NA BASHIR YAKUB -
Hasara yoyote ambayo mtu atakusababishia yafaa akufidie
isipokuwa kama umeamua kusamehe, au kama
ilitokana na mchakato ambao haukuwa
halali kisheria. Katika ufafanuzi makala yatajikita katika Sura ya 345, Sheria
ya Mikataba ambayo kimsingi ndiyo inayoongelea jambo hili.
Tutaliangalia hili kwa ujumla wake kupitia mafungu matatu,
kwanza KUKATAA KUFIDIWA, pili KUKUBALI KUFIDIWA, na tatu MAMBO YANATOTAKIWA
WAKATI WA KUFIDIWA.
1.KUKATAA KUKUFIDIA.
Yumkini yule aliyesababisha hasara anaweza kukataa kukulipa
au kufidia kile alichosababisha. Ikiwa hili litatokea basi yafaa umwandikie
taarifa ya kumtaka kukufidia mara moja. Taarifa hii inapendeza zaidi akiandikwa
na Wakili na kwa anuani yake Wakili. Hata hivyo hata wewe mwenyewe waweza
kuandika.
Taarifa itakuwa ikieleza kile alichotenda, hasara
iliyosababishwa na hilo tendo lake, kumtaka afidie hiyo hasara, siku au muda ambao unampa afidie hiyo hasara,na nini utafanya ikiwa
atashindwa kufidia hiyo hasara ndani ya muda uliompa.
Kawaida unaweza kumpa siku 7, siku 14, siku 30 , siku 45, au muda
wowote kadri unavyoona unafaa na kutosha. Na utaeleza pia kitu
ambacho utafanya/hatua utakazochukua ikiwa atashindwa kukulipa. Na kawaida kitu
cha kufanya huwa ni kumfikisha mahakamani
mhusika. Usije ukamdhuru, au kingine chochote ambacho hakimo katika utawala wa
sheria.
Basi, ikiwa kweli muda huo umeisha na huyo mtu hajakufidia au
kukuita katika mazungumzo basi yafaa sasa kumfikisha mahakamani. Kumfikisha
mahakamani ni kumlazimisha kufidia hasara aliyoisababisha. Na unapokuwa umemfikisha
mahakamani malipo yanaongezeka kwasababu
na gharama za kesi pia huingia. Hivi
ndivyo unavyoweza kumlazimisha aliyekataa.
2. KUKUBALI KULIPA FIDIA.
Kukubali kupo aina mbili. Kwanza kukubali kwa maandishi kuwa
nimesababisha hasara kwahiyo nitakulipa, na pili kukubali tu kwa mdomo kuwa
nimesababisha hasara hivyo nitakulipa. Kwa mujibu wa kifungu cha 10 cha Sheria
ya Mikataba , makubaliano ya mdomo ambayo hayako katika maandishi nayo ni mkataba
halali kisheria.
Kwahiyo iwe ameahidi kulipa hasara kwa maandishi au kwa mdomo
bado yote ni makubaliano na yanakubalika kisheria. Lakini pia ile ahadi pekee ambayo huyu
aliyesabababisha hasara ataitoa kwa yule aliyemsababishia hasara nayo ni mkataba kamili kisheria. Ahadi tu, yaani
ile kutamka tu kuwa nitakulipa au nitakufidia tayari ule ni mkataba tosha na
yafaa utekelezwe.
3. MAMBO AMBAYO YANATAKIWA KUFIDIWA.
Mambo haya ni kwa mujibu wa kifungu chav 77 cha Sheria ya
Mikataba. Kwanza ni uharibifu wa aina yoyote ikiwa upo. Pili, ni gharama ambazo
umetumia kuanzia unahangaika na huyo mtu mpaka kufikia mnakubaliana, pengine
ulimtafuta, ulifungua kesi, ulitumia nauli, ulipiga simu na kila aina ya
gharama ambayo uliingia anatakiwa kuilipa. Tatu ni malipo mengine ambayo
mtakubaliana, au yalikuwa yamekubaliwa katika ule mchakato wa mwanzo aliouharibu.
Hivi ndivyo unavyoweza kufidiwa hasara.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MWANDISHI
WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI
LA JAMHURI KILA JUMANNE.
0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment