Wednesday, 2 September 2020

NINI UFANYE UNAPOSABABISHIWA HASARA.

|0 comments

 


Ushahidi waliochoma polisi Bunju waendelea - MtanzaniaGARI YA KUBEBEA WAGONJWA YAPATA AJALI MBAYA YA KUOGONGANA NA GARI NYINGINE  NDOGO | EDDY BLOG | Edwinmoshi Official Blog

NA  BASHIR  YAKUB -  

Hasara yoyote ambayo mtu atakusababishia yafaa akufidie isipokuwa kama  umeamua kusamehe, au kama ilitokana na mchakato  ambao haukuwa halali kisheria. Katika ufafanuzi makala yatajikita katika Sura ya 345, Sheria ya Mikataba ambayo kimsingi ndiyo inayoongelea jambo hili.

Tutaliangalia hili kwa ujumla wake kupitia mafungu matatu, kwanza KUKATAA KUFIDIWA, pili KUKUBALI KUFIDIWA, na tatu MAMBO YANATOTAKIWA WAKATI WA KUFIDIWA.

1.KUKATAA KUKUFIDIA.                                       

Yumkini yule aliyesababisha hasara anaweza kukataa kukulipa au kufidia kile alichosababisha. Ikiwa hili litatokea basi yafaa umwandikie taarifa ya kumtaka kukufidia mara moja. Taarifa hii inapendeza zaidi akiandikwa na Wakili na kwa anuani yake Wakili. Hata hivyo hata wewe mwenyewe waweza kuandika.

Taarifa itakuwa ikieleza kile alichotenda, hasara iliyosababishwa na hilo tendo lake, kumtaka afidie hiyo  hasara, siku au muda ambao unampa  afidie hiyo hasara,na nini utafanya ikiwa atashindwa kufidia hiyo hasara ndani ya muda uliompa.

Kawaida unaweza kumpa siku 7, siku 14, siku 30 , siku 45, au muda wowote  kadri unavyoona  unafaa na kutosha. Na utaeleza pia kitu ambacho utafanya/hatua utakazochukua ikiwa atashindwa kukulipa. Na kawaida kitu cha kufanya  huwa ni kumfikisha mahakamani mhusika. Usije ukamdhuru, au kingine chochote ambacho hakimo katika utawala wa sheria.

Basi, ikiwa kweli muda huo umeisha na huyo mtu hajakufidia au kukuita katika mazungumzo basi yafaa sasa kumfikisha mahakamani. Kumfikisha mahakamani ni kumlazimisha kufidia hasara aliyoisababisha. Na unapokuwa umemfikisha mahakamani  malipo yanaongezeka kwasababu na gharama za kesi pia huingia.  Hivi ndivyo unavyoweza kumlazimisha aliyekataa.

2.  KUKUBALI KULIPA FIDIA.

Kukubali kupo aina mbili. Kwanza kukubali kwa maandishi kuwa nimesababisha hasara kwahiyo nitakulipa, na pili kukubali tu kwa mdomo kuwa nimesababisha hasara hivyo nitakulipa. Kwa mujibu wa kifungu cha 10 cha Sheria ya Mikataba , makubaliano ya mdomo ambayo hayako katika maandishi nayo ni mkataba halali kisheria.

Kwahiyo iwe ameahidi kulipa hasara kwa maandishi au kwa mdomo bado yote ni makubaliano na yanakubalika kisheria.  Lakini pia ile ahadi pekee ambayo huyu aliyesabababisha hasara ataitoa kwa yule aliyemsababishia hasara  nayo  ni mkataba kamili kisheria. Ahadi tu, yaani ile kutamka tu kuwa nitakulipa au nitakufidia tayari ule ni mkataba tosha na yafaa utekelezwe.

3.  MAMBO AMBAYO YANATAKIWA KUFIDIWA.

Mambo haya ni kwa mujibu wa kifungu chav 77 cha Sheria ya Mikataba. Kwanza ni uharibifu wa aina yoyote ikiwa upo. Pili, ni gharama ambazo umetumia kuanzia unahangaika na huyo mtu mpaka kufikia mnakubaliana, pengine ulimtafuta, ulifungua kesi, ulitumia nauli, ulipiga simu na kila aina ya gharama ambayo uliingia anatakiwa kuilipa. Tatu ni malipo mengine ambayo mtakubaliana, au yalikuwa yamekubaliwa katika ule mchakato wa mwanzo aliouharibu.

Hivi ndivyo unavyoweza kufidiwa hasara.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MWANDISHI  WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI  LA JAMHURI KILA JUMANNE.  0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com

 


Monday, 10 August 2020

KUCHELEWA KUPATA NAKALA YA HUKUMU.

|0 comments

 

Judiciary of Tanzania | Home


Na  Bashir  Yakub  - 

1.UMUHIMU WA NAKALA YA HUKUMU.

Mara nyingi wale ambao hawakuridhishwa na maamuzi ya mahakama kwenye hukumu hutaka kukata rufaa. Rufaa ni malalamiko yanayopelekwa mahakama ya juu zaidi  yakilalamikia  hukumu au maamuzi  yaliyotolewa  na mahakama ya chini. Rufaa hufunguliwa na mtu ambaye hakuridhika na kile kilichoamuliwa. Kwahiyo hata wewe kama unayo kesi ambayo tayari imetolewa hukumu na  hukuridhishwa na kile kilichoamuliwa basi unayo haki ya msingi ya kukata rufaa.

Na huna haja ya kuhofu kama unazo sababu za msingi na za kisheria. Waweza kuwa umeshindwa mahakama ya chini lakini ukaibuka mshindi mahakama ya juu ambako umekata rufaa.

Hata hivyo, huwezi kukata rufaa bila kuwa na nakala ya hukumu. Na hapa ndipo linapojitokeza suala la kupata nakala ya hukumu kwa wakati na bila kucheleweshwa. Narudia huwezi kukata rufaa ikiwa hujapata nakala ya hukumu kutoka  mahakama  iliyotoa uamuzi.

2. HASARA ZA KUCHELEWA KUPATA NAKALA YA HUKUMU.

Ikiwa lengo lako ni kukata rufaa basi yafaa ujue kuwa rufaa zote huwa zina muda wake. Zipo za siku 45,za siku 30 nk. Muda huo unahesabika tokea siku hukumu iliposomwa. Ni ndani ya muda huo ambapo unatakiwa kukata rufaa. Nje ya muda huo huruhusiwi na unakuwa umepoteza haki hiyo.

Sasa wakati mwingine muda huo waweza kuisha ukiwa bado unashughulikia kupata nakala  ya hukumu. Ni hapa tunapotakiwa kujua la kufanya ili kuepuka kadhia na mazingira hatari kama haya.

3.  KUCHELEWA  KUPATA NAKALA YA HUKUMU.

Unaweza kuchelewa kupatiwa nakala ya hukumu kwasababu mbalimbali. Moja ni kutokuomba kwako kupatiwa nakala ya hukumu. Kesi au shauri linapoisha yafaa mara moja uombe kupatiwa nakala ya hukumu. Katika mada nyingine nitaeleza utaratibu wa kuomba nakala ya hukumu. Kwahiyo kumbe waweza kuchelewa kuipata kwasababu hukuiomba.

Pili, waweza kuchelewa kuipata kwasababu ya uwezo na ufanisi wa mahakama husika. Nakala  ni lazima iwe imechapwa na imesahihishwa vizuri. Ukosefu wa vitendea kazi kama kompyuta laweza kuwa tatizo la kuchelewa kupata hata kama uliiomba kwa wakati.

Tatu, uchache wa watumishi/makarani wachapaji ambapo huwa na mizigo mingi na hivyo huchapa kazi moja moja kwa awamu jambo ambalo laweza kukuchelewesha ukisubiri kazi yako ifikiwe.

Nne,uzembe wa wachapaji  na wakati mwingine huwa ni makusudi ili kujenga mazingira ya  kupozwa(rushwa).

4.  NINI UFANYE IWAPO NAKALA YA HUKUMU IMECHELEWESHWA.

Jambo la kwanza, kesi au shauri linapoisha hakikisha siku hiyohiyo au inayofuata umeandika barua ya kuomba nakala ya hukumu. Hii itakusaidia  kwani hata ukichelewa kukata rufaa ukapitwa na mda utasema mimi niliomba nakala mapema kwahiyo kuchelewa sio makosa yangu.

Pili, ikiwa unaona makarani au wachapaji wanakuchelewesha bila sababu au huelewi ni namna gani wanavyoshugulikia suala lako  tafuta muda muone hakimu aliyetoa hukumu na mpe maelezo  yako na namna ambavyo hujapatiwa nakala hiyo. Au waweza kumuona hakimu mfawidhi. Hakimu mfawidhi ndiye kiongozi wa mahakama husika. Ukiuliza hakimu mfawidhi ni nani utaoneshwa na hapo utampatia malalamiko yako. Hivi ndivyo unavyoweza kuepuka kupoteza haki hii.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MWANDISHI  WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI  LA JAMHURI KILA JUMANNE.  0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com

 

 


KOSA LA KUJIPATIA MALI KWA NJIA YA UDANGANYIFU LINATUMIWA VIBAYA NA POLISI.

|0 comments

 

Mtuhumiwa wa kifo cha Mowzey Radio mikononi mwa Polisi - Bongo5.com


NA  BASHIR  YAKUB - 

Yapo mambo ambayo kwa mujibu wa sheria sio kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu. Hata hivyo polisi kwenye vituo vyao wamekuwa wakilazimisha mambo hayo kuwa kosa hilo la kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu kwasababu wanazozijua wao, mojawapo ikiwa ni mchongo kutoka kwa mlalamikaji.

Masuala ya watu kudaiana hela ama migogoro ya ardhi  kama mtu mmoja kuwauzia watu tofauti ardhi moja si masuala ya polisi, na wala si makosa ya kujipatia pesa ama mali kwa njia ya udanganyifu.

Tumesema mara nyingi kuwa, mamlaka ya polisi ni  kushughulikia masuala ya jinai tu. Masuala ya kudaiana hela ni masuala ya madai na sio jinai. Kwa msingi huu yapo nje kabisa ya mamlaka yao. Masuala ya kudaiana hela yanaongozwa na sheria ya mikataba Sura ya 345, pamoja na Sheria nyingine za fedha na rehani, wakati masuala ya migogoro ya ardhi yanaongozwa na Sheria namba 4 na 5 za ardhi, Sheria ya Usajili wa ardhi na nyinginezo mtambuka.

Kwahiyo makosa haya na mengine yanayofanana na haya hayawezi kuitwa ya kujipatia mali ama fedha kwa njia ya udanganyifu. Mara nyingi makosa haya yamekuwa yakipelekwa huko kwenye kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu kwa makusudi ili kumkomoa mtu ili awekwe ndani nk.

Vifungu vya 301, na  302, vya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16, vinaelezea kosa la kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu kumaanisha ujinai. Mfano wa makosa ya kujipatia mali ama fedha kwa njia ya udanganyifu ni wale wanaotuma SMS au kupiga simu na kusema umejishindia kitu fulani na hivyo utume hela ili upate kitu hicho, na pesa kweli zikatumwa kwake, huku jambo hilo sio kweli. Fedha hiyo itakuwa imepatikana  kwa njia udanganyifu.

Au mtu anakwambia lete hela nikuletee mali fulani au nakuagizia japan huku akijua sio kweli. Fedha hizo akizipokea na asilete alichoahidi zitakuwa zimepatikana kwa njia ya udanganyifu. Mifano kama hiyo ndiyo ya kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu.

Aidha, tunasisitiza tena kuwa masuala ya kudaiana hela, au ugomvi wa ardhi hayaingii kwenye jinai ya kujipatia pesa/mali kwa njia ya udanganyifu, bali ni madai. Na hivyo, ni kosa kabisa askari yeyote katika kituo chochote kujihusisha na masuala ya madai, labda iwe kwa ushauri. Kama askari atachukua masuala haya ili awashauri au awapatanishe hiyo itakua ni sawa. Ila kama atayachukua ili afungue jalada la kesi hilo ni kosa.

Mahakama kuu ya Tanzania imeshatoa maamuzi mengi kuelezea jambo hili na moja ya maamuzi ya hivi karibuni ni katika Madai ya Rufaa Namba 23/2017 kati ya RIBENT RWECHUNGURA vs PONSIAN MUTAYABARWA ambapo Jaji  KAIRO alisema ni makosa mgogoro  wa ardhi kufunguliwa polisi.

 

Sehemu husika ambapo yafaa upeleke masuala hayo ni mahakamani moja kwa moja. Ukiulizia mahakamani au ukampata Wakili utaelekezwa utaratibu mzima wa hapo mahakamani.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MWANDISHI  WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI  LA JAMHURI KILA JUMANNE.  0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com

 


|0 comments


NOTISI YA SIKU 14 KABLA YA KUPIGA MNADA NYUMBA.

|0 comments

 

NYUMBA ZA LUGUMI ZAPIGWA MNADA - HABARI MSETO


NA  BASHIR  YAKUB  - 

Hii ni moja ya sehemu ambayo wanadishaji/madalali(auctioneer)  wengi  huwa wanawakosea wadaiwa. Huwezi kufikia hatua ya kuuza nyumba au kiwanja cha mtu kabla hujampa taarifa ya siku 14, na kuhakikisha hizo siku 14 kuwa zimepita. Madalali wengi  akishapewa kazi na benki ama taasisi nyingine ya mikopo kwa ajili ya kunadisha, basi anaanza kazi ya kuuza hapo hapo,au baada ya mda mchache.

