Na
NA BASHIR YAKUB-
Kuomba talaka si dhambi. Kama lingekuwa dhambi
sheria isingeruhusu jambo hilo kwakuwa si kawaida ya sheria kuhamasishi madhambi. Ni kwasababu hii nasema kuwa atakayeona amebanwa
basi aombe talaka. Si kosa hata kidogo kufanya hivyo isipokuwa ndivyo
tunavyoelekezwa na sheria zetu tunazozipenda
na kuziheshimu sana.
1. KUVUNJIKA KWA NDOA.
Kuvunjika kwa ndoa kwa mujibu wa sheria zetu za
Tanzania kuna mazingira mengi. Baadhi ya mazingira hayo ni yale
yaliyoorodheshwa kifungu cha 12 (a-e) cha Sheria ya ndoa ambayo ni pamoja na
kifo cha mmoja wa wanandoa, talaka ambayo tunaiongelea lakini
pia yapo mazingira mengine mengi.
2. AINA ZA TALAKA
Talaka twaweza kuzigawa katika makundi mawili nayo
ni, talaka itolewayo nje ya mahakama ambayo hutokana na ndoa zilizo katika mfumo
wa kimila na nyingine ni talaka itolewayo mahakamani ambayo sisi hapa
tutaiongelea.
3. UKITAKA TALAKA
FUATA HATUA
HIZI.
( a ) Hatua ya kwanza kabisa kwa anayehitaji kupata
talaka ni kupeleka malalamiko yako kwenye kitengo maalum kijulikanacho
kama Bodi ya usuluhishi wa ndoa ambayo imeanzishwa na Sheria ya ndoa kifungu
cha 102(1).
Bodi itasikiliza malalamiko na kujaribu kufanya usuluhishi. Lengo la bodi
ni kusuluhisha ambapo ikishindwa kusuluhisha itaandaa maelezo yanayohusiana na
kilichojiri wakati wa usuluhishi ikiwa ni pamoja na kueleza namna ilivyoshindwa
kusuluhisha. Sharti hili limewekwa ili kulinda ustawi wa familia
kwa kuwa kupitia bodi wakati mwingine kunarejesha mahusiano ambayo yalikuwa
tayari kuvunjika.
4. BODI
YA USULUHISHI NI IPI NA IKO WAPI.
Kwa waislamu
bodi ya usuluhishi ni Bakwata.Hautakiwi kufika mahakamani kudai talaka
mahakamani mpaka una maelezo ya Bakwata
kuwa umepitia kwao na suluhu imeshindikana.Ofisi za Bakwata zipo maeneo
mbalimbali lakini haswaa ukiuliza misikitini watakuonesha.
Kwa wakiristo bodi
ya usuluhishi iko ustawi wa jamii. Hautakiwi kufika mahakamani kudai
talaka mpaka una maelezo kutoka ustawi
wa jamii kuwa wamesuluhisha na imeshindikana. Ofisi za ustawi wa jamii
zipo katika makao makuu ya kila wilaya
ukifika hapo uliza utaoneshwa.
( b ) Hatua ya kwanza tumeona ni kupitia hizo bodi za
suluhu sasa ni hatua ya pili ambayo ni mahakamani ambapo
mwombaji atatakiwa kufika akiwa na kibali chake kutoka bodi kinachoonesha
mwenendo wa usuluhishi na kushindwa kwa bodi kurejesha mahusiano. Ni katika
mahakama ambapo mwombaji atatoa maelezo ya kuomba talaka huku akionesha sababu
za kuishawishi mahakama hiyo ili ipitishe hukumu ya kuvunja ndoa. Kubwa zaidi
atakalolionesha ni kuwa ndoa hiyo
haiwezekani tena hata kwa namna gani.
Kwahiyo hatua ni mbili tu ile ya bodi ya usuluhishi na unamalizia
na mahakamani.
5.SABABU ZA KISHERIA ZINAZOWEZA KUKUFANYA UOMBE TALAKA NI
HIZI.
( a ) Kwanza ni zinaa. Inapotokea kuwa mmoja
wa wanandoa amejamiiana na mtu mwingine ambaye si mme/mke wake na hali yupo
katika ndoa ni sababu ya kubwa ya
kuombea talaka.
( b ) Sababu nyingine ambayo mtu anaweza kuitoa
akiwa anadai talaka ni kunyimwa unyumba kunakoendelea. Linatumika neno
kunyimwa unyumba kunakoendelea kumaanisha kuwa haiwezekani
mwanandoa akanyimwa unyumba maramoja au mara mbili halafu akaamkia
mahakamani kudai talaka. Kunyimwa unyumba ili iwe sababu inabidi kiwe ni
kitendo chenye kuendelea na si kitendo ambacho kimejitokeza maramoja au
mara mbili.
( c ) Tatu , ukatili nao ni sababu anayotumiwa na mwombaji
kuombea talaka. Tunaweza kusema kuwa ukatili ni matendo ambayo hayakubaliki
yanayofanywa kwa makusudi na ambayo kimsingi yanaweza kusababisha
hatari kwa afya ya mtu na maisha yake kwa ujumla kama kumpiga mtu mara kwa
mara, kumtukana mtu mara kwa mara, kumuumiza kwa aina yoyote ile, kumwingilia
mwenza wako kinyume na maumbile, ulevi wa kupindukia na wenye kuendelea,
na mengine yote ambayo ni kinyume na ubinadamu.
( d ) Nne, talaka inaweza kutolewa iwapo mmoja wa wanandoa
amethibitisha mahakamani kuwa mwenzake amemtelekeza . Kumtelekeza mtu katika ndoa kuna maana ya kujitoa katika
mazingira ya uana ndoa bila sababu za msingi na bila ridhaa
ya mwenzako hata kama mnaishi chini ya paa moja. Kwa hiyo kutelekezwa si tu kuondoka nyumbani
mnakoishi na mwenza wako isipokuwa hata kuishi pamoja lakini bila kushirikiana
katika mambo mbalimbali nako ni kutengwa.
( e ) Tano mtu anaweza
kuomba talaka iwapo mwenzake amehukumiwa kifungo cha maisha au kwa
kipindi kisichoshuka miaka mitano. Kama mtu amehukumiwa kifungo kama nilivyosema ni hiari ya mwanandoa kuamua kuivunja kwa
talaka au kusubiri.
MWANDISHI WA
MAKALA HAYA NI
MWANASHERIA NA MSHAURI
WA SHERIA KUPITIA
GAZETI LA SERIKALI
LA HABARI LEO
KILA JUMANNE , GAZETI
JAMHURI KILA JUMANNE
NA GAZETI NIPASHE
KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com
Ahsante kwa ushauri mzuri
Asante kwa ufafanuzi