Sunday, 25 January 2015

MNUNUZI WA NYUMBA/KIWANJA JIHADHARI SERIKALI ZA MITAA HAWARUHUSIWI KUSIMAMIA MIKATABA KISHERIA.







NA   BASHIR     YAKUB----

Wiki  iliyopita  niliandika  kuhusu  Asilimia kumi ambayo  serikali  za mitaa huwa  wanaidai  hasa  maeneo  ya  mijini baada  ya  wahusika  kuwa wameuziana nyumba au  kiwanja. Nikasema  wazi  kabisa  bila  kungata  meno  kuwa  hiyo  pesa iitwayo asilimia kumi au pesa nyingine yoyote   mtu  atakayolipa  serikali  za  mitaa eti  kwakuwa amenunua  au  ameuza

eneo  lake   ni rushwa. Na  leo   nakumbusha na  kusisitiza  tena   kuwa  Watanzana wajue ukitoa   pesa  ile   umetoa  rushwa  na huyo  kiongozi  wa  serikali   za   mitaa uliyempa amepokea rushwa  kwakuwa  malipo  hayo  hayatambuliwi  na hayaainishwi  na sheria  yoyote. Lazima ifike   hatua  haya  mambo yaeleweke.   Pia  nimetahadharisha mara nyingi kuhusu  umakini unaponunua  kiwanja/nyumba  na kueleza baadhi ya mambo  ambayo  ukiyafanya utakuwa umefanya manunuzi salama na utakuwa umeepuka migogoro na hata mgogoro ukitokea wewe hautapoteza. Anayetaka kusoma  haya  yaliyopita aandike neno  MAKALA  SHERIA  kwenye google ataona makala  hizo. Leo tena  naeleza uhalali kisheria wa serikali za mitaa kusimamia mikataba.

(  a  )  KISHERIA   HAIRUHUSIWI   SERIKALI  ZA  MITAA   KUSIMAMIA   MAUZO  YA NYUMBA/KIWANJA.

Kwanza  nataka  nieleweke  wazi  kuwa nazungumzia  sana   ununuzi wa nyumba /viwanja   kwa  kuona  huruma  jinsi  watu wanavyopoteza  umiliki  wa maeneo  yao waliyonunua kwa kuamini wameyanunua  kihalali  kumbe  kuna  nukta  walizokosea  katika taratibu  za  kimanunuzi  na  sasa zinawagharimu. Ninayosema  hapo yanatokea  karibia  kila siku mahakamani. Watu wanalia  lakini mda  huo huna  wa  kumlilia.Nianze hivi  kisheria Wakili ndio  mtu  ambaye anaruhusiwa kusimamia  mkataba  . Wakili ana vyeo vitatu, kwanza  ni wakili, pili mthibitishaji wa umma ( notary  public)  tatu  ni afisa  wa viapo. Uwakili nao ni cheo katika vyeo alivyonavyo  wakili. Vyeo  viwili yaani uwakili na uthibitishaji  wa umma ndivyo humpa  mamlaka  ya kusimamia mikataba.  Hapa  naongelea nyumba/viwanja lakini kimsingi  vyeo hivi si tu humpa mamlaka ya kusimamia mikataba  ya  viwanja/nyumba  lakini  pia mikataba  yote. Hakuna  katka nchi hii sheria  yoyote  ambayo  imemruhusu kiongozi   wa  serikali  za  mitaa  kusimamia mkataba, uwe wa nyumba, mkopo au wowote ule hata  wa  mauzo  ya  baiskeli. Kama hakuna sheria hiyo maana yake  ni kuwa kusimamia mikataba  si  kazi yao. Kwa maana hii hii narudia  kusema na  kusistiza kuwa hairuhusiwi  serikali  za  mitaa  kusimamia  mauzo  ya  nyumba/kiwanja.

(  b  )  MKATABA   WANGU  WA   MANUNUZI  YA  NYUMBA/KIWANJA  UMESIMAMIWA  NA   SERIKALI   ZA   MITAA   JE  UNA HADHI   GANI?.

Kama  ndani kwako una mkataba wa manunuzi  ya nyumba/kiwanja  ambao ulisimamiwa  na  serikali  za  mitaa   basi  ujue   kuwa  mkataba huo  hadhi yake  ni sawa  na umesimamiwa na   jirani yako , ndugu yako au mtu mwingine yeyote unayemuamini  ambaye  amekusaidia  kukamilisha  mkataba. Tuache  kuishi  kwa  mazoea  hii  ndiyo  hali  halisi  kisheria.  Mkataba  wa  mauzo  ya  nyumba/viwanja au  mkataba  mwingine  wowote  uliofanyika serikali  za   mitaa ni  sawa   na  mkataba  uliofanyika  nyumbani  kwako. Hiyo ndio hadhi au nafasi  ya  mkataba wa aina hiyo kisheria. Kiongozi yeyote wa serikali  za mitaa  anaweza  kuwa shahidi yako ukiamua kumuita  lakini  lazima ujue kuwa  ushahidi wake  katika  mkataba wako  kisheria  ni sawa na ushahidi wa mtu  mwingine  yeyote. Hakuna  eti kwakuwa  huyu  au  hawa ni  serikali  za  mitaa  kwahiyo wakionekana katika mkataba  wangu ndio utakuwa na uzito na  wenye  kuaminika  zaidi,  hapana. Hawa  kama utaamua  kuwashirikisha  maana hata  kuwashirikisha  nayo ni  hiari  yako  wanaweza  kuwa  mashahidi  sawa na  shahidi ndugu yako  au jamaa yako  mwingine  yeyote . Anayeufanya mkataba  kuwa  na  uzito  mbele ya macho  ya  sheria ni  wakili na huyu ndiye aliyepewa  kazi hii.  Kwa hiyo wanunuzi  wa  viwanja/nyumba  jihadharini  kwakuwa   serikali za mitaa kisheria  hilo si  jukumu lao. Wanayo  majukumu yao  lakini hili si  miongoni mwa hayo.  Watu  wasifanyiwe  utapeli serikali haisimamii mikataba ya watu binafsi. Kama  serikali  kuu  haiwezi kusimamia  mkataba  kati Bakhresa  na  Mohammed enterprise   hata  serikali  za  mitaa  hawezi  kusimamia  mkataba kati  yangu  na  wewe. Nawatahadharisha zaidi   wanunuzi  kwakuwa  upande  wa ununuzi  ndio upande  wa  kupoteza linapotokea  tatizo.

(  c  )  USHAURI     KWA    WANUNUZI     WA  NYUMBA/VIWANJA.

Kama unataka kununua nyumba/kiwanja  na  unataka  mkataba   wako  wa manunuzi  uwe  na nguvu na hadhi  ya usimamizi  wa  kisheria  basi  epuka  kuwatumia serikali za mitaa kufanya jambo  hili. Serikali  za  mitaa  wanajua vyema  kuwa  kusimamia mikataba ya kuuza na kunuua si  katika majukumu  yao isipokuwa kwakuwa  hapa  ndipo penye  hela  kuliko   hata  hizo  posho zao wanazopewa na serikali kuu basi hawako  tayari  kulisema  hili  kwa  mtu  yeyote.   Hili utakuja  kulijua  vyema ukishapata mgogoro wakati  wao hawapo  tena   wameshaondoka  na   chao. Mikataba  ya   serikali  za  mitaa  haina hadhi   na  wanasheria    wanaichallenge sana  mahakamani  wakati  wa  migogoro  kiasi  cha  kuonekana  kama  vile pengine hukufanya mkataba  kabisa. Migogoro  ya  nyumba  na viwanja ni mingi mno  lakini   wewe unaweza kuiepuka  migogoro hiyo  ikiwa utazingatia   ushauri  wa kitaalam  na   utaepuka   kukurupuka  unapotaka kununua  kiwanja/nyumba.  Leo nilitaka  nikuhadharishe  na  hilo  ndugu mpendwa. 


MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO. PIA  NDIYE MWANZILISHI  NA  MKURUGENZI   WA  BLOG HII.    
0784482959,        
 0714047241,         

bashiryakub@ymail.com

0 comments:

Post a Comment