Kifungu cha 12((2) and (3) cha Sheria ya Madalali Wanadishaji sura ya 227 kinasema kuwa hakuna ruhusa kwa dalali yoyote kuuza nyumba ama kiwanja cha mtu mpaka mtu huyo awe amepewa taarifa ya siku 14, na siku hizo ziwe zimeisha.

Kumbe tunaona kuwa haitoshi tu kumpa mtu taarifa  ya siku 14, bali pia hizo siku 14 alizopewa ni lazima ziwe zimeisha. Maana yake tunahesabu siku 14 tangu ulipopokea taarifa,na baada ya huo mda ndo tunasema zimeisha.  Kuuza kunaweza kuanza siku ya 15, siku ya 14 kamili dalali hawezi kuuza nyumba yako.

Nasisitiza eneo hili kwasababu baadhi ya madalali wamekuwa na tabia ya kutoa hiyo notisi ya siku 14, lakini kabla ya muda huo kuisha  anauza nyumba/kiwanja. Hili ni kosa na kama hilo limetokea kwako basi uuzaji huo ni batili na hautambuliwi na sheria.

Katika kesi ya DOSCA DIDON KARANJA vs TPB BANK PLC, NAMIC INVESTMENT LTD na HAIDARI MOHAMMED HARIRI, Madai ya Ardhi Namba 64/2015, Dosca alipewa notisi ya kuuza tarehe 14 August 2015 na tarehe 16 August 2015, yaani siku mbili baadae, dalali akauza nyumba yake.

Dosca alifungua kesi mahakamani kulalamikia baadhi ya mambo likiwemo hili. Mahakama kuu ilitoa hukumu kuwa, hata kama alikuwa anadaiwa na benki na ameshindwa kurejesha marejesho,bado mauzo ya nyumba yake yalikuwa batili na haramu. Kwa msingi huu akarejeshewa umiliki wa nyumba yake.

Kwahiyo ni muhimu ukalijua hili  ili haki iweze kutendeka. Ni vigumu sana haki yako kutendeka kama wewe mwenyewe hujui hata hiyo haki kama unayo.Nimeandika mara nyingi kuwa kudaiwa au kushindwa kurejesha hakuna uhusiano wowote na kusigina haki za mdaiwa. Mdaiwa ana haki nyingi na lazima zizingatiwe anaposhindwa kurejesha.

Moja ya tatizo la taasisi za mikopo ni kuwapa wakopaji limkataba kama kitabu, lenye kurasa nyingi,lililoandikwa kwa kiingereza kigumu cha kisheria, kiasi kwamba hata kama unajua kiingereza bado lugha iliyo kwenye likitabu hilo itakutatiza tu. Jambo ambalo hata kama zimeelezwa haki za mkopaji mle ndani, si rahisi kuzijua  na akajifunza. Ingekuwa ni vyema zaidi mkopaji pamoja na semina za matumizi ya pesa ya mkopo, lakini pia akafundishwa haki zake hasa wakati atakaposhindwa kurejesha.

Kifungu nilichotaja hapo awali cha 12((2) and (3) cha Sheria ya Madalali Wanadishaji Sura ya 227, kinasisitiza kuwa haitoshi tu kumpa mdaiwa notisi ya siku 14, bali pia notisi hiyo iwe katika lugha inayoeleweka, na yasiwe tu maandishi katika karatasi, bali pia namna nyingine za kumjulisha zitumike.

Kwahiyo  wadaiwa yafaa myajue haya ili muwe na uwezo wa kuchukua hatua stahiki.  

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MWANDISHI  WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI  LA JAMHURI KILA JUMANNE.  0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com

 


MKURUGENZI WA KAMPUNI HARUHUSIWI KUFUNGUA KESI KWA NIABA YA KAMPUNI.

|0 comments

 

Appointment of Directors: Managing Director, Shareholders, Resolution


NA  BASHIR  YAKUB -  

Kampuni zote, ziwe kubwa au hata zile zenye watu wawili au zile za familia huwa na wakurugenzi wake(Directors). Kampuni ikiwa na watu wawili utakuta hao hao ndio wanahisa na haohao ndio wakurugenzi. Basi yote ni sawa na inaruhusiwa kisheria.

Hata hivyo, kampuni hiyo hata kama ni ya watu wawili au ya familia mke na mme ama vinginevyo, mkurugenzi yeyote katika hiyo kampuni haruhusiwi kufungua kesi kwa niaba ya kampuni. Anaweza kufungua kesi kama yeye binafsi kwa kutumia jina lake lakini si kwa niaba ya kampuni na kwa kutumia jina la kampuni.

Kwa mfano kampuni inaitwa MECCO CO. LTD. Hawezi kufungua kesi kwamba MECCO CO. LTD inamshitaki fulani yaani MECCO CO. LTD vs SHABAN. Hataruhusiwa kutumia jina la kampuni namna hiyo. Hii ni hata kama kampuni imetendewa kosa fulani ambalo kampuni ni lazima ishitaki. Bado hataruhusiwa kufanya hivyo. Na hii ni kwa maafisa wote wa kampuni wakiwemo wanahisa,mameneja, katibu wa kampuni(company secretary), mwanasheria wa kampuni na afisa yeyote yule wa kampuni.

Kitu pekee chenye mamlaka ya kushitaki kwa niaba ya kampuni na kwa kutumia jina la kampuni ni maamuzi ya bodi ya kampuni(Board Resolution). Maamuzi haya ya bodi hufanywa na wakurugenzi wa kampuni kwa niaba ya kampuni na baada ya kupata ridhaa ya wanahisa.

Kama hakuna maamuzi ya jumla ya bodi ya wakurugenzi ya kampuni (Board Resolution)  ya kuamua kampuni kushitaki basi mkurugenzi yeyote, ama mwanahisa, ama afisa yeyote wa kampuni hawezi hata kidogo kushitaki kwa niaba, na kwa jina la kampuni.

Katika maamuzi ya mahakama kuu yaliyotolewa na Jaji Maghimbi tarehe 6/3/2020 katika kesi ya ardhi No. 147/2018 kati ya Evarist Steven Swai na Msafiri Enterpises Co. Ltd  vs The Registered Trustee of Chama cha Mapinduzi na wengine wawili, mahakama kuu imeifuta kesi iliyofunguliwa na mkurugenzi wa kampuni kwa niaba ya kampuni kwasababu ya kutokuwa na Maamuzi ya jumla ya bodi ya wakurugenzi(Body Resolution).

Mahakama imesema kuwa,hata kama kampuni husika inaonekana kuwa ni ya familia, na kuwa mkurugenzi aliyefungua kwa niaba ya kampuni kuonekana ndiye pia mwenye hisa kubwa katika kampuni hiyo kuliko wote, bado hana mamlaka ya kufungua kesi kwa niaba na kwa kutumia jina la kampuni kama hana Maamuzi ya jumla ya Bodi ya Kampuni(Body Resolution).

Mahakama imesisitiza kuwa alitakiwa kwanza aitishe kikao cha wakurugenzi, wakae na watoe maamuzi kwa kuandaa nyaraka ya maamuzi ya bodi ya wakurugenzi(Body Resolution) ambayo itakua inampa mamlaka, na kuridhia kampuni kushitaki. Kinyume cha hivyo ni kosa ambalo adhabu yake ni kesi kufutwa,kulipa gharama, ama vinginevyo.

Katika uamuzi huu mahakama haikuwa inatoa uamuzi mpya  bali maamuzi ya namna hii ndio msimamo wa mahakama na sheria kwa mda mrefu  na hapa ilikuwa ikisisitiza tu msimamo wake.

Sababu za kutoruhusu kila mkurugenzi,ama mwanahisa, ama afisa mwingine kushitaki kwa niaba ya kampuni bila Maamuzi ya bodi, ni kuondoa uwezekano wa kila mmoja kutumia jina la kampuni kushitaki jambo ambalo linaweza kuitia hasara kampuni, lakini pia kuepuka kutumia jina la kampuni vibaya,kuepusha kuiingiza kampuni kwenye migogoro isiyoisha nk.

Kwa wenye makampuni ambao wanahitaji kushitaki kwa kutumia majina ya kampuni,hasa makampuni madogo ya wajasiriamali ambayo pengine kwao hili ni geni, yawapasa wakae kikao cha wakurugenzi, wapitishe maamuzi ya jumla(Body Resolution) ya kuruhusu kampuni kushitaki, na maamuzi hayo yawe katika maandishi/nyaraka maalum iitwayo,”COMPANY/DIRECTORS BODY RESOLUTION”.

Nyaraka hiyo ni lazima iambatanishwe kwenye mashtaka(Plaint) ili wakati kesi inafunguliwa iwe ushahidi kuwa maamuzi ya kampuni kushitaki yalipitia hatua hii muhimu kisheria.  Basi tufanye hivyo.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MWANDISHI  WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI  LA JAMHURI KILA JUMANNE.  0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com

 

MNAPOUZIWA KIWANJA KIMOJA WATU WAWILI, NANI ANAKUWA MMILIKI HALALI ?.

|0 comments

 

MBUNGE WA MVOMERO AMOS MAKALLA ATEMBELEA ENEO LA MGOGORO WA ARDHI KINYENZE


NA  BASHIR  YAKUB - 

Mtu mmoja anadai yeye amenunua kiwanja, na mwingine naye anadai amenunua kiwanja hichohicho. Na wote hawa wawili kila mmoja anadai kuwa ameuziwa kiwanja na mtu huyohuyo mmoja, na wote wana nyaraka za mauziano zenye jina na sahihi za huyohuyo muuzaji.

Maelezo yote katika makala haya yatakuwa yanarejea misingi ya sheria katika maamuzi ya mahakama kuu katika kesi ya JOVENT CLAVERY RUSHAKA NA DEVOTA YIPYANA MPONZI  dhidi ya BIBIANA CHACHA,Land Case No. 303/2016. Makala haya yanahusu pia nyuma na mashamba.

1.NANI MNUNUZI HALALI KATI YA WAWILI.

Ni hivi, pale ambapo watu wawili wameuziwa kiwanja kimoja kutoka kwa mtu mmoja basi mmiliki halali anakuwa yule aliyenunua wa kwanza. Suala la msingi iwe tu kuwa yule aliyenunua wa kwanza awe alinunua kwa kufuata utaratibu wa kisheria.

Ikithibika kuwa mnunuzi wa kwanza ana ushahidi wa kununua kwa kufuata utaratibu wa kisheria basi yeye ndiye anakuwa mmiliki halali. Na hapa hata kama baada yake kuna wanunuzi wengine kumi, bado yeye atabaki kuwa mnunuzi halali na mmiliki halali.

Kwa msingi huu, wale waliomfuatia katika kununua watakuwa si wanunuzi halali na hawatakiwi kudai umiliki wa kiwanja hicho. Ni muhimu kueleza hili kwa uwazi ili watu waelewe na waache kuwa wanagombana.

2. KWANINI MNUNUZI WA PILI HAWI HALALI.

Mnunuzi wa pili au mwingine yeyote anayemfuatia hawi halali kwasababu hadhi ya umiliki(good title) aliyokuwa nayo muuzaji anakuwa ameishaipoteza kwa kumuuzia yule wa kwanza. Kawaida unapokuwa na mali unakuwa na hadhi ya umiliki(good title), hadhi ambayo unaweza ukaitoa kwa kuiuza, kuitoa zawadi, au kuirithisha. Hadhi hiyo ukishaitoa kwa njia yoyote kati ya nilizosema hapa kwa mtu mwingine unakuwa umebakiwa huna kitu. Maana yake ukiitoa kwa njia ya kuuza,huna kitu tena cha kuuza baadae, labda kiwe kingine na sio kilekile. Kwahiyo akija mtu wa pili naye ukamuuzia kitu hichohicho maana yake umemuuzia kitu ambacho huna, na wewe mnunuzi wa pili umenunua kitu kutoka kwa mtu ambaye hana. Tafsiri rahisi anakuwa amekuuzia hewa.

3. NAMNA YA KUTAMBUA MNUNUZI WA KWANZA.

Namna pekee ya kujua nani mnunuzi wa kwanza na ni aliyefuatia ni kwa kila mmoja kuonesha mkataba wake wa mauziano na kutizama tarehe. Tarehe iliyotangulia ndiyo ya mnunuzi wa kwanza na tarehe zinazofuatia ni za wanunuzi wengine waliofuata.

Mashahidi walioshudhudia nao ni muhimu kuthibitisha hili. Lakini hawa ili wathibitishe ni lazima kuwe na mkataba wa mauziano. Hii ni kwasababu sheria inakataza kununua ardhi bila maandishi. Ardhi ikinunuliwa bila maandishi ni sawa na kusema haijanunuliwa. Kwa hiyo mashahidi watakuja kuthibitisha tarehe iliyo katika maandishi.  Hivi ndivyo tunavyojua nani aliyetangulia kununua.

4.  NINI AFANYE MNUNUZI WA PILI.

Haki aliyonayo mnunuzi wa pili au mwingine yeyote aliyefuatia ni  haki za aina mbili. Kwanza ni haki ya madai ya pesa yake ya manunuzi kwa ukamilifu pamoja na fidia kutoka kwa muuzaji aliyeuza mara mbili. Hili anaweza kulidai kawaida au akaitumia mahakama  na atapata haki hiyo.

