamefika mahakamani
au hapana. Kitendo cha kufikishwa polisi kwamba umetenda kosa fulani wakati si
kweli tayari umebambikizwa kesi.
( c ) Pia kama
ulibambikizwa kesi ikafika
mpaka mahakamani na ukaachiwa huru hakikisha unapata nakala ya hukumu inayoonesha kuwa uliachiwa huru kwakuwa itakuwa ushahidi
kuwa kesi haikuwa ya kweli na ndio maana
mahakama iliitupilia mbali.
( d ) Tatu jiiandae kuonesha kuwa aliyekufungulia kesi alifanya hivyo bila
sababu za msingi. Yaani ionekane wazi kuwa hapakuwa na sababu zozote za msingi
za kufanya hivyo yaani kukufungulia mashtaka kama hayo.
( e ) Pia andaa ushahidi au mashahidi
ili kuonesha ni kwa kiasi gani
uliathirika kutokana na kubambikizwa kesi ili uweze kupata pesa ulizoomba kulipwa. Kuathirika
au kupata madhara
kunakoongelewa hapa sio lazima ziwe athari za kimwili tu. Zipo athari
kama mtu kuharibiwa hadhi yake katika jamii, athari ya kumharibia mtu sifa njema
katika jamii, na athari za kumpotezea mtu mali pamoja na
muda kutokana na kesi hiyo. Aidha athari ya mali na muda inatokana
na mtu kuacha kufanya shughuli zake na kuanza kusughulikia kesi hiyo ya uongo.
Katika kufanya hivyo ni rahisi mtu kufukuzwa kazi au kupoteza kazi yake kwa
namna yoyote ile ikiwa ni pamoja na kumharibia mtu mipango yake mbalimbali
ambayo ingeweza kumwingizia kipato. Haya yote yanahesabika ni athari ambapo mtu
aliyesababisha atatakiwa kuyafidia.
Na hizo athari si lazima zitokee zote. Hata ikitokea moja kati ya hizi
inatakiwa kufidiwa
( f ) Jambo jingine la
muhimu na la mwisho katika kufungua shauri la kubambikizwa kesi ni kuwa lazima
mashtaka aliyosingiziwa mtu yawe ni ya jinai. Yaani ulisingiziwa kutenda jinai kama kuiba, kubaka, kupiga, kutapeli, kutukana,
kusingiziwa kumiliki silaha, n.k.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA
GAZETI LA SERIKALI
LA HABARI LEO
KILA JUMANNE , GAZETI
JAMHURI KILA JUMANNE
NA GAZETI NIPASHE
KILA JUMATANO. PIA NI KATI YA WANASHERIA WAANZILISHI WA BLOG HII. 0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com
TANGAZO MUHIMU
VIWANJA NA NYUMBA ZINAUZWA.
-WANASHERIA WETU WATAKUANDALIA MIKATABA YOTE BURE NA KUKUSIMAMIA MPAKA MANUNUZI YAKAMILIKE BURE.
-UHALALI WA NYARAKA NA UMILIKI UMETHIBITISHWA NA WANASHERIA WETU.
-UTAPEWA MTU WA KUKUSAIDIA KUFANYA TRANSFER KWA HARAKA BURE.
-IKIWA UTATOKEA MGOGORO NDANI YA MWAKA TANGU TAREHE YA MANUNUZI UTAPEWA WAKILI WA KUSIMAMIA MGOGORO BURE
0783851726.
0 comments:
Post a Comment