Wednesday, 11 February 2015

NINI UFANYE KISHERIA UNAPOHISI MWENZAKO KATIKA NDOA ANATAKA KUUZA NYUMBA/KIWANJA BILA RIDHAA YAKO.

Image result for kuweka zuio

NA  BASHIR  YAKUB-

Upo wakati kwenye  ndoa ambapo mmoja  wanandoa  anaweza akawa anataka  kuuza au kubadili jina la nyumba/kiwanja  bila ridhaa ya mwenzake ilihali  nyumba  hiyo  ni ya  familia. Lakini  pia  nje ya  hilo kuna  mazingira  ambayo  mtu anaweza  kuwa  si  mwanandoa lakini ana maslahi  katika  nyumba au  kiwanja cha mtu fulani  na anataka  kuzuia  nyumba/ kiwanja  hicho  kisibadilishwe  jina au kisiuzwe.  Kisheria jambo hilo linaruhusiwa  na huitwa zuio( Caveat).

Hili sio zuio la kwenda mahakamani  kama  mazuio tuliyoyazoea.Hili  ni zuio jingine  kama  nitakavyolieleza. Aidha  kuzuia hati  isibadilishwe  kimsingi ni sawa na  kuzuia nyumba isiuzwe.  Hii ni kwakuwa  hakuna namna ambavyo  mnunuzi anaweza kununua  kitu ambacho  hakiwezi  kubadilika  na kuingia  katika  jina  lake. Ikiwa  mke ana wasiwasi kuwa mume  anaweza kumzunguka  na kuuza mali ya familia  au mume ana wasi wasi juu ya uwezekano  wa mke kuuza basi wanayo  ruhusa  ya kuweka zuio ili hati  ya  nyumba  isibadilishwe.  Yapo mambo mengi kuhusu hili nitaeleza baadhi.
      
  1.         NINI  MAANA  YA  ZUIO.

Zuio ni usitishwaji wa muda ambao huwekwa ili kuzuia mabadiliko yoyote katika hati. Kama maana  yenyewe inavyojieleza  huu unakuwa ni usitishwaji wa muda  ambao unalenga  kulinda  maslahi ya  mtu aliyeomba  zuio.Kuitwa  zuio  la  muda haimaanishi  kuwa  mtu akizuia   itakuwa  ni mwezi mmoja  au  miwili basi, hapana. Ni  zuio  la  muda  kwakuwa  haliwezi kukaa milele  lakini  mtu akishaliweka  linaweza  kukaa  hata  miaka  mingi  kutegemea  na  sababu  za  zuio  hilo.

      2.      MWANANDOA   KUZUIA   HATI  ISIBADILISHWE.

Lazima  ieleweke  wazi kuwa si  kila  mtu anaweza  kuamua  na akazuia   hati  ya mtu isibadilishwe  . Wapo watu ambao  kwa mujibu  wa  sheria  wanayo  haki  ya  kuomba  hati  isibadilishwe.  Kwanza mke au mume  mmoja  kati  yao anaweza  kuweka  kizuizi katika nyumba ya ndoa (matrimonial  home) iwapo kuna  dalili  kuwa mmiliki aliyeandikishwa  anaweza kuiuza au  kuiweka  rehani  bila ya ridhaa ya mwingine. Mara  nyingi  migongano  katika  familia  inapoanza  mmoja  kati  ya wanandoa  hukimbilia  kuuza  baadhi  ya  mali  kwa aidha kumkomoa  mwenzake au  sababu nyingine yoyote.  Kwa hiyo  ili kuliepuka  hilo unapogundua  kuwa  kuna  uwezekano  huo  basi  sheria  imekuruhusu  mwanandoa  kuweka  zuio  ili  hati  isibadilishwe  na hivyo  kuepuka kuuzwa kwa  mali.

3. HATA  MKOPESHAJI   NAYE  ANAWEZA  KUWEKA   ZUIO KWENYE   HATI   YAKO.

Nimezungumzia  zaidi  wanandoa  kuzuia   lakini  pia  ieleweke  wazi kuwa suala  la  kuzuia  si  tu la wanandoa. Kampuni, shirika, mtu  binafsi au taasisi  ya  fedha  iwapo imemkopa  mtu  na  akaweka  nyumba/kiwanja  kama  dhamana  ambacho  kina  hati basi  wanayo  ruhusa  ya  kisheria  ya  kuomba  zuio  liwekwe  kwenye   hati ile  ili dhamana  isije kutumiwa  kukopea  pesa  katika  taasisi  nyingine  au  kuuzwa  wakati ipo  kulinda  deni. Kwa hiyo  iwapo  mtu ana  maslahi ya  namna  hii kwenye  ardhi  inayomilikiwa  na mwingine  basi  ni haki  kwake  kuweka  zuio hili  ili  kulinda  maslahi  yake.

4. WAPI UPELEKE MAOMBI YA KUZUIA  HATI           ISIBADILISHWE.

Mamlaka  za ardhi  ni mamlaka  ambazo  hutakiwa  kupelekewa  maombi  haya  ya  zuio.  Mara nyingi  mamlaka  za ardhi  huwa zipo  katika  ofisi  za wilaya  au  manispaa katika mkoa wako isipokuwa  kwa walio  Dar  es salaam  maombi  hupelekwa   makao  makuu  pale  wizara  ya ardhi  kama  ni hati.

5. MAOMBI YA KUZUIA HATI ISIBADILISHWE         HUANDALIWAJE.

Maombi  haya  si  maombi  kama  maombi  mengine  yalivyo. Maombi  haya  ni maombi  ya  kisheria  na  huandaliwa   katika  ofisi  za wanasheria   na  hupelekwa  yakiwa  na  muhuri  wa mwanasheria. Karika  maombi  hayo  mwombaji  hueleza  jina  lake  kwa urefu, anuani  yake,  uhusiano  wake  na  yule ambaye  jina  lake  ndilo  liko kwenye  hati yaani anayemwekea zuio   huku  akieleza  sababu  za  msingi  kwanini   anataka  kuzuia  hati  isibadilishwe.

6.  LAZIMA  MAOMBI  YAAMBATANE  NA  NYARAKA  HIZI.

Kwanza,  picha  2  za mwombaji  huku kila picha  moja  ikibandikwa kwenye  nyaraka  moja.

Pili, risiti  za malipo ya ada ya usajili. Maombi  haya hulipiwa  kiasi  cha  fedha lakini si kikubwa sana kwahiyo  lazima uambatanishe  na risiti  za malipo.

Tatu, mwombaji aambatanishe vielelezo vinavyompa haki juu ya kiwanja husika kwa  mfano  cheti  cha  ndoa, mkataba  wa mkopo n.k.
Kwa  leo  ni hayo.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.  PIA NI KATI  YA  WANASHERIA  WAANZILISHI  WA BLOG HII.  0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com



0 comments:

Post a Comment