Haki ya pili ni kumfungulia jinai ya utapeli mtu huyohuyo aliyeuza mara mbili. Hapa muuzaji anaweza kukabiliwa na adhabu ya kifungo, faini, pamoja na fidia.  Aidha aliyeuziwa mara ya pili anaweza kuamua kuchukua hatua hizi zote mbili kwa pamoja, yaani akamfungulia madai akidai kurudishiwa hela yake pamoja na fidia, na wakati huo huo akamfikisha polisi kwa ajili ya kesi nyingine ya jinai kwa ajili ya adhabu ya kifungo nk. Kwahiyo atachagua kuchukua mojawapo au zote mbili kwa pamoja.

Pamoja na hayo, kama inawezekana kufanya mazungungumzo na huyo muuzaji kurudisha hela yako pamoja na fidia za usunbufu basi ni bora zaidi. Na wakati mwingine aliyetapeliwa anaweza kufidiwa kwa kupewa kiwanja kingine ikiwa ataridhika nacho.

5. HALI IKOJE KAMA MNUNUZI WA PILI AMESHATAFUTA HATI MILIKI KWA JINA LAKE.

Mfano nyote mliuziwa kiwanja ambacho hakijapimwa, lakini  yule mnunuzi wa pili tayari akajiwahi na kutafuta hatimiliki, na yule mmiliki wa kwanza akabaki tu na mkataba wa mauziano. Na tunajua pengine hatimiliki ina hadhi kubwa kuliko mkataba wa mauziano.

Hali hii haibadilishi msimamo wa sheria katika hili. Bado mnunuzi wa kwanza mwenye mkataba wa mauziano anaendelea kuwa mmiliki halali dhidi ya mnunuzi wa pili mwenye hati miliki. Kwa maana hiyo hatimiiliki yake haimsaidii chochote katika hili.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MWANDISHI  WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI  LA JAMHURI KILA JUMANNE.  0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com

                                            

 

 


KUIOMBA MAHAKAMA KUTEMBELEA ENEO LA MGOGORO.

|0 comments

 

WAZO HURU: SERIKALI KUUPATIA MUAROBAINI MGOGORO WA ENEO LA ITUHA JIJINI  MBEYA-WAZIRI HASUNGA

NA  BASHIR  YAKUB - 

Ni muhimu ukiwa na kesi ya ardhi ambayo kwa maoni yako unahisi mahakama haiwezi kutoa haki inavyostahili bila kulitembelea na kulijua eneo la mgogoro(Locus in Quo) kuiomba itembelee. Sheria iko wazi na inakuruhusu wewe kuiomba mahakama kutembelea eneo la mgogoro ili kushuhudia hicho unachotaka iamini. Na hii haijalishi upo pande gani wa kesi, uwe mlalamikaji ama mlalamikiwa kila upande unayo haki ya kuomba kutembelea eneo la mgogoro.

Hatua hii ni muhimu sana kwasababu itatoa picha na mwanga wa kile ambacho unakiongelea. Itatoa taswira na ushahidi wa dhahiri. Wakati mwingine waweza kushindwa kueleza jambo vizuri  pengine kutokana na jiografia ya eneo lenyewe, kwakuwa si rahisi kuelezeka ama sababu nyinginezo. Lakini kwa mahakama kufika na kuona mazingira, basi kila kitu kitajieleza chenyewe.

Hata hivyo, huwezi kuomba mahakama itembelee eneo la mgogoro kama kesi ipo hatua ya rufaa. Hii ni kwasababu hatua ya rufaa ni hatua ambayo sheria hairuhusu ushahidi mpya kutolewa. Kwahiyo kama unahitaji kuomba jambo hili ni vema uliombe mapema kabisa kule kesi ilipoanzia.

Kwa mahakama za ardhi kesi inaweza kuwa imeanzia baraza la ardhi la kata, au imeanzia baraza la ardhi la wilaya, au imeanzia mahakama kuu. Popote itakapokuwa imeanzia unayo haki ya kuomba mahakama itembelee eneo la mgogoro ili iweze kujiridhisha katika kile unachosema.

Aidha, sio migogoro yote ya ardhi inahitaji kutembelewa na mahakama. Mgogoro kama umenyooka una ushahidi na mashahidi wa kuweza kuthibitisha na kila jambo likaeleweka, basi hamna haja ya kuomba kutembelea. Lakini ikiwa kwa mtazamo wako unaona kuna jambo hata likielezwa haliwezi kueleweka mpaka mahakama ifike na kuona basi utaomba.

Unapoomba mahakama nayo itapima na kuona iwapo kuna umuhimu wa kufanya hivyo ama hapana, bali kila kitu kinaweza kuishia ndani ya mahakama. Katika kutoa uamuzi wa kutembelea ama hapana mahakama itaongozwa na misingi ya sheria iliyowekwa ikiwemo ile iliyoelezwa katika kesi ya Evelyn Even Gardens NIC LTD and the Hon.Minister , Federal Capital Territory and Two Others, No.FCT/HC/CV/1036/2014;Motion No. FCT/HC/CV/M/5468/2017 .

 

Misingi ni pamoja na;-  Kama kutembelea eneo kutawezesha kuondoa mashaka juu ya kinachobishaniwa, Kama mgogoro unahitaji utambuzi wa mipaka, majirani na ukubwa au kiwango cha eneo,na  Kama ubishi unahusu hali halisi ya eneo, na jingine lolote ambalo mahakama itapima na kuona linafaa kuisukuma itembelee.

Misingi hii pia imeelezwa katika kesi ya MARTIN MGANDO vs MICHAEL .F. MAYANGA , Rufaa Namba 93/2019, chini ya Jaji Bahati.

Nisisitize tu kwamba mahakama inaweza kuamua yenyewe(sua moto) kutembelea eneo la mgogoro bila kuombwa na mtu yeyote. Hata hivyo ni muhimu wewe uliye kwenye kesi mlalamikaji ama mlalamikiwa kuwa wa kwanza kulianzisha hili ikiwa unaona ni la muhimu. Hii ni kwasababu wewe ndiyo mwenyue kesi ambapo matokeo mabaya ama mazuri yanakuja kwako. Kwa leo yatutoshe haya.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MWANDISHI  WA MAKALA YA SHERIA KUPITIA GAZETI  LA JAMHURI KILA JUMANNE.  0784482959, 0714047241bashiryakub@ymail.com

 

JE WAJUA KUMILIKI LAINI YA SIMU ZAIDI YA MOJA NI KOSA NA ADHABU NI KIFUNGO ZAIDI YA MWAKA MMOJA JELA.

|0 comments

 

HABARI ZA JAMII YA WAKAZI WA MKOA WA RUVUMA: WAKULIMA WA KIJIJI CHA  NAKAHUGA SONGEA VIJIJINI WANUFAIKA NA KILIMO CHA MPUNGA

NA BASHIR  YAKUB -  

JE WAJUA KUMILIKI LAINI YA SIMU ZAIDI YA MOJA NI KOSA NA ADHABU NI KIFUNGO ZAIDI YA MWAKA MMOJA JELA.

Bashir Yakub, WAKILI.

+255714047241

Huwa nawaambia kila siku kuwa jambo mpaka likukute ndo utajua kuwa lipo. Na nyote si mnajua kuwa kutokujua sheria sio kinga/hoja/udhuru. Hautafikishwa mahakamani ukasema nilikuwa sijui, halipo hilo.

Kanuni ya 18  ya GN. No.112/2020 Kanuni za Mawasiliano ya Posta na Simu(usajili wa line za simu) inakataza mtu kumiliki laini ya simu zaidi ya moja kutoka mtandao mmoja.

Kosa hili adhabu yake ni  kifungo kisichopungua mwaka mmoja jela au faini isiyopungua milioni tano au vyote kwa pamoja. 

Kwa kipindi hiki tulichomo yawezekana kosa hili ni kati ya makosa yanayotendwa sana na wengi. 

Kwa mujibu wa sheria hii kampuni pekee ndo yenye uwezo wa kumiliki line za simu kufikia hadi 30.  Mtu binafsi hata line mbili za mtandao mmoja ni kosa.

Hili sio kosa la madai ni jinai tuelewane hapa. Hili jambo ni serious. Wengi mnazo line hadi tano, ni basi tu siku yenu haijafika.

Nyongeza ya adhabu nilizotaja hapa juu, kanuni inasema pia ukikutwa na hatia utatakiwa kulipa Tsh 75,000/= kwa kila siku ambayo umemiliki hiyo Laini au kila siku ambayo umeitumia.

Kwahiyo upige hesabu kama umemiliki miaka 2 basi ni Tshs 75,000/= mara kila siku katika hiyo miaka 2.  Sikwambiii kama unayo miaka 5 au zaidi.

Hii ni nyongeza ya zile adhabu za juu. Yaani baada ya kupewa zile adhabu za juu sasa unahesabiwa hizo siku ambazo umekaa nayo ili ulipe.

Incase mtu anakutafutia kosa hapa hawezi kukukosa. 

Haya mambo yapo tukipata mda tuelezane tu kama hivi.