Saturday, 21 February 2015

UNATAKA KUFANYA TRANSFER (KUBADILI JINA) LA KIWANJA/NYUMBA, UTARATIBU WA HARAKA NI HUU .

Image result for WIZARA YA ARDHI

NA   BASHIR  YAKUB-.

Watu wengi wamenunua viwanja/nyumba  lakini mali hizo zimeendelea  kubaki katika  majina  ya waliowauzia. Wapo ambao  imepita  hata  miaka  kumi  tangu wanunue  maeneo   lakini  bado  hawajabadili  jina kuingia  jina  lake. Zipo sababu  nyingi  zinazosababisha  hali hiyo  lakini  moja  ni  watu  kutokujua  umuhimu  wa kubadili  jina  kwa haraka. Hapa sizungumzii  tu  kubadili jina  isipokuwa nazungumzia  kubadili  jina  kwa haraka. Kupitia  makala  haya  napenda  kuwaamsha  watu kuhusu  umuhimu mkubwa wa  kubadili  jina  kwa haraka  iwapo umenunua nyumba/kiwanja  kwa  mtu. Ni muhimu  sana  kufanya  hivyo  na itakuepusha na mambo mengi.

1. KAMA  HUJABADILI   JINA  ALIYEKUUZIA   BADO                          NDIYE   MMILIKI.

Ikiwa  kutatokea  mgogoro  wa umiliki  wakati ambao umenunua  nyumba/kiwanja  na  hujabadili  jina  kwenda  kwenye  jina  lako   kuna  hatari  kubwa zaidi  ya  kupoteza  ulichonunua. Hii ni kutokana  na ukweli kuwa utapokuwa  unatatuliwa  mgogoro  wa nani mmiliki  swali la  kwanza  huwa ni nani   ambaye  nyaraka  ya umiliki ina  jina lake.

Yule  ambaye  jina lake  linaonekana  kwenye  hati au  leseni  ya  makazi  ndiye  hupewa  kipaumbele   na kwa mujibu  wa sheria  mwenye  jina  kwenye  hati  au leseni  ya  makazi  ndiye mmiliki. Wewe  uliyenunua  utakuwa  na mkataba  na  jina  lako litakuwa  kwenye  mkataba lakini  pamoja  na kuwa  na jina kwenye mkataba  bado  huwezi  kulinganisha  mkataba  na  hati au  leseni  ya  makazi. Jina  linalotokea  kwenye  hati  au leseni  ya  makazi  huwa  na nguvu  zaidi kuliko lile  la kwenye  mkataba.

2. UMUHIMU  WA  KUBADILISHA  JINA  KWA HARAKA.

Upo umuhimu  mkubwa  mara  tu baada ya  manunuzi  ya  kiwanja/nyumba  kukimbilia  hatua  za  kubadili  jina. Ni  vyema wakati unajipanga  kununua  nyumba/kiwanja  ukajipanga  moja kwa  moja  na  hatua  za kuanza  kubadili  jina  mara  baada  ya kukamilika  kwa  mkataba wa manunuzi.  
Mara  nyingi  tumekuwa  tukiwashauri  watu  kuwa  mkataba  wa  manunuzi  unapokuwa  umekamilika  leo  basi hakikisha  kesho unaanza  taratibu  za  kubadili jina( transfer). 

Ni  utaratibu huu pekee utakaokufanya  kujiamini  na ulichonunua. Pia  unapotokea  mgogoro  kabla  ya kubadili  jina  kuanzia  hapo unakuwa  na nafasi  ndogo  ya kuweza kubadili jina kwakuwa  kama mgogoro  utaenda mahakamani  inaweza kutokea  kuzuiwa  kufanya  hivyo  mpaka  kesi itakapokwisha. Kesi  yenyewe itaisha lini haijulikani . Kama ikiisha  baada  ya  miaka  kumi,  kumi  na tano    ina maana  muda wote  huo utakuwa una  mali  ambayo  ni kama  si  ya kwako.

3. UTARATIBU  WA  KUBADILI  JINA( TRANSFER)  BILA                   USUMBUFU.

( a ) Kwanza  hakikisha  una  mkataba  wako wa kununulia  ambao  una  muhuri  wa wakili   uliondaliwa   kitaalam huku  ukiwa  na picha  za wote  mnunuzi  na muuzaji ikiwa  ni  pamoja  na sahihi  zenu wote.  Kwa  ufupi  hakikisha   mkataba  wako  ni mzuri  ambao  una  viwango  vya  kisheria  ili kuepuka  kurudishwa rudishwa kwa ajili  ya marekebisho au  kukataliwa  kabisa   uwapo  mamlaka  za ardhi.

( b ) Pili hakikisha  una  fomu  namba  29  ambayo  ni taarifa  ya  kutoa  umiliki .Fomu hii ni taarifa  maalum  ambayo  aliyekuuzia  anatoa  taarifa  kwa  kamishna  wa ardhi  kuwa  anataka  kutoa  umiliki wake  kwa  wewe  mnunuzi. Atakuwa  akizungumza  kwa  mtindo  wa kiapo  kuwa mimi  fulani  wa sehemu  fulani  ninatarajia kutoa  umiliki  wangu  wa ardhi  wa eneo fulani  kwa  fulani  fulani.  
Mwisho  muuzaji ataweka sahihi  yake na atakuwa ameichambua  plot  anayotoa  umiliki  na  anuani  zake  za makazi  zitakuwa zimeoneshwa vyema. Fomu  hii  hupatikana  mamlaka  za  ardhi  na  kwenye  ofisi  za wanasheria.

( c ) Tatu ni kujaza  fomu  Namba 30  ambayo  ni kudhibitisha  nia  ya  kutoa umiliki. Ile  ya juu namba 29  inatoa  umiliki  wakati  hii inathibitisha  nia ya  kutoa  au  kuachia umiliki  kwenda kwa mnunuzi. Hivyo hii namba  30  ni msisitizo wa namba  29. Hii ni  kutokana  unyeti  wa masuala  ya ardhi. Aidha taarifa  nyingine  katika  fomu hii ni zilezile  zilizo  katika  fomu namba  29. Fomu hii  nayo  hujazwa  na  muuzaji  tu na hupatikana  mamlaka  za ardhi  au ofisi  za wanasheria.   

( d )Nne  baada  ya  fomu  hizo  hapo  juu sasa inakuja  fomu  namba  35  ambayo ni  fomu rasmi  ya kuhamisha  umiliki ( transfer  of right  of  occupancy). Katika  fomu hii ndimo  muuzaji  anapotamka  rasmi  kuachia  umiliki  na  kuutoa  kwa mnunuzi  ikiwa  ni pamoja  na kuainisha  bei  ya mauzo.

Fomu hii itachambua  nyumba/kiwanja  ambacho  kimetolewa umiliki  na  hii itakuwa  na  majina  yote mawili  yaani  muuzaji  na mnunuzi. Pia  itakuwa  na  sahihi  zao  wote  ikiwa  ni pamoja  na picha. Pia  itakuwa  na muhuri  wa wakili  akiwa  kama  shahidi  wa  wote  wawili  muuzaji  na  mnunuzi. Fomu  hii nayo  hupatikana  mamlaka  za ardhi na  ofisi  za wanasheria.
      
       4.                 LAZIMA  UWE  NA  RISITI   ZA  KODI.

Hiki  ni  kiambatanisho  kingine  kinachohitajika. Utatakiwa  kupeleka  taarifa ya uthamini  wa ardhi mamlaka  ya mapato  ambapo kupitia taarifa  hiyo watakupa  hesabu  za kodi  utalipa  na utapewa  risiti  na  risiti  hiyo  ndiyo  utakayoambatanisha  kwenye  maombi  yako.

      5.                       USHAURI  WA  KITAALAM.

Hakikisha  siku  ya  kununua  nyumba/kiwanja  inakuwa  ndio  siku  ya  kuanza  hatua  za  kufanya  transfer. Kuchelewa  kunapunguza hadhi  yako  ya umiliki  na  kunakuweka  karibu zaidi  na mgogoro. Ni  vigumu  kumaliza  mgogoro  kwa usalama  pindi utakapotokea ukiwa haujafanya  transfer.  Zingatia sana  haya.

Image result for AKIWA ANAANDIKA
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.  PIA     NI   KATI     YA WANASHERIA    WAANZILISHI   WA    BLOG    HII  0784482959,       0714047241              bashiryakub@ymail.com


0 comments:

Post a Comment