Thursday, 12 February 2015

KISHERIA, MAHUSIANO KATI YA MME NA MKE KWA MIAKA MIWILI NI NDOA

Image result for MAHUSIANO
NA   BASHIR   YAKUB-
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, zipo aina nyingi za ndoa. Pamoja na kuwa na aina nyingi za ndoa, ndoa hizi tunaweza kuzigawa katika makundi makuu mawili. Kwanza, ndoa za serikali(civil marriage) na Pili ni ndoa za kimila(customary marriage).
Ndoa za serikali ni zile ndoa zinazofungwa kwa mkuu wa Wilaya, Msajili wa ndoa pamoja na katika Ofisi nyingine za serikali kama Ubalozini n.k.
Ndoa za kimila ni zile ndoa zinazofungwa kulingana na taratibu za kabila la wahusika; kwa mfano ndoa za wahaya, wachaga, ndoa za wazaramo na ndoa nyingine zitokanazo na makabila mbalimbali. Ndoa za kidini pia zinaingia katika kundi hili la ndoa za kimila. Ndoa za kidini ni zile zinazofungwa kutokana  na imani ya dini za wahusika. Katika ndoa za dini kuna ndoa za kiislamu, kuna ndoa za kikiristo, ndoa za kibudha na dini nyingine nyingi wanazo ndoa zao. Mbali na aina hizo za ndoa nilizotaja hapo juu ipo aina nyingine ya ndoa ambayo kwa masikio ya wengi yaweza kuwa ngeni kwa wasomaji wetu  hapa.

Aina hii ya ndoa inapatikana katika kifungu cha 160 kifungu kidogo cha kwanza katika Sheria ya Ndoa. Kifungu hiki kinasema kuwa “Itakapothibitika kuwa mwanaume au mwanamke wameishi wote kwa miaka miwili au zaidi  katika hali ambayo maisha yao yamekuwa kama mume na mke, litajengwa wazo au dhana (presumption) kuwa watu hao wameoana.” 
Maana yake ni kuwa  mwanaume na mwanamke wakiishi wote kwa kipindi cha miaka miwili au zaidi bila kufunga ndoa, kwa mujibu wa sheria watu hao watahesabika kama watu waliooana  hata kama watu hao hawakufunga ndoa kanisani, msikitini au  serikalini.
Ni kwa ufupi sana tunaweza kusema kuwa wachumba au wapenzi wanaoishi kama mke na mume kwa kipindi cha miaka miwili au zaidi, hao wanahesabika kuwa wameoana na sheria inawalinda sawa kabisa na inavyomlinda mke na mume waliofunga ndoa ya kawaida.
Ina maana hata haki zote wanazokuwa nazo watu waliooana kwa ndoa za kawaida hata hawa walioishi wote kwa muda wa miaka miwili na zaidi watakuwa nazo. Wana haki ya kuitana mke na mume, wana haki ya kushiriki nyumba pamoja na mali nyingine, wana haki ya kugawana mali wakiamua kufanya hivyo au uhusiano wao ukivunjika, wana haki kushiriki tendo la ndoa bila kuwekeana vikwazo, wana haki pia ya kupata watoto wakiamua kufanya hivyo.
Mwanamke ana haki ya kutumia jina la mme wake  na wana haki pia ya kufunguliana mashauri ya madai kwa makosa yanayoanzishwa na Sheria ya Ndoa pamoja na Sheria nyinginezo zinazotawala masuala ya ndoa.
Izingatiwe kuwa sheria inaposema ‘kuishi wote miaka miwili’ haimaanishi kuwa unahesabu miaka miwili tangu mwanzo wa mahusiano yenu halafu unasema kuwa kwa mujibu wa sharia hii tayari kuna ndoa. Kuishi wote miaka miwili au zaidi kunakoongelewa hapa ni kule ambako ni kwa mwendelezo. Yaani tangu mmeanza kuishi wote hakuna wakati wowote mrefu ambao mlishawahi kutengana au kuachana. Mnaweza mkawa mlikuwa mnatengana lakini kutengana huko kusiwe kulikuwa ni kwa muda mrefu. Kwa mfano kama mtu na mchumba wake wameanza kuishi wote mwaka 2000 hadi 2002 bila kuwa na muda mrefu wa kutengana katikati, itahesabika kuwa tayari kuna ndoa.
Lakini wawili hawa kama wameanza kuishi wote mwaka 2000 hadi 2002 halafu ikatokea kuwa mwaka 2001 hawakuwa wote  na ikatokea wakarudiana mwaka 2002, haiwezi kuhesabika kuwa wamefikisha miaka miwili na hivyo mahusiano yao kuitwa ndoa kisheria.
 Hii ni kwa kuwa kuna muda mrefu katikati ambao hawakuwa wote. Ingeendelea kuhesabika kwamba kuna ndoa baada ya kufika mwaka 2002 kama kipindi chao cha kuachana katikati kilikuwa kifupi labda mwezi mmoja,miezi miwili, au wiki mbili.  Kwa ufupi sana ieleweke kuwa wakati unahesabu miaka miwili hakikisha katikati hakuna kipindi kirefu mlicho tengana na hivyo kupunguza miaka hiyo.
Napenda tujue kuwa miaka hiyo yote miwili  mliyoishi wote inapaswa kuthibitishwa mbele ya mahakama. Kushindwa kuthibitisha uhusiano wenu wa miaka miwili kunaweza kuifanya mahakama isitambue uhusiano wenu kama ndoa. Lakini hata kama mahakama ikishindwa kutambua uhusiano wenu kama ndoa  na hivyo kuuvunja, kama kuna watoto ambao walikwisha patikana katika mahusiano hayo watoto hao itabidi watolewe matumizi na mwanamke atastahili matunzo.
Pia mahakama itaangalia nani wa kukaa na watoto hao kama itakuwa imeamua kuwatenganisha  kwa muda wenza hao au kama itakuwa imeamua  kuwatenganisha moja kwa moja. Wanachopaswa kuzingatia watu hapa ni kuwa isitokee watu kukaa wote kwa kipindi nilichotaja hapo juu halafu baadae mmoja akaachwa bila hata kupewa lolote kama stahili zake za ndoa.
Jambo hili lina umuhimu hasa katika kipindi hiki ambapo watu hukaa wote kwa muda mrefu bila ya ndoa ya msikitini au kanisani. Kutokana na hali hii ambayo kwa sasa imekuwa kama mtindo(fashion) nisisitize tena kuwa unapokaa na mtu kwa muda huo  halafu ikatokea mkawa mmeachana, wewe uliyeachwa au kuacha unastahili haki zote kutoka kwa mtu huyo kwa mfano  kugawana mali kama zipo, kupewa gharama za kutunza mtoto au watoto kama wapo na haki nyingine zote sawa na mtu aliyekuwa amefunga ndoa ya kidini au ya serikali.
MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO.    PIA  NI  KATI   YA  WANASHERIA  WAANZILISHI   WA   BLOG  HII  0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com




0 comments:

Post a Comment