NA BASHIR YAKUB-
Wakopwaji/wadaiwa wamekuwa wakipata shida sana kutoka kwa wanaokopesha. Mkopesha awe ni mtu binafsi,
taasisi ya fedha , kampuni binafsi au
mwingine yeyote wamekuwa wakiwasumbua sana wadeni
wao. Kubwa zaidi hasa taasisi za
fedha hutumia masharti ya mikataba ambayo
huwa yameandaliwa kitaalam kiasi cha
mtu ambaye si mwanasheria kutoelewa kwa undani maana yake
kuwabana wadeni ambao hushtukia
masharti hayo baada ya kuwa wameshaanza kudaiwa. Mbaya zaidi wamekuwa
wakifanya hivi bila kufuata taratibu za
kisheria. Kwakuwa wamemsaidia mtu kwa
kumkopa basi wamekuwa
wakiichukulia hali hiyo kama
leseni ya kufanya lolote ilimradi tu
wanadeni na wewe. Mali za watu
huuzwa hovyo , wengine hufikishwa mpaka
vituo vya polisi ilimradi
tu wakopeshaji hupenda kupindisha
utaratibu. Hapa tutaeleza baadhi ya mambo
kadhaa ya msingi ambayo
mkopeshaji haruhusiwi
kumfanyia mdeni.
1. WAKOPESHAJI KUTOFUATA TARATIBU KATIKA UUZAJI
NYUMBA/KIWANJA CHA MDENI.
Sababu kubwa ambayo
imekuwa ikisababisha wakopeshaji
hasa taasisi za fedha kutofuata taratibu wakati wa kuwadai wadaiwa ambao wako nje ya
mda kutokana na mikataba yao ya mkopo
ni kwasababu wadaiwa wenyeywe hawajui haki zao za
kisheria. Kama nilivosema hapo juu mikataba
ya kukopa fedha iko kitaalam sana
na ni watu wachache wenye uwezo
wa kugundua utaalam ambao unapatikana
katika mikataba ya
mikopo wanayoichukua. Mkopaji ana haki za
msingi katika hatua tatu muhimu za mkopo wake. Kwanza haki
wakati wa kuchukua mkopo, haki
wakati wa kurejesha mkopo, na haki wakati anaposhindwa kurejesha
mkopo. Wakopaji wengi hawajui haki zao katika hatua
hizi tatu muhimu. Hii ndio sababu hujikuta wakilazimika kuzisujudia taasisi zilizowakopesha
zinapokuwa zikiwatisha.
2. LAZIIMA MKOPAJI APEWE TAARIFA YA MAANDISHI
KABLA YA KUUZA NYUMBA YAKE.
Sheria ya Ardhi ya 1999 kifungu cha 25( 1) kimeweka bayana
kuwa mkopeshaji hapaswi
kuuza nyumba ya mdeni bila kumpa taarifa ya mandishi(notice). Huwezi kuamka asubuhi unaanza kutangaza mnada wa
nyumba ya mtu. Haya yamewakuta wengi
mtu mali yake inauzwa bila kupewa
taarifa ya maandishi. Wengine hupewa taarifa ya
mdomo kwa mfano mtu
anapozuru ofisi za taasisi iliyomkopesha
maafisa wanamwambia usipolipa jumapili tunauza nyumba yako halafu wanahesabu eti hiyo
ni taarifa. Kwa mujibu wa sheria
hiyo sio taarifa na huwezi kuuza nyumba
ya
mtu kwa taarifa ya namna hiyo.
3. KABLA
YA KUPEWA NOTISI YA KUUZA LAZIMA UWE UMEPITA MWEZI MMOJA.
Hapo juu tumeona
kuwa kabla nyumba kuuzwa ni lazima mdaiwa apewe notisi. Hata hivyo ili mdaiwa apewe
notisi ni lazima uwe umepita
mwezi mmoja tangu aache kulipa kama mkataba wake unavyosema. Hii ina maana kuwa mdaiwa hawezi
kuwa amepitisha mda wa malipo kwa
siku moja , wiki moja, wiki mbili au tatu halafu akaletewa notisi ya kutaka
kuuzwa nyumba yake. Kwa mfano mdaiwa alitakiwa kurejesha tarehe 1 / 1 / 2015. Tarehe 2, 3, 4 , 5 mpaka tarehe
30 hawezi kupewa notisi. Isipokuwa ni baada ya tarehe 30 ndipo anapoweza
kupewa notisi.
4. LAZIMA IPITE MIEZI MIWILI TANGU SIKU YA NOTISI
MPAKA KUUZA NYUMBA YA MDENI.
Hapo juu tumeona kwamba
notisi inatolewa siku thelathini baada
ya kupitisha mda wa kurejesha. Lakini hapa kumbe tunaona kuwa hata baada ya siku thelathini kupita na mdeni ukapewa notisi bado notisi nayo ina mda wake ambao ni tofauti ni zile
siku thelathini za mwanzo. Hii ni kusema
kuwa huwezi kumpa mdaiwa
notisi leo halafu ukauza nyumba yake kesho au
ukampa wiki hii halafu ukauza
wiki ijayo. Sheria inasema
mkopeshaji anaweza kuuza nyumba ya
mdaiwa baada ya kupita miezi
miwili tangu siku ya kupewa notisi ya
kuuza. Kwahiyo kama notisi ya kuuza
imetolewa mwezi wa kwanza uuzaji utafanyika mwezi wa tatu. Ina maana huu muda wote wa
katikati ni nafasi ya mdaiwa kujipanga kwa namna ya kulipa au kwenda mahakamani kuzuia
nyumba isiuzwe. Ni muda unaotoa fursa
ya haki ya mdaiwa kujipanga nini
afanye. Sio kama ambavyo taasisi za fedha zimekuwa zikifanya, mtu anapewa notisi
jumatatu halafu anaambiwa
nyumba yake inauzwa jumapili.
5. HUWEZI KUUZA NYUMBA YA MDAIWA BILA KIBALI
CHA MAHAKAMA.
Taasisi za mikopo
zimekuwa zikiuza nyumba za watu mara tu muda wa notisi unapoisha. Hii
hairuhusiwi kisheria kwakuwa muda
wa notisi ambao ni miezi miwili
unapoisha mkopeshaji lazima aende mahakamani afungue kesi dhidi ya yule anayemdai. Anayedaiwa naye ataitwa mahakamani
ataambiwa shauri lake atapewa nafasi ya
kujitetea na hukumu ya kawaida kama hukumu
katika kesi nyingine zilivyo itatolewa. Katika hukumu hiyo mkopeshaji anaweza kushinda au kushindwa.
Halikadhalika mdaiwa anaweza kushinda au
kushindwa. Mtoa mkopo akishinda basi ndipo atakapopewa kibali
maalum cha kuuza kama
mahakama itakuwa imeona
hiyo ndio suluhu. Kwa hiyo muhimu
hapa ni kuwa nyumba yako haiwezi kuuzwa bila hicho kibali cha mahakama. Suala kwamba muda wa rejesho na notisi tayari
umepita halitoi haki ya
moja kwa moja (automatic right) ya kuuzwa
kwa nyumba yako.
6. BAADA
YA MCHAKATO HUU NDIPO NYUMBA YA MDENI YAWEZA KUUZWA.
Kwanza ni baada ya
muda wa kulipa deni kumalizika na mdeni akapitisha siku thelathini. Pili baada ya muda wa notisi wa miezi miwili kuisha . Na tatu baada ya kesi kufunguliwa, kusikilizwa na kutolewa
hukumu ndipo hatua
ya kuuza nyumba inapofikiwa. Hii si
hatua nyepesi na ya
haraka kama ambavyo imekuwa ikitekelezwa na tasisi za mikopo. Ni mchakato ambao una muda.
7. USHAURI WA KITAALAM KWA WAKOPAJI/WADAIWA.
Muda wa kufanya mambo kienyeji umekwisha. Kufanya mambo kienyeji
ndiko kunakopelekea haki zako kuminywa.
Mkopaji/mdaiwa hakikisha unapata ushauri wa kisheria
katika hatua hizi, kwanza wakati ukitaka kuchukua mkopo, pili wakati wa kupitia mkataba wa mkopo ikiwezekana ule mkataba
mwanasheria aupitie na akushauri kwasababu mikataba ya taasisi za mikopo ina
mitego ambayo kwa mtu asiye na elimu ya sheria si rahisi kuigundua. Na tatu pata ushauri wa kisheria mara tu taasisi ya mkopo inapoanza kukusumbua au unapohisi
kuonewa. Kwa uzoefu wangu kwa kufuata
ushauri huu nyumba nyingi zimeokolewa mpaka
sasa na haki za watu zimepatikana.
8. UNAWEZA KURUDISHA
NYUMBA YAKO IWAPO
ILIUZWA BILA KUFUATA UTARATIBU NILIOELEZA.
Utaratibu wa kisheria
unapofuatwa ndipo jambo fulani huwa
halali na unapokiukwa jambo hilo huwa batili kuanzia hapo( ab
initio). Hii ni kusema kuanzia hapo( ab initio). Iwapo nyumba yako iliuzwa bila
kufuatwa kwa baadhi ya taratibu nilizoorodhesha hapa hata kama ilikiukwa moja tu bado waweza kuirudisha nyumba yako kwakuwa uuzwaji ule ulikuwa haramu na aliyenunua
alinunua kitu haramu. Hili wala si la
ajabu isipokuwa ndivyo sheria ilivyo. Na
wala mtu asihisi kuwa amechelewa kwakuwa masuala yanayohusu ardhi
sheria imetoa kipindi cha zaidi ya miaka kumi tangu kuonewa hadi kufungua shauri. Na hii haijalishi
nyumba yako iliuzwa kwa nani na sasa
amefanya maendelezo gani.
Yapo mengi kuhusu haki za
mkopaji yaliyo katika sheria Na. 4 & 5 ya 1999 lakini
leo tuanze na haya.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA
GAZETI LA SERIKALI
LA HABARI LEO
KILA JUMANNE , GAZETI
JAMHURI KILA JUMANNE
NA GAZETI NIPASHE
KILA JUMATANO. PIA NI MMOJA WA WANASHERIA WAANZILISHI WA BLOGI HII 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
Maelekezo haya ni muhimu na yakufaa sana kwa wanaojali.