NA BASHIR YAKUB--
Makala zilizopita nilieleza mambo au taarifa muhimu zinazopaswa kuwa kwenye mkataba wako unapokuwa unanunua nyumba/kiwanja. Nikasema katika niliyosema kuwa mkataba lazima uoneshe ukitokea mgogoro utatatuliwa vipi, ueleze kuwa utapotokea mgogoro muuzaji lazima awajibike kuhakikisha anakupa ushirikiano mnunuzi ili kumaliza mgogoro huo na kuwa muuzaji kama ana mke basi mke wake ni lazima aandaiiwe nyaraka iitwayo ridhaa ya mwanandoa ambayo ni tofauti na mkataba na aisaini pamoja na kuweka picha yake. Nilieleza mengi lakini hayo ni baadhi tu. Leo tena naeleza hatua muhimu sana au ya lazima na lazima haswaa kwa mnunuzi wa kiwanja/nyumba ambayo anatakiwa apitie kabla ya kufanya manunuzi.Hatua hii kwa jina la kitaalam huitwa OFFICIAL SEARCH kwa lugha rahisi tu waweza kuiita utafiti,upekuzi, upembuzi au upelelezi rasmi ambayo hufanywa na wanasheria. Mi napenda niite upelelezi.
(1)AINA ZA VIWANJA/NYUMBA UNAPOTAKA KUFANYA
UPELELEZI KUJUA KAMA KUNA
MGOGORO.
Nyumba/viwanja tunavyouziana
kila siku vimegawanyika katika hadhi mbalimbali. Kwanza kuna nyumba/viwanja vyenye hati, vyenye leseni za makazi, vyenye
ofa na ambavyo havina hati, leseni ya makazi wala ofa.Kutokana na makuzi ya
miji yetu viwanja/nyumba zenye hati mara nyingi huwa ni chache sana.Zenye leseni
za makazi ni nyingi kiasi na haya ni maeneo ambayo hasa hujulikana kama uswahilini. Zenye ofa huwa
ni chache nazo kwakuwa ofa ni hatua anayopitia mtu anapoelekea kupata hati au leseni ya makazi. Pia maeneo ambayo hayana hati wala leseni ya makazi wala ofa nayo ni mengi sana pia. Kwa Dar es salaam haya ni maeneo ya pembeni pembeni
mwa mji Tegete,bunju, pugu, chanika, mbagala, baadhi ya maeneo ya kigamboni n.k. Hata hivyo eneo liwe na hati leseni ya makazi au hapana bado
kisheria linatambulika .
(2)NAMNA YA KUJUA KAMA NYUMBA/KIWANJA KINA MGOGORO
Kama kiwanja/nyumba
ina hati kuna maombi rasmi ya kisheria ambayo huwa yanafanywa
kwenda ardhi wizarani, wizara ya ardhi makao makuu kwa Dar es salaam na kwa mikoani maombi hayo
mara nyingi huenda makao makuu ya
mkoa ambapo katika
maombi hayo mnunuzi anaiomba
mamlaka ya ardhi imjulishe mambo
yafuatayo;
( a ) KUJUA JINA
LA MMILIKI HALALI
WA NYUMBA/KIWANJA.
Kwanza kujua jina la
mmiliki. Jina hili linatakiwa kufanana sawasawa
bila tofauti yoyote na yule mtu
anayetaka kukuuzia eneo. Hii husaidia
kuthibitisha kuwa anayeuza ndiye kweli mmiliki wa eneo.Kama
majina yatatofautiana basi haraka sana achana
na hilo eneo ili kuepuka mgogoro.
( b ) KUJUA KAMA NYUMBA/KIWANJA
UNACHONUNUA KIMEWEKWA KAMA DHAMANA
YA MKOPO.
