Saturday 17 January 2015

JIFUNZE JINSI YA KUUNDA KAMPUNI

NA  BASHIR  YAKUB----

NI ukweli usiofichika kuwa  biashara  na ujasirimali  kwa pamoja vimekua kwa kiwango kikubwa hapa nchini. Yote hii inatokana na sababu nyingi, ikiwemo ya kukua kwa biashara za kimataifa, maendeleo ya mawasiliano, marekebisho ya baadhi ya sera za nchi na sababu nyinginezo. 
Kwa hakika hali yote hiyo, imesababisha ugumu kwa wajasiriamali wanaofanya biashara zao nje ya kampuni. Kwa dunia ilivyo kwa sasa, si rahisi mtu kufanikiwa katika biashara yake kama biashara yake hiyo haiku katika mfumo wa kampuni. Hata iwe ndogo ya kuuza mayai au kufuga kuku, mafanikio zaidi ni pale biashara hiyo utakapoifanya iwe katika mfumo wa kampuni. 
Ni kutokana na umuhimu huo, imenilazimu niwasilishe mjadala huu kwa wasomaji wangu, hasa vijana, kuhusu kampuni, tukijielekeza zaidi katika aina na uundwaji wake kutokana na Sheria ya Makampuni  ya mwaka 2002.

KAMPUNI   NI NINI? 

Awali ya yote, yatupasa tufahamu maana ya kampuni. Kwa ufupi, tunasema kampuni ni muunganiko wa kibiashara wa mtu zaidi ya mmoja ulioundwa na kusajiliwa chini ya Sheria ya Makampuni  ya 2002. Katika maana hii, tunaona kwamba kampuni lazima uwe muunganiko wa watu. Waweza kuwa wawili, watatu na kuendelea. Hii ina maana kwamba hakuna kampuni ya mtu mmoja. 
Lazima umiliki wake uwe zaidi ya mmoja, uwe na mke wako au mume wako au na rafiki, au na mtoto wako, itategemea mazingira ya biashara yenyewe, lakini huwezi kuwa mmoja.
Pili; tumeona katika maana hiyo kwamba ili iitwe kampuni, lazima iwe imesajiliwa chini ya sheria ya makampuni. Hiyo ndiyo kampuni, zaidi ya hapo biashara yako itakuwa katika mfumo mwingine kabisa, ni kitu kingine na si kampuni.

AINA   ZA   KAMPUNI

Kabla hatujaingia katika mchakato wa kuunda kampuni, ni vyema pia tukafahamu aina za kampuni. Hii itakusaidia kujua sifa za kila kampuni na aina ya kampuni unayotaka kuiunda. 

KAMPUNI  ZIMEGAWANYIKA  KATIKA  MAKUNDI  YAFUATAYO:-

Kampuni ya umma (public company)
Hii ni kampuni umma kama jina lake lilivyo kwa sababu kwamba kila mtu au kila mwanajamii, anaruhusiwa kuomba  uanachama ikiwa tu atatimiza masharti ya kuwa mwanachama au mshirika. Uanachama katika kampuni ndiyo umiliki. Ukisikia mtu ni mwanachama ( member) ni mmiliki. Na umiliki au uanachama unatofautiana kutokana na kiasi cha hisa anazomiliki mtu. 
Kwa hiyoi, katika kampumi ya aina hiyo mtu hawezi kuzuiwa kuwa mmoja wa wamiliki, bali yeyote mwenye uwezo, hata kama ni adui yako, ili-mradi umesajili kampuni kama ya umma, atakuwa pamoja nawe katika umiliki wa kampuni.
Pili; ili kampuni ya umma iweze kuanzishwa ni lazima iwe na wanachama wasiopungua saba. Wanachama wakiwa sita, watano na kushuka chini hawawezi kuanzisha kampuni ya aina hiyo.
Tatu; Wakurugenzi wake lazima waanzie wawili. Maana yake ni kwamba mtu mmoja hawezi kuwa mkurugenzi katika kampuni yoyote ya umma.
Nne; ni kwamba katika kampuni ya umma hisa zake ni huru, ikiwa na maana kuwa hisa zake zinaweza kuhama kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. 
Mwanachama mmoja anaweza kumuuzia  mwanachama mwingine hisa zake zote au kiasi. Kila mtu yuko huru na hisa zake, anaweza kumuuzia mwingine au akampa zawadi, haizuiwi.

*Kampuni binafsi (private company)
Hii ni aina ya kampuni wengi wetu wameziunda. Karibu asilimia kubwa ya kampuni tunazoziona zikifanya biashara, ni kampuni binafsi. Kampuni hizi zina sifa zifuatazo:-
   
Kwanza; wanachama wake hawazidi 50, bila kuhesabu au kujumuisha wafanyakazi. Pili; hisa zake hazihamishiki kirahisi, kwa maana kwamba huwezi kuuza au kugawa hisa zako kwa mtu mwingine bila ridhaa ya wanachama wenzako.
Kwa kuwa ni kampuni binafsi, mtu yeyote anayeingia lazima awe  amekubalika kwa wanachama wengine, pengine asiwe adui au yeyote asiyehitajika.
Tatu; inakatazwa kwa kampuni binafsi kuwaalika au kuwaita watu wengine wa nje kununua hisa. Nne; inawezekana ikawa hata na mkurugenzi mmoja, na si lazima wawe wawili au zaidi.
*Kampuni za kisheria (statutory company). Hizi ni kampuni zinazoanzishwa kwa Sheria Maalum za Bunge. Mara nyingi kampuni hizi, huundwa ili kutimiza majukumu maalum katika jamii hasa huduma za kijamii. Taasisi nyingi za Serikali pamoja na mashirika ya umma, huwa ni kampuni za aina hii. Kwa uchache, hizo ndizo aina ya kampuni.

JINSI  YA  KUUNDA   KAMPUNI

Huu ndio mzizi wa mada hii kwa kuwa wengi wetu tungependa kufahamu ni taratibu zipi, zinaweza kufanya kampuni ikaundwa. Kwa Tanzania, kampuni inaundwa kwa kufuata utaratibu huu.
*
Hatua ya kwanza ni kuchagua jina la kampuni
Kampuni lazima iwe na jina linalotambulika na linalojitofautisha na majina ya makampuni mengine nchini. 
Hatua hii, kwa lugha ya biashara huitwa ‘Name Search’ ambapo unatakikwa kuandika barua kwa Msajili wa Kampuni, kwa maana ya Brela. Ukifika katika ofisi hizo, utaeleza jina la kampuni linalopendekezwa, hivyo jina hilo huingizwa kwenye mtandao wa makampuni yaliyosajiliwa na Brela, ili kuona kama kuna yenye jina linalofanana na hilo lako.

Kwa kuwa majina yote ya kampuni nchini yako ofisi hiyo, hivyo si rahisi kampuni zaidi ya moja kuwa na majina yanayofanana. Ikibainika kuwepo kwa kampuni yenye jina kama la kwako, Ofisa wa Brela, atakuelekeza utafute jina jingine, na kama atakuta hakuna jina la kampuni linalofanana na la kwako, basi jina hilo litapokelewa kwa hatua inayofuata.

Baada ya jina kuwa limethibitishwa, kwa maana ya kukubaliwa na Msajili wa Kampuni, hatua inayofuata ni kuwasilisha kwa Msajili waraka wa kampuni na katiba ya kampuni. 
Waraka wa kampuni au kwa lugha ya kigeni ‘memorandum of association’, ni waraka maalum uliosainiwa na wanachama wote ambao hueleza na kuchambua kile ambacho kampuni itakifanya. Shughuli za kampuni zinatakiwa kuelezwa vyema ndani ya waraka huu. Waraka huu lazima uwe na mhuri wa mwanasheria.

Katiba ya kampuni au kwa lugha ya kigeni, ‘article of association’ kwa upande mwingine, nayo lazima iwe imesainiwa na wanachama wa kampuni husika. Katiba hii ndiyo inayoeleza uendesahaji mzima wa kampuni.

Aidha, inaeleza haki na wajibu wa wanahisa, uongozi wa kampuni, mgao wa mapato, nguvu na mamlaka ya wakurugenzi, mikutano na utaratibu wake, umiliki na ugawaji wa hisa, uhamisho wa hisa na kadhalika. Hii nayo lazima iwe imesainiwa na mwanasheria.
Lazima kupeleka kwa Msajili wa Makampuni maelezo (statement) yanayowahusu wakurugenzi wa kampuni. Maelezo hayo lazima yaambatane na wasifu wa kila mkurugenzi na unatakiwa kuwa umeelezwa vyema.

