NA BASHIR YAKUB-
Wapo watu ambao baada ya
kupata
cheo au nafasi ya kuwa
wasimamizi wa mirathi hugeuka waungu.
Huwa hawaambiwi wala hawasikii
la mtu. Huwezi kuamini kuwa
kuna baadhi ya wasimamizi wa
mirathi wamekataa kugawa
mali za marehemu sasa ni zaidi ya miaka kumi. Na
si kwamba wamefanya hivyo kwa maslahi mapana ya familia, hapana. Wamefanya hivyo kwa ukorofi lakini kubwa zaidi wanafanya hivyo
ili waendelee kunufaika na mali za marehemu peke
yao. Mambo hayo yameleta sana faraka
kwenye familia.
Warithi na wote wenye
haki katika mali za marehemu wengi wao huchukizwa na
matendo haya yumkini wapo ambao hujua
la kufanya na wapo ambao hubaki njia panda wasijue la kufanya. Mali zinaliwa
lakini warithi
wafanye nini, hawaoni njia.
Katika makala haya nini mfanye iwapo hamridhishwi au hamumtaki kabisa
msimamizi wenu wa mirathi ni kati ya mambo
yatakayoguswa.
1. MSIMAMIZI WA
MIRATHI NI NANI.
Msimamizi wa mirathi ni mwakilishi
halali wa kisheria wa mambo yote ya marehemu na mali zote za
marehemu
ambazo huwa chini
yake. Neno mwakilishi katika maana hii
linamaanishi uwakilishi kama uwakilishi tunaoujua. Uwakilishi sio umiliki. Hivyo msimamizi
wa mirathi ni mwakilishi .
Msimamizi wa mirathi
hupatikana kwa njia
mbili kwanza huteuliwa na marehemu
mwenyewe kupitia wosia na pili
huweza kuteuliwa na wana familia ikiwa marehemu hakuacha wosia au aliacha wosia lakini wosia
wenyewe hauoneshi kwa namna
yoyote ile nani awe msimamizi wa
mirathi.
2. AINA ZA WASIMAMIZI
WA MIRATHI.
Wafuatao wanaweza kuwa wasimamizi wa mirathi:
Kwanza ndugu wa marehemu na wale wenye maslahi na
mirathi ya marehemu. Hawa wanaweza kuwa
ni watoto, wazazi, wajukuu, kaka au
dada wa marehemu na ndugu
au wasio ndugu
kutegemeana na nani alikuwa
hai wakati wa kifo cha marehemu au
wakati mirathi inachakatwa.
Pili, kabidhi wasii mkuu
anaweza kuwa msimamizi
wa mirathi ya
marehemu. Kabidhi wasii ni ofisi ya
serikali ambayo hujihusisha pamoja na mambo mengine,usimamizi wa mirathi,endapo
itaombwa na mtu yeyote lakini
mwenye maslahi katika mali za marehemu au
marehemu mwenyewe wakati wa uhai wake.
Tatu, mwakilishi wa kisheria wa mtu aliyetajwa kama msimamizi wa
mirathi (mtu aliyepewa power of attorney).
Mtu aliyeteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi
naye anaweza kumpa mtu mwingie
kitu kiitwacho nguvu za kisheria (power of attorneys)
ambapo kupitia kitu hicho yule aliyepewa atakuwa na mamlaka sawa na yule msimamizi
wa mirathi. Lakini hii ni katika mazingira malum
ya kisheria. Aidha huyu aliyepewa
naye ataitwa msimamizi wa
mirathi. Wapo wengine hao ni
baadhi tu.
3. JINSI YA KUMUONDOA MSIMAMIZI
WA MIRATHI MKOROFI.
Zipo njia mbili
za kulitekeleza hili.
( a ) Kumtaka ajiondoe mwenyewe. Haki hii anayo mtu yeyote mwenye maslahi na mirathi
ya marehemu. Nimesema hapo juu kuwa wenye
maslahi wanaweza kuwa watoto,
wazazi, ndugu, jamaa, wajukuu kutegemea na nani yupo hai. Hawa wote wana haki ya kumtaka msimamizi ajiondoe katika usimamizi. Haijalishi aliteuliwa na marehemu au wanafamilia. Watu
wengi hujua msimamizi wa mirathi
ambaye ametajwa katika wosia na marehemu hawezi kuondolewa . Hili si
kweli hata kama aliteuliwa
na marehemu akifanya mambo
nitakayotaja hapa baadae
kuondoka kwake si kwa hiyari.
( b ) Njia ya
pili ya kumuondoa
msimamizi wa mrathi ni njia
ya mahakama. Hii mara nyingi hutumika
iwapo ile ya kwanza ya kujiondoa kwa hiyari
inaposhindikana. Njia hii hufika
mahakamani kwa njia ya pingamizi. Aidha mtu yeyote ambaye anaona ana haki au ana maslahi na mirathi ya marehemu
anaweza kuweka pingamizi mahakamani dhidi ya msimamizi wa mirathi ikiwa kama
njia ya kumkataa na
kama mahakama itaridhika
basi ataondolewa mara moja.
4.HIZI NI SABABU ZA KISHERIA ZA KUMUONDOA MSIMAMIZI WA
MIRATHI .
( a ) Ikiwa kuteuliwa kwake kulikuwa kwa mashaka labda
kikao cha familia kilichomteua
hakikuwa chenye kueleweka pengine
kilifanywa kwa siri na wanafamilia wengine au warithi walipigwa chenga na hivyo hawakuhdhuria. Hii itakuwa ni sababu ya kumuondoa. Pia kasoro yoyote katika mchakato
wa kupatikana kwa msimamizi wa mirathi
ni sababu inayoweza kumuondoa.
( b ) Ikiwa msimamizi
wa mirathi atatumia vibaya
mali za marehemu itakuwa
ni sababu ya kumuondoa. Hili linaeleweka.
( c ) Ikiwa msimamizi wa mirathi
anatumia mali za marehemu kujinufaisha kwa mfano anazifanyia biashara ambayo yeye ndio
mpata faida ni sababu ya kumuondoa.
( d ) Ikiwa anasababisha
uharibifu wa aina yoyote katika mali za marehemu ni sababu
ya kumuondoa.
( e ) Ikiwa msimamizi wa
mirathi kwa makusudi ameshindwa kuleta orodha ya mali za marehemu na taarifa ya jinsi alivyozishughulikia. Wapo wasimamizi
ambao hupenda kuwa wasiri wakati wa kushughulikia mali za marehemu. Hili si
sawa lazima wenye maslahi wapate taarifa
za mara kwa mara za namna msimamizi anavyoshughulikia mali za marehemu laa sivyo wamwondoe kwasababu hiyo.
MWANDISHI
WA MAKALA HAYA
NI MWANASHERIA NA
MSHAURI WA SHERIA
KUPITIA GAZETI LA
SERIKALI LA HABARI
LEO KILA JUMANNE
, GAZETI JAMHURI KILA
JUMANNE NA GAZETI
NIPASHE KILA JUMATANO. PIA NI KATI YA WANASHERIA WAANZILISHI WA BLOG HII.
0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment