Sunday, 25 January 2015

JIFUNZE NAMNA YA KUANDIKA MKATABA KISHERIA UNAPOUZA AU KUNUNUA


NA  BASHIR  YAKUB----

Katika shughuli zetu za kuuza na kununua  ambazo tunazifanya kila siku mikataba ya maandishi  ni jambo ambalo wengi tunakutana nalo. Mikataba hii iwe rasmi au isiwe rasmi suala la msingi ni kuwa  huwa tunaifanya. Aidha wakati mwingine si  wote wenye kuhusisha suala la mikataba ya maandishi  katika makubaliano yaombalimbali  na hii hutokana na  sababu mbalimbali ikiwemo ya kuaminiana. Kuhusu kuaminiana niseme jambo moja tu kuwa suala la mikataba ni muhimu sana  hata kana  mwenzako unamuamini kwa kiwango cha juu kabisa( highest degree of trust). 

Nathubutu kusema kuwa hata awe mzazi wako kama kuna jambo la msingi mmelifanya  ni vema kukawapo mkataba wa maandishi.  Nasema hivi kwakuwa kwa uzoefu wangu wa mambo haya  mara nyingi mgogoro hautokani na waliouziana  au kukubaliana isipokuwa mgogoro unakuja kuanzishwa na walio nyuma ya hao.  
Kwa mfano baba anaweza kumpa mwanae kiwanja   na wasifanye  mkataba wowote wa maandishi kwa kuwa wanaaminiana.  Hiyo ikaenda kwa miaka kadhaa ambapo baba akawa amefariki. Baaada ya hapo anaibuka mtu anasema mimi  ni mtoto wa  marehemu kwa hiyo nahitaji  kiasi kadhaa kutoka mali hii. 
Hapa mgogoro si kati ya baba na mwana tena   isipokuwa ni kati ya mwana na mtu mwingine. Kama huna mkataba wowote wa maandishi  mpaka kesi hii kuisha waweza kuwa umepoteza kila kitu. Huu ni mfano tu katika kusisitiza kuwa mtu asiseme mi na  fulani tunaaminiana. Mgogoro sio lazima utokane na nyie wawili  isipokuwa walio nyuma yenu waweza kuanzisha mgogoro.

1.  MADHARA   YA   KUTOFANYA  MKATABA  WA  KISHERIA .
Ni vema sana kujihadhari kwakuwa ukisikia neno  mgogoro ujue kuna mambo makubwa mawili. Kwanza gharama kubwa ni uwezekano wa kupoteza kabisa ile mali na haijalishi iwe uliinunua au ulipewa isipokuwa tu ukishakuwa na mgogoro upo katika hatari hiyo. Pia gharama ya pesa  kama kuwalipa wanasheria, gharama za uendeshaji kesi,  nauli  na matumizi mengineyo ambayo hujitokeza bila hata kutarajia. Pili kuna  gharama ya muda . 

Hii  huhusisha  kushinda mahakamani kila siku  na wote mwajua  mahakama zetu  zilivyo, kushinda vituo vya polisi huku shughuli zako za msingi za kila siku zikisimama. Pia hapa  kuna muda wa  kusubiri hukumu ambapo kesi yaweza kukaa mahakamani hata miaka  sita . Hakika unakuwa umesurubika(suffer) na  umepoteza mambo mengi katika kushughulikia jambo hili.

2.  USHAURI.
Ushauri wa kawaida tu kwa hili ni  kuwa na utamaduni wa kuweka katika maandishi kila  makubaliano  na hii iwe kwa watu wote mnayeaminiana sana au msiyeaminiana. Fanya hili kuwa utamaduni wako kwa kuweka kila muamala wako katika maandishi suala la kuaminiani lisiwe hoja tena kwakuwa mgogoro hautakuwa kati yako na yeye isipokuwa unaweza kuwa kati ya mtu wa nyuma yake na wewe au mtu wa nyuma yako na         yeye. Nitatoa mfano mwingine halisi  ambapo mfano huu ni kesi ipo mahakamani hadi leo. 

Mwaka  2010 mwezi wa saba mtu mmoja alimuuzia rafiki yake gari aina ya land cruiser akiwa anatafuta fedha kwa ajili ya safari yake ya uingereza baada ya kupata kazi huko. Wakauziana na kwakuwa waliaminiana sana hawakuandikishana popote. 

Mwaka mmoja na nusu baadae  gari hiyo ikakamatwa maeneo ya Sinza na polisi  kwasababu  kuwa mwaka 2009 Disemba iliwagonga watu wawili na kuuwa mmoja maeneo ya tabata na kukimbia. Mnunuzi alijitetea kwa urahisi tu kuwa gari amelipata 2010 July kwa hiyo hawezi kuwa anahusika na lolote kabla ya muda huo. 
Utetezi wake ulikubaliwa  isipokuwa tu alitakiwa atihibitishe kwa kuonesha  mkataba halali wa mauziano ambao utaonesha kuwa  ameanza kumiliki gari hilo  baada ya ajali. Ilikuwa  vigumu  kwake  na hilo  likamwingiza moja kwa moja katika  kesi hiyo na mpaka naandika makala haya amesota na kesi hiyo kwa miaka minne sasa na haijajulikana inaisha lini ambapo kwa mtazamo wa kitaalam kuna uwezekano mkubwa wa kupatikana na hatia na kwenda jela.Kwa hiyo utaona hapa kuwa kufanya maandiko ya kisheria katika kila muamala si muhimu tu katika  kudhulumiana  bali pia hata mambo mengine kama haya ambayo   yanaweza kujitokeza bila kutarajia.


3.  JE  KILA  MAANDISHI  NI  MKATABA.
Aidha uandishi mzuri wa mkataba wa kisheria  hupelekea mkataba wenye hadhi na mkataba wenye hadhi ndio mkataba halali ambao hukubalika kisheria  na pia huweza kutumika kama ushahidi endapo kuna tatizo. Yawezekana unao mkataba lakini hauna hadhi kisheria na likijitokeza jambo mkataba wako hautakubalika. Si kila maandishi ni mkataba isipokuwa mkataba  huwa na vitu maalum vya kisheria ambavyo huufanya kukubalika na kutambuliwa. Haya hapa ndio mambo ya msingi ambayo  hutakiwa kuwa ndani ya mkataba.


 4.  MKATABA  MZURI  HUWA  NA  HAYA :
( a ) Lazima uwe na majina ya wahusika ambayo yatakuwa yameandikwa kwa urefu  na kwa kueleweka.Mfano jina liwe Paschal Mayenge Archard. Epuka kuandika vifupi  mfano P.M. Archard. Jina linatakiwa liwe katika ukamilifu wake na hasa pawe na majina matatu kamili. Pia majina  ya pande zote mbili yaani muuzaji na mnunuzi yatokee hivyohiyvo  si tu majina ya upande mmoja. Yawezekana mkataba mwingine unahusisha watu wengi zaidi  pia ni muhimu  majina matatu ya kila mmoja yaonekane hata kama  wako ishirini.

( b ) Katika majina hayo hadhi ya kila mmoja iainishwe mbele ya jina lake. Mfano kama ni muuzaji  au mnunuzi mbele iandikwe kuwa huyu ni muuzaji na huyu ni mnunuzi. Halikadhalika kama ni mkopaji, mkopeshwaji, mtoa zawadi mpokea zawadi viainishwe.

(  c  )  Bei au gharama halisi ya mauziano ioneshwe. Iandikwe kwa tarakimu yaani namba mfano 1,000,000/= na kwa maneno katika mabano ( Milioni moja tu).Ni muhimu yote mawili yaonekane , hii huondoa utata.Tarehe ya mkataba ioneshwe sambamba  na maelezokama fedha imelipwa yote au kiasi.

( d ) Kama kuna kiasi kilichobaki kianishwe kwa tarakimu na pia kwa maneno  kama nilivyoonesha hapo juu. Muda wa kulipa kilichobaki nao uainishwe ikiwa ni pamoja na hatua za kuchukua ikiwa muda uliowekwa utapita. Mkataba  lazima uoneshe muda ukipita  nini kifanyike mfano ikifika tarehe 7. 12. 2015 saa kumi jioni kiasi cha pesa iliyobaki hakijalipwa basi mali itamrudia mwenye nayo na mnunuzi hatakuwa na deni lolote dhidi ya muuzaji, au itahesabika kuwa mkataba umevunjika  na  mnunuzi atatakiwa kumlipa fidia ya kiasi fulani muuzaji kwa kuvunja mkataba.

( e  ) Mashahidi ni muhimu kila upande. Kila upande hata ukiwa na shahidi mmoja wala si mbaya. Shahidi awe mtu wa kuaminika , mtu mzima na mwenye akili timamu. Wataandika majina yao matatu kwa urefu kama yalivyo  ya wahusika  na pia wataweka sahihi zao huku  ikioneshwa shahidi yupi wa upande upi na yupi wa upande upi. Wakili ni mtu muhimu sana kwa wakati huu kwani  wakili anaweza kuwa shahidi pekee bila kuwapo shahidi mwingine yeyote. 
Wakili  anakuwa shahidi wa  wote wawili na panakuwa hapahitajiki mwingine yeyote.Pia wakili ni shahidi wa kuaminika  zaidi na anaaminiwa na kila mamlaka ikiwemo mahakama na hivyo uwepo wake katika mkataba  ni ulinzi tosha kwa mkataba wako.

(  f  ) Mali inayouzwa au iliyohusishwa kwenye mkataba ichambuliwe vyema. Kama ni kiwanja au nyumba ielezwe mtaa, kata, tarafa kitongoji,mkoa,plot namba kama ipo, urefu, upana, ikiwezekana  jirani wa kushoto na kulia.au magharibi, mashariki,  na kama ni gari, pikipiki maelezo yote yaliyo kwenye kadi yaingie katika mkataba ili kutambua  kwa undani mali yenyewe.

( g ) Anuani za muuzaji au mnunuzi  ziwepo ikiwa ni pamoja na namba ya simu. Hili la namba ya simu  ni muhimu sana kwasasa kutokana na msaada mkubwa wa mawasiliano haya endapo mtu atahitajika.

( h ) Picha  ndogo yenye kuonesha taswira ya mtu kwa ukamilifu (passport size) ni  muhimu sana na ibandikwe mbele ya jina la mtu. Si muhimu sana kwa mashahidi lakini  kwa wahusika wenyewe ni muhimu sana.

( I ) Alama ya  dole gumba mbele ya jina nayo ni muhimu sana. Hii ni kutokama na alama hii kutoweza kwa namna yoyote kuingiliwa au kughushiwa.Tia dole kwenye kablasha ya muhuri na weka dole gumba mbele ya kila jina. Hii pia si lazima kwa mashahidi.

( j ) Kama ni kiwanja au nyumba ni muhimu mkataba uoneshe kama kimelipiwa kodi ya ardhi ( Land rent) na kama hakijalipiwa mkataba ueleze nani atalipa kodi hiyo kati ya anayenunua au anayeuza.

( k ) Pia ni muhimu sana mkataba uoneshe iwapo mgogoro wowote utatokea kuhusiana na mkataba huo nini wahusika wafanye, mfano endapo mgogoro utatokea kuhusiana na mkataba huu mahakama ya Tanzania yenye mamlaka  ndio itahusika na utatuzi wa mgogoro. Sambamba na hilo  mkataba uweke wajibu  kwa muuzaji kuwa tayari kumpa ushirikiano   mnunuzi iwapo mali aliyomuuzia itaonekana kuwa na mgogoro mbeleni mfano muuzaji atampa ushirikiano mnunuzi endapo kutatokea mgogoro wowote kuhusiana na mauziano haya.

Kwa ufupi hayo ni baadhi  tu ya mambo ya msingi katika kukufanya kuwa salama katika mikataba. Nirudie tu kusema kuwa  si kila maandishi uliyoandika na kuhifadhi nyumbani kwako ni mkataba jitahidi kuwa na mkataba wa kisheria.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO. PIA  NDIYE MWANZILISHI  NA  MKURUGENZI   WA  BLOG HII.    
0784482959,        
 0714047241,         
bashiryakub@ymail.com0 comments:

Post a Comment