Thursday 28 July 2022

KWANI MATUNZO YA MTOTO NI SHILINGI NGAPI KWA MWEZI ?.





Na Bashir  Yakub, WAKILI  -

Hakuna kiwango maalum cha kutoa kwa mzazi mwenza kama matunzo ya mtoto.

Kuna wengine hulazimisha wapewe Tshs 150,000/ kwa mwezi, wengine 50 elfu kwa mwezi, wengine hutaka mpaka Laki tano kwa mwezi nk, nk, nk.

Narudia hakuna kiwango maalum bali unaweza kutoa kiwango chochote kulingana na vigezo maalum ambavyo huzingatiwa.

Kifungu cha 44 cha Sheria ya Mtoto, pamoja na Kanuni ya 84(2) ya Kanuni za Sheria ya Mtoto vimeainisha Vigezo ambavyo huzingatiwa ili kujua utoe kiasi gani cha matunzo.

Vigezo(factors) hivyo ni Mali na Kipato chako.  Mali na Kipato ni pamoja na mshahara na posho unazopata, pato kutoka biashara/shughuli zako, pensheni na kiinua mgongo,  pato kutoka kwenye kodi za nyumba, frem,  mashamba, mifugo, nk. 

Vitu hivi hata ukifikishwa mahakamani kwa suala la matunzo ya mtoto ndo vitu vitazingatiwa ili kujua itolewe amri ya kuwa unalipa kiasi gani.

Kwa hiyo hakuna haja ya kulazimishana kuhusu kiwango. Na Kifungu cha 49 Sheria hiyo ya Mtoto kinaruhusu kiwango unachotoa kupungua ama kuongezeka ikiwa kipato chako kitashuka ama kupanda.

Ni muhimu sasa kujua kuwa hakuna kiwango maalum cha kutoa kwa mzazi mwenza au penginepo kama matunzo ya mtoto.


0 comments:

Post a Comment