Lazima pia ijazwe fomu maaalum yenye maelezo yanayohusu anuani kamili ya ofisi za kampuni. Anuani hapa si tu Sanduku la Posta, bali pia mahali zilipo ofisi za kampuni, kwa maana ya mahali ambapo kampuni hiyo itaendeshea shughuli zake.
Aidha, lazima ijazwe fomu maalum ambayo ipo kama kiapo kuonesha kuwa matakwa yote ya kisheria yametimizwa, hivyo kampuni inatakiwa kupatiwa usajili.
Fomu hiyo inajazwa na Wakili au mtu yeyote ambaye jina lake limetajwa katika katiba kama mkurugenzi wa kampuni au katibu wa kampuni. Fomu hii inakuwa ni ushahidi kuwa matakwa yote yametimizwa kwa ukamilifu.

Baada ya kutimiza matakwa yoter hayo, hapo kampuni inaweza kusajiliwa kwa kupewa Cheti cha Usajili. Taratibu zote hizi, ikiwa ni pamoja na kuandaa katiba, fomu na waraka, mara nyingi na kwa wepesi zaidi, zinashauriwa zifanyike katika ofisi za wanasheria.  
Kwa kumalizia nishauri kuwa kufanya biashara kwa mfumo wa kampuni, ni muhimu mno kuliko ambavyo baadhi ya watu wanaweza kufikiria.

Karibu biashara zote za kisasa, hufanyika kwa mfumo huo wa kampuni. Asikudanganye mtu kuwa atapatikana mfanyabiashara mkubwa kutoka Ulaya, Amerika au hata hapa kwete ambaye atakubali kufanya biashara na mtu binafsi. Labda biashara hiyo iwe ya kukufanya wewe kuwa kibarua!
Kampuni zote za ndani na nje, huwa hazifanyi biashara na watu binafsi, bali kama kama watu hao wamejiunga pamoja na kuwa kampuni. 

Nieleweke vyema hapa kwamba ninaposema biashara, simaanishi biashara kubwa sana, bali biashara hiyo hiyo ndogo unayoifanya, hata kama ni ya ufugaji kuku wa mayai au wa nyama, biashara ya kuuza maziwa biashara ya duka la vyakula, biashara ya huduma ya pesa kwa njia ya simu, kuuza mazao, kijiwe chako cha ufundi magari au seremala na kadhalika, zote hizo usizifanye wewe kama wewe.

Ukweli ni kwamba hakuna atakayekupa kazi ya maana kama wewe ni mtu binafsi. Biashara ya sasa haifanywi hivyo. Usikwamishe kukua kwa biashara zako, anza sasa kuunda kampuni yako!

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI  LA  SERIKALI   LA   HABARI   LEO  KILA  JUMANNE  , GAZETI  JAMHURI   KILA  JUMANNE  NA  GAZETI  NIPASHE  KILA  JUMATANO. PIA  NDIYE MWANZILISHI  NA  MKURUGENZI   WA  BLOG HII.    
0784482959,        
 0714047241,         
bashiryakub@ymail.com


6 comments:

  • Unknown says:
    13 January 2020 at 23:44

    ASANTE SANA

  • Unknown says:
    26 February 2020 at 04:06


    ahsante kwa maelezo mazuri

  • Unknown says:
    4 May 2020 at 10:33

    Asante sana

  • Jamaal says:
    17 June 2020 at 01:57

    Sisi tupo wawili je twaweza fungua kampuni kwa mtaji wetu mdogo.pia inakuwaje katika kodi kuilipa serikal

  • Unknown says:
    26 November 2021 at 08:20

    Asante kwa ufafanuzi, anataka kuanziasha kampuny Nina wafanyakazi 2/na mie watatu na kijana wangu mbona idadi naona haitoshi kama mlivyoeleza kwemye taratibu zenu? Naomba msaada kwa hili

  • Unknown says:
    26 November 2021 at 08:22

    Pia biashara nilizo Nazi ni maduka ya dawa na duka LA vifaa vya umeme na pia nafuga kuku na nguruwe je hapa activities zangu sitaonekanaje kwnye logo?

Post a Comment