Kitu kingine
unachouliza kwenye hayo maombi rasmi ni
kama hiyo nyumba/kiwanja kimewekwa
kama dhamana kwa ajili ya vitu
kama mkopo . Wakati mwingine yawezekana mtu kukuuzia eneo ambalo limewekwa
dhamana kwa mkopo wa hela nyingi
tu. Na kisheria kama eneo limewekwa dhamana yule anayelimiliki kwa dhamana ndiye mwenye nalo kwa muda huo na wewe uliyenunua sheria iko wazi unakuwa umeliwa. Ieleweke kuwa ni vigumu sana kujua kama eneo unalouziwa limewekwa dhamana au hapana ikiwa hukufanya upelelezi huu. Wakati mwingine mtu huweka dhamana eneo lake na
kubaki na hati . Kwa hati ile wewe
mnunuzi ni rahisi kuhadaika kuwa eneo ni lake lakini kumbe ni eneo lenye deni kubwa. Ukinunua eneo kama hilo utakuwa
umenunua mgogoro mkubwa ambao wewe mnunuzi kushindwa na kunyanganywa
ulichonunua ni lazima tu.
( c ) KUJUA KAMA KUNA MGOGORO WA KIFAMILIA.
Kitu kingine ambacho utaomba kujua katika yale
maombi ni kama kuna mgogoro wowote wa kifamilia kama migogoro ya mirathi, migogoro ya kindoa ambapo mwanandoa mmoja anaweza kuwa
ameweka zuio kuhusu uuzwaji wowote wa nyumba/kiwanja
hicho. Usipofanya upelelezi huu utanunua halafu siku ya kubadilisha jina ndio
siku utajua kuwa eneo lile lilikuwa haliruhusiwi kuuzwa.Aidha ifahamike kuwa mamlaka za ardhi hupata taarifa hizi za
viwanja vya watu kupitia utaratibu wa mazuio uitwao CAVEAT.
( 3 ) MNUNUZI WA
ENEO LENYE LESENI YA MAKAZ I
AKAFANYE UPELELEZI WAPI.
Maeneo yenye
leseni za makazi maombi haya ya upelelezi wa kiwanja/nyumba yanapelekwa
manispaa. Manispaa
inayohusika ni ile ambayo lilipo eneo
husika . Kwa mfano ukitaka kununua eneo kinondoni manispaa ya
kinondoni ndiyo inayopelekewa
maombi, kama eneo unalotaka kununua lipo
temeke basi manispaa ya temeke ndio
ipelekewe maombi. Aidha
kuhusu mpangilio wa maombi na kile
unachotaka kujua kuhusu eneo ni
kama nilivyoeleza hapo juu kwenye
hati .
( 4 ) MAENEO AMBAYO HAYANA HATI,
LESENI ZA MAKAZI
UPELELEZI HUFANYIKAJE.
Kwakuwa maeneo ya namna hii yanakuwa hayana
nyaraka yoyote maalum katika
mamlaka za serikali basi wakati mwngine huleta ugumu
kidogo katika kujua ukweli ili kuepuka mgogoro. Lakini kitu ambacho huwa tunashauri katika
maeneo ya hivi ni kuwa kwanza muuzaji akueleze eneo alilipataje. Kama
alilinunua kwa mtu ni vema akaonesha ule
mkataba alionunulia na kama mauzo yatafanyika basi ni lazima mnunuzi apate kopi ya ule mkataba.
Pili kama amelirithi ni lazima aoneshe fomu ya usimamizi wa mirathi ambayo ndiyo itakuwa inampa mamlaka ya kuuza. Na kama alipewa zawadi basi aonesha
waraka wa zawadi ( deed of
gift) ambao umesajiliwa.
Jingine la msingi sana katika maeneo yasiyo na hati wala leseni za makazi huwa ni kuuliza majirani. Eneo unalonunua kama wapo majirani hebu waulize tu kwa nia njema na mara nyingi ukiwapata wawili watatu hivi ni rahisi kupata ukweli au kukuwezesha kujenga shaka. Na majirani usiwaulize kwa pamoja, mtafute mmoja mmoja kila mtu kwa muda wake ili kuepusha kuoneana haya katika kusema ukweli. Pia hakikisha wakati wa kuwahoji majirani muuzaji asiwepo, we tafuta tu muda wako nenda peke yako na pata taarifa. Uwepo wa muuzaji unaweza kuingilia (influence) ukweli. Usikurupuke utalia, ni hayo kwa leo.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA
GAZETI LA SERIKALI
LA HABARI LEO
KILA JUMANNE , GAZETI
JAMHURI KILA JUMANNE
NA GAZETI NIPASHE
KILA JUMATANO. PIA NI MKURUGENZI NA MWANZILISHI WA BLOG HII 0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment