NA BASHIR YAKUB-
Ndoa inapovunjika kuna
kuna mambo makuu matatu ambayo hutokea yakiwa kama matokeo ya ndoa hiyo kuvunjika.
Kwanza ni kugawana mali walizochuma wanandoa , pili hifadhi ya watoto na tatu matunzo ya watoto. Haya ni matokeo
ya kuvunjika kwa ndoa, mengine
zaidi kuhusu kuvunjika kwa ndoa
tutayaona hapa wakati nikieleza mgawanyo wa mali za wanandoa.
1.MALI ZIPI
HUTAKIWA HUGAWANYWA NDOA INAPOVUNJIKA.
Ndoa inapotangazwa kuvunjika mali ambazo hupaswa
kugawanywa ni mali za wanandoa wenyewe. Swali mbele yetu ni kuwa ni zipi mali
za wanandoa. Mali za wanandoa ni zile mali zote zilizochumwa na wanandoa hao
kwa jitihada au juhudi za
pamoja wakati wa ndoa
yao. Mali hizo zaweza kuwa zinahamishika au hazihamishiki. Mali zisozo
hamishika ni kama nyumba, viwanja, mashamba n.k. Mali zinazohamishika ni kama
magari, baiskeli, pikipiki,vifaa vya
ndani kama fenicha, fedha benki, na
mali nyingine ambazo hazionekani kwa macho au hazigusiki kama hisa n.k. Zingatia sana usije kudhulumiwa kwa kuwa hata hisa pamoja na akiba ya fedha benki
nayo ni mali inayostahili kugawanywa.
2. JE MALI ILIYOPATIKANA KABLA YA NDOA HUGAWANYWA.
Mali zilizopatikana kabla ya ndoa haziwezi
kugawanywa ndoa inapovunjika isipokuwa tu
kama zilibadilishwa kuwa za wanandoa wakati wa ndoa. Swali ni zinawezaje kubadilishwa
kuwa za wanandoa. Zinabadilshwa kuwa za wanandoa iwapo wanandoa walikubaliana kwa makubaliano maalum
kuwa mali kadha wa kadha zitakuwa zetu wote. Na hii inaweza kuwa kwa maandishi au kwa
kubadili majina ya nyaraka za umiliki
na kuzifanya kuwa na majina yote
mawili ya wanandoa kutoka la mmoja
la awali. Lakini pia zaweza
kuwa za kwao wote kimatendo, kwa mfano
kabla ya ndoa mmoja wa wanandoa alikuwa na nyumba lakini haijamaliziwa.
Wakati wa ndoa
nyumba hiyo imemaliziwa kwa nguvu zao za pamoja na sasa imekamiliki. Nyumba ile inageuka kuwa
ya wote. Kwa ufupi maendelezo yoyote yanayofanywa
na wanandoa katika mali ambayo
hapo awali kabla ya ndoa ilimilikiwa na
mmoja peke yake
yanaibadilisha mali ile kuwa ya ndoa. Hata
kupaka rangi ni tendo la kuifanya
mali kumilikiwa kwa pamoja na hivyo
kustahili mgao ndoa inapovunjika.
3. MAMA WA NYUMBANI NI LAZIMA KUPATA
MGAO NDOA INAPOVUNJIKA.
Hapo juu wakati naeleza maana ya neno mali za
wanandoa ambazo hustahili mgao ndoa
inapovunjika nilieleza kuwa mali hizo inabidi ziwe zimepatikana kwa nguvu,
juhudi au jitihada au mchango wa pamoja kipindi cha ndoa. Swali ni nini maana nguvu, jitihada, au mchango wa pamoja.
Watu wengi hujua kuwa juhudi au mchango wa pamoja unaopelekea
mali kuwa za wote na hivyo kustashili mgao ndoa inapovunjika ni ile leta ni
lete. Yaani kama ni nyumba inajengwa mume akitoa saruji mwanamke atoe nondo au
mume akitoa hela na mwanamke atoe hela na kama ni gari mwanaume akitoa milioni
kadhaa na mwanamke naye achangie za kwake kadhaa na hapo ndipo itakuwa mali yao
wote na eti hapo ndipo mgao unapostahili. Hiyo ni
maana lakini finyu sana.
Maana ya kisheria
ya mchango au juhudi za pamoja hujumuisha kazi anazofanya mama nyumbani
wakati baba akiwa nje ya nyumba kwa uzalishaji mali. Kuosha vyombo,kupika,usafi
wa nyumbani,kutunza na kuandaa watoto,kufua, na kila kazi ya nyumbani ni mchango
na juhudi ya pamoja kwa maana
niliyosema na lazima ilipwe kwa kugawana
mali ndoa inapovunjika. Kwa maana hii mama wa nyumbani hustahili mgao wa mali
ndoa inapovunjika. Hii ni sheria na
kufanya hivyo ni lazima si hiari wala hisani ya mtu.
4. KWANINI SHERIA IMEAMURU
MGAO WA MALI
KWA MAMA WA
NYUMBANI.
Sheria
inamini kuwa wakati wa ndoa mwanamke huwa ametoa sadaka maisha yake na utu wake katika kuwatunza watoto(kama
wapo) na kuitumikia familia kwa ujumla kwa
kufanya kazi zote za nyumbani kitu ambacho humwekea ugumu
wa kuzalisha pesa na baadhi ya mali zitokanazo na pesa. Sheria inaamini kuwa
hilo hutokana na nafasi yake hiyo ya
kuwa mwangalizi wa nyumba wa muda wote. Hivyo basi haiwezi kuwa busara,hauwezi
kuwa ubinadamu, hauwezi kuwa utu, hauwezi kuwa ustaarabu, haiwezi kuingia
katika akili ya yoyote na haiwezi kamwe kuwa sawa kwa mwanamke kama huyo baada
ya talaka asipate chochote na aondoke bila chochote baada ya kuwa
amepoteza miaka mingi katika kuitumikia familia hiyo. Hii ndiyo sababu kuu
ya kumpa
mgao wa mali mama ambaye
hushinda nyumbani.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA
GAZETI LA SERIKALI
LA HABARI LEO
KILA JUMANNE , GAZETI
JAMHURI KILA JUMANNE
NA GAZETI NIPASHE
KILA JUMATANO. PIA NI KATI YA WANASHERIA WAANZILISHI WA BLOG HII . 0784482959, 0714047241 bashiryakub@ymail.com
0 comments:
Post a Comment