Tuesday 3 February 2015

WE NI MJASIRIAMALI, UNATAKA KUFUNGUA SHULE, UTARATIBU MWEPESI NI HUU.


NA  BASHIR  YAKUB---.

Wapo Watanzania ambao ndoto zao ni kumiliki shule. Ninapoongelea shule simaanishi lazima  yawe yale mashule makubwa. Hata shule za awali ambazo zinaanzishwa na wajasiriamali wadogo mitaani nazo ni shule kwa  maana hii katika makala haya.
Nyaraka kuu inayoongoza  taratibu za usajili wa shule binafsi huitwa fomu namba RS8. Huu ndio mwongozo mkuu wa usajili. Kuna mambo ya msingi na ya kisheria ambayo  mtu hutakiwa kujiandaa nayo iwapo  anataka kuanzisha shule binafsi.Mambo haya huwa yanakamilishwa kwa wepesi na bila usumbufu  ikiwa yanapitia kwa wanasheria lakini pia mtu anaweza kufanya mwenyewe isipokuwa  hata   akifanya mwenyewe kuna document  za lazima ambazo lazima zisainiwe na kuthibitishwa na mwanasheria.

1.           USHAURI  MUHIMU  KWA WALIO/WANAOTAKA KUANZISHA  SHULE.

Kwanza kabisa kabla ya lolote ni muhimu kujua shule yako itamilikiwa  namna ipi  kisheria. Utaimiliki  binafsi wewe kama wewe, utaunda kampuni halafu kampuni ndo imiliki shule, au utaweka chini ya taasisi  fulani. Kila kimoja katika haya kina faida zake  halikadhalika hasara zake. Pamoja na hayo faida na hasara hizo zinazidiana viwango. Katika  baadhi ya makala zilizopita  niliwahi kuzungumza umuhimu na faida za kitaalam za  kufanya biashara chini ya kampuni.Kwa  ushauri wangu wa kitaalam hasa katika masuala ya  makampuni  nashauri kuwa ni vema sana  ukianzisha mradi wa shule fungua na kampuni ili shule iwe chini ya kampuni. Zipo faida nyingi sana  utazipata  kupitia kufanya hivyo. Hata wenye mtaji mdogo hasa ndugu zangu wanaoanzisha nursery mitaani fungua kampuni na nursery yako iweke chini ya kampuni  halafu utaona matokeo yake baada ya muda.Kufungua kampuni ni bei ndogo sana  na rahisi mno hivyo si jambo la kumuogofya mtu.

2.           MAOMBI  YA   USAJILI  WA SHULE  HUPELEKWA  WAPI.

Maombi ya usajili wa  huelekezwa kwa kamishna mkuu  wa Elimu. Ofisi ya kamishna mkuu wa elimu Tanzania iko Dar es Salaam. Hata hivyo  nakala ya maombi hayo hupelekwa kwa mkaguzi mkuu wa elimu wa kanda husika. Kanda husika ni kanda ambayo  itaanzishwa shule husika. Mkaguzi wa kanda ndiye  hujushughulikia karibia mambo yote ya msingi kuhusu usajili wa shule.

3.           MAMBO  MUHIMU  UNAYOTAKIWA  KUJIANDAA   NAYO.

Kila biashara  huwa ina maandalizi  yake  kabla ya kuanza kwake. Shule binafsi nayo kama biashara nyingine yoyote inayo mambo ya  msingi na ya kisheria ambayo  mtu anatakiwa kuyazingatia  kabla ya kuanzisha  biashara hii.Mambo haya pia ndiyo hayohayo utayotakiwa kuyajaza  kwenye fomu maalum ya  kuombea usajili wa shule yako.

( a ) Jina la shule. Lazima kwanza ujue shule yako itaitwaje.Huwezi kufanya mipango ya shule bila jina. Pia  jina  hutakiwa  kujazwa kwenye fomu maalum ya kuombea usajili.    

( b ) Lazima ujue unataka kuanzisha shule ya aina gani. Shule ziko aina nyingi, unataka shule  ya awali(nursery),shule ya msingi,sekondari ya form iv au v & vi. Pia ujue iwapo shule hiyo itakuwa kutwa au ya kulala, ya wasichana na wavulana au wavulana tu au wasichana tu. Kama shule yako ni sekondari lazima ujue itakuwa inashughulika na michepuo ipi  sanaa, biashara,kilimo, sayansi, elimu ya ufundi au kitu gani.Haya lazima ujiandae nayo na  uyajue.Pia taarifa hizi huwa  zinahitajika unapokuwa unajaza  fomu ya usajili hivyo ni muhmu kuziandaa.

( c ) Jambo jingine ni tarehe au kipindi ambacho shule inatarajiwa kufunguliwa. Taarifa hii hutakiwa kwasababu mamlaka za usajili zinajenga dhana(assume) kuwa mtu anapoamua kujaza fomu ya usajili  basi huwa yuko tayari kuanzisha shule na hivyo lazima awe  na tarehe ambayo shule yake itaanza.Hivyo lazima uandae tarehe kama una mpango huu.

( d ) Pia huwezi kuanzisha shule bila kuwa na  Meneja wa Shule. Sheria inataka kabla ya usajili lazima awepo meneja na atajwe katika fomu ya usajili.

( e ) Anuani kamili ya mahali ambapo shule inakusudiwa kufunguliwa ni jambo jingine linalopaswa kufafanuliwa kupitia fomu hii. Anuani hapa si tu P.O BOX………  hapana. Unataja mtaa,kitongoji,kata,wilaya, na mkoa. Hii ndio anuani.

( f ) Pia uandae hati ya Umiliki wa Ardhi au Mkataba wa Pango wa eneo ambalo shule itafunguliwa.

( g ) Utatakiwa kuonyesha sifa na idadi ya walimu watakaoajiriwa, uwiano wa walimu na wanafunzi kwa maana ya wastani wa mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi wangapi (Teacher-Students ratio)

( h ) Utatakiwa kueleza vifaa vitakavyokuwa shuleni na pia kuonyesha kiwango cha juu zaidi (maximum) cha wanafunzi wanaoweza kusoma kwa wakati mmoja katika shule itakayofunguliwa.

( I )  Kutaja  kiwango cha ada unachokusudia kuwatoza wanafunzi wa shule hiyo, huku ukipambanua pia tozo nyinginezo kama vile gharama za bweni na aina ya vifaa ambavyo wanafunzi wenyewe wanapaswa kuja navyo shuleni.

4.           VIAMBATANISHO MUHIMU.

Vimbatanisho muhimu vya kuandaa ni Hati za Idhini za matumizi ya Ardhi chini ya taratibu za mipango miji kutoka mamlaka husika hasa manispaa, Mhandisi wa Wilaya au Mji, serikali za vijiji, na kadhalika.
Cheti kutoka kwa bwana afya kuthibitisha kwamba eneo litakalotumika kwa ya ajili ya shule  linakidhi vigezo vya afya na usalama wa wanafunzi, pia ambatanisha taarifa za wafanyakazi wasio walimu,na nakala ya ramani ya majengo.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO. PIA NI MKURUGENZIU WA BLOG HII   0784482959,        0714047241              bashiryakub@ymail.com






7 comments:

  • JULIUS AKILI says:
    12 November 2020 at 12:46

    nimekuelewa

  • Unknown says:
    22 December 2020 at 08:11

    Asante sana

  • Shaitu Hassan says:
    24 January 2021 at 11:17

    Ahsante sana unatutia hamasa vijana!! Mungu akutie nguvu!

  • Shaitu Hassan says:
    24 January 2021 at 11:20

    Ahsante sana unatutia hamasa vijana!! Mungu akutie nguvu!

  • Unknown says:
    15 July 2021 at 00:04

    Thanks alot

  • Unknown says:
    1 September 2021 at 13:18

    Blessed

  • Unknown says:
    26 January 2022 at 18:19

    Asante.mimi nipo katika hatua za mwisho za kuandaa mazingira ya shule daycare madarasa (vyumba 9)maeneo ya kinyerezi msikitini/bonyokwa stendi ilala.mwenye uzoefu umeneja anitafute 0717789992

Post a Comment