Thursday 5 February 2015

JE UNAHITAJI PASIPOTI, HII NI NAMNA NYEPESI YA KUPATA PASIPOTI.



NA  BASHIR   YAKUB--

Yapo mambo  ambayo huwaumiza  watu vIchwa  yumkini  yakiwa  ni mambo madogo na ya kawaida.  Tatizo mara nyingi  huwa ni taarifa. Taarifa  zikimfikia  mtu ndipo huhisi jambo  ambalo alikuwa halijui  kuwa ni jepesi. Lakini kabla  ya taarifa mtu  huendelea kufikiria jambo hilo kwa ugumu. Katika kipindi kama hiki kuwa na kitu kama pasipoti si jambo la  anasa  au ufahari tena isipokuwa ni jambo  ambalo limeishaingia katika matumizi ya kawaida   ya kila siku ya walio wengi. Hii ni kutokana na kukua kwa  biashara za kimataifa, mawasiliano, utalii,usafirishaji  na kila kitu ambacho husababisha  watu kutoka nchi moja hadi nyingine.  Kwasasa kuwa na pasipoti  hata kama huna safari ya hivi karibuni ni jambo muhimu sana. Yumkini  usisubiri ikutokee safari ya ghafla halafu ndio uanze kukimbizana  na  pasipoti. Pasipoti inayo manufaa mengi  lakini moja ni kuwa pasipoti  ni mali kama mali nyingine. Pasipoti inaweza kumdhamini mtu kama  mali nyingine inavyoweza kumdhamini  mtu.Pasipoti  ni amana tena amana ya kuaminika. Ni  kutokana na umhimu huu nikaona leo nieleze  pasipoti na namna ya kupata pasipoti.

1.      PASIPOTI   HUOMBWA  NA  MWOMBAJI  LAKINI  HUBAKI MALI  YA  SERIKALI.

Hakuna mtu mwenye umiliki wa  kudumu wa pasipoti. Kwa mujibu wa sheria licha ya kuwa pasipoti hutolewa kwa jina na maelezo ya mwombaji,hati hiyo hubaki kuwa ni mali ya serikali. Hii ndio sababu serikali huweza kumnyanganya  mtu  pasipoti panapo jambo fulani. Ni kwakuwa pasipoti ni mali yake. Wewe  mwombaji uliyepewa pasipoti unayo haki ya  matumizi  na uhifadhi wake  lakini mmiliki  mkuu ni serikali.


2.     ILI   KUPATA  PASIPOTI  UNAHITAJI  KUWA  NA  VITU   HIVI.

( a ) Cheti cha kuzaliwa, hati ya kiapo au cheti cha uraia wa kuandikishwa cha mwombaji.Cheti cha kuzaliwa  ni hivi vyeti vya kawaida ambavyo hutolewa  mahospitalini  au mamlaka  nyingine baada ya kuzaliwa kwa mtu. Katika kipindi hiki wapo wengine wamekwisapata  vyeti vya uraia. Cheti cha uraia  chaweza kutumika kama mbadala wa cheti cha kuzaliwa. Pia tumesema hati ya kiapo. Hii hutolewa kwenye ofisi za wanasheria. Mwombaji huwa anaapa pamoja na mambo mengine  kuthibitisha kuwa taarifa anazozitoa  ni za kweli  kwa dhati yake. Pia  tukasema vyeti vya uraia wa kuandikishwa. Hivi  wanavyo raia wa Tanzania  ambao si wa kuzaliwa. Katika kuomba kupata pasipoti  nao hutakiwa  kuwa navyo.

( b ) Cheti cha kuzaliwa, hati ya kiapo au cheti cha uraia wa kuandikishwa cha
mzazi au wazazi wa mwombaji. Hapo juu tumeona vitu kama hivihivi lakini ilikuwa  ni kwa mwombaji wa pasipoti mwenyewe. Hivi  hapa sasa  ni kwa ajili ya mzazi wa mwombaji. Vile vitu vyote alivyowasilisha mwombaji  pale  juu ndio  vilevile anavyopaswa kuwasilisha  mzazi wa mwombaji. Si kwamba mzazi mwenyewe ndio anapeleka vitu hivyo hapana, wewe mwombaji ndio unabeba vitu hivi kwa niaba ya mzazi. Hapa mzazi ni yeyote anaweza kuwa baba au mama.Lengo lake  ni kutaka kujua historia fupi ya nasaba ya mzazi wa mwombaji.

( c ) Inahitajika picha ya hivi karibuni ya pasipoti size. Sharti kubwa waliloweka hapa  ni kuwa picha hiyo isiwe katika fremu. Fremu hapa si tu ile fremu ya kawaida tuliyoizoea bali pia hata pasipoti kuwa na maringo au mapambo ya kuzungushia pembeni nayo ni fremu kwa maana hii. Pasipoti iwe mnyooko(plain) isiwe na mbwembwe zozote.

( d ) Iwapo mwombaji ana umri wa chini ya miaka kumi na nane (18), wazazi walezi wawasilishe ridhaa ya maandishi. Nyaraka  hii ya ridhaa ya maandishi huandaliwa  na mwanasheria.Hii ni kusema kuwa utaratibu wa mtu mzima aliyevuka miaka kumi na nane  ni tofauti na mtu aliye chini ya  miaka hiyo katika kupata pasipoti. Baada ya kukamilisha vitu hivi kama  nilivyoeleza  basi hatua inayofuata ni kufuata utaratibu huu chini.

3.     FOMU ZA  MAOMBI  HUPATIKANA  WAPI.

Ofisi  za uhamiaji ndipo zilipo  fomu za maombi ya pasipoti. Hii ni popote  Dar es salaam au  mikoani. Suala la  msingi  ni kuwa ofisi hiyo iwe ya uhamiaji  utapata fomu hizo. Utachukua fomu hiyo utaijaza  na baada ya kuijaza itawasilishwa kwa mkurugenzi wa uhamiaji. Aidha suala jingine la msingi ni kuwa fomu hii itawasilishwa sambamba na nyaraka zote zinazotakiwa kama ilivyoelezwa hapo juu.

4.        BEI  YA  PASIPOTI   NI  KIASI GANI.

Ada rasmi ya kupata pasipoti ni fedha za Kitanzania kiasi cha shilingi 50,000/=( Elfu hamsini tu). Aidha kwakuwa wanasheria ndio hushughulika na kutafuta pasipoti basi bei yao haiingizwi katika ada rasmi ya serikali kama nilivyoieleza hapo juu.

5.      UNAWEZA  KUOMBWA  VIAMBATANISHO  VYA   ZIADA.

Jambo jingine ni  kuwa safari zimeainishwa kwa namna mbalimbali.Ukisoma nyuma ya fomu ya maombi utaliona hili. Kutokana na hilo wakati mwingine waweza kuombwa viambatanisho vya ziada. Hii ni kutokana na utofauti wa safari. Hii ni kusema kuwa yawezekana mwombaji akaombwa viambatanisho viitwavyo viambatanisho “maalum”. Hivyo basi mtu asishangae kukutana na kitu cha namna hiyo.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI  MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.  PIA  NI  MKURUGENZI  NA  MWANZILISHI  WA  BLOG  HII  0784482959,        0714047241           bashiryakub@ymail.com






0 comments:

Post